Monday, September 26, 2011

UWAZAJI CHANYA

Je umewahi kujiuliza, kwa nini kuna hisia tofauti- tofauti juu ya janga fulani? Kwa nini majanga kama kupoteza ndugu, mafuriko, n,k upokewa kwa hisia tofauti na wahanga?

Hii ni kwa sababu watu hupokea na kuchambua taarifa kwa namna tofauti, wengine chanya na wengine hasi.

Watu wanaochukua majanga kwa mtazamo chanya wanafaida zifuatazo:
-huimarisha mahusiano yao na jamii inayowazunguka
-huongeza ufanisi katika taaluma, kazi n.k
-huimarisha kinga ya mwili
-hupunguza maumivu ya ajali na majeraha mengineyo

Je Mtu Anawezaje Kuwaza Chanya?

Kukataa mawazo hasi ni hatua muhimu na ya awali kwa mtu yeyote anayetaka kuwa na furaha na ustawi maishani.
Uwaji chanya unafaa uwe wa kudumu, na si wakati wa matatizo au baada ya ushauri kutoka kwa wanasaikolojia na wataalamu wa akili.

Ili kuwaza chanya, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa kipindi chote cha maisha ya binadamu.

1) Uwazaji chanya juu ya mtu binafsi.
Epuka kuishi kwa kujilinganisha na watu maarufu kwenye TV, jamii n.k.

Kipimo cha mafanikio kiwe ni malengo na si mafanikio ya wale uliozaliwa nao, uliosoma nao, uloanza nao kazi n.k.
Yakubali mapungufu yako, na dhamiria ili hayo mapungufu yasitokee tena maishani.

2) Kuwaza chanya juu ya yaliyopita.
Historia haibadilishwi, ikubali hata kama ina chembechembe nyingi za uchungu.
Kuilaumu historia kana kwamba ndiyo iliyopelekea hali ngumu uliyo nayo haisaidii chochote!!
Mfano, kama baba angenipeleka shule...., kama fulani asingenisaliti... n.k

Kumbuka yote mazuri yaliyotokea nyuma, yatakusaidia na kukupa ujasiri wa kufanya maamuzi.
Kwa mfano, wazazi wamenipa malezi bora, kusalitiwa kumeniimarisha n.k
Kumbuka mawazo, mitizamo na mawaidha ya wazazi, marafiki n.k ingawaje hawapo duniani.

3) Kuwaza chanya juu ya yajayo.
Kesho inatengenezwa na mitizamo yako ya leo. Ukiwaza kwa ujasiri na kijiamini kuhusu kesho kunaongeza uwezekano wa kufanikiwa.

Hata kama changamoto zitatokea utaweza kuzikabali, kuwa na mipango sahihi bila ya malalamiko na hasira.
Mfano, nimefeli mtihani! Akili imefunguka na ntasomea ufundi kisha kujiajiri binafsi.

4) Kuwaza chanya juu ya watu na mazingira.
Kumbuka hakuna kilichotimilifu, ila kuna mema na matamu katika kila mtu na mazingira.

Usijenge hasira juu ya watu na mazingira fulani, amini watu na mazingira huku ukifanya jtihada kukabiliana na changamoto.

Jitahidi kuelewa kwa undani watu na mazingira husika.
Jiulize je, ni watu wote walio katika mazingaira fulani (mfano mijini) wamefanikiwa?

Jenga imani na wote wanaokuzunguka (marafiki, ndugu, majirani n.k) na kuchukua mawazo na changamoto wanazotoa kama mtaji kwako. Na hatiamye.

5) Mshirikishe Mungu.
Jaza moyo wako mawazo ya kiimani kwa kumtanguliza Mungu, kwani dini (imani) zote zinajenga utulivu wa akili.
Amini ya kwamba kufanikiwa ni kwa ajili ya binadamu wote, watu wote ni sawa mbele ya Mungu. Mruhusu Mungu akupe silaha na nguvu za kupambana na hila zote kutoka kwa waovu.

Monday, September 19, 2011

Mawazo Yako Ndio Mtaji Wa Maisha Yako

Upo uhusiano mkubwa sana baina ya namna mtu anavyofikiri na jinsi anavyoishi. Kushindwa kwa mtu hakutegemei nguvu yoyote aliyonayo isipokuwa ufahamu wa mtu husika.
Kuanguka kwa mtu hakutegemei idadi ya maadui aliyonao, isipokuwa aina ya mtazamo aliyonao. Kurudi nyuma kwa mtu (kiuchumi, kijamii n.k) hakutegemei historia aliyowahi kuwa nayo mtu husika, isipokuwa uendekezaji wa mawazo ya kushindwa.

Binadamu huongozwa/hujengwa na mawazo, mawazo ambayo yanapatikana katika mazingira husika.
Kwa kawaida mtu anapoona, anaposikia au jambo linapomtokea yeye mwenyewe, akili yake humpa tafsiri tofauti-tofauti juu ya jambo husika. Fikira hizo zinampa mtazamo fulani (- au +) katika maisha yake.

Mawazo hayo, baada ya muda huwa yanajitokeza katika maneno yake na hata katika matendo yake. Hivyo mtu huzugumza kufanikiwa au kutofanikiwa na baadaye kukifuatiwa na matendo.

Ni sawa na kusema kufanikiwa au kutofanikiwa ni suala la kimtazamo kuliko kuwa nacho au kutokuwa nacho.
Mifano ya kufanikiwa ni kama kuwa na; marafiki, upendo maadili mema n.k. Kwa upande mwingine kutofanikiwa ni kama kuwa na; huzuni, umasikini, maadui, n,k. Mawazo ndiyo asili ya hali inayoonekana kwa nje.

Kuna mifano michache:
¤Mark (26) aliamini anaweza kufanya biashara lakini hajui pakuanzia. Siku moja alihudhuria semina yenye lengo la kujenga uwezo wa vijana juu ya ujasiriamali.
Mazingira ya ukumbi, ufasaha wa lugha kutoka kwa wahadhiri, mifano halisi kutoka kwa wajasiriamali wazoefu n.k viliamsha hari ya Mark juu ya kuanzisha biashara.
Kuanzia hapo, Mark akatafuta ushauri zaidi, akatembelea maduka ya jumla, akatafuta mtaji kutoka kwa marafiki zake kisha kuanzisha biashara ya kuuza viatu vya mtumba.
Biashara ambayo imebadilisha maisha yake na ya familia yake.

¤Halima (27) alitoka kwa chakula cha jioni na rafiki zake watatu aliosoma nao high school.
Walifurahia mazungumzo, mazungumzo yaliyohusu mambo na matukio muhimu katika maisha ya sekondari, chuo na hata kazini.
Katika maongezi na michapo na michapo, Halima akaoanisha maisha yake na yale ya rafiki zake ndani ya miaka nane. Hatimaye akaona ya kwamba rafiki zake wanabahati zaidi yake. Ghafla akakumbwa na huzuni ukifuatiwa na msongo wa mawazo na kukosa usingizi kwa siku kadhaa.

Mtu akitaka kubadili hali yake (ya uchumi, mahusiano, kazi n.k) anapaswa kudhibiti yote anayoyaona au kusikia juu ya hali yake ya sasa, pamoja na hayo anahohubiriwa na mazingira yanayomzunguka.

Ni lazima kuchuja kile kinachoingia akilini kupitia milango ya fahamu. Chujio lako liruhusu mawazo chanya tu! Mawazo chanya (furaha, upendo, ushirikiano n.k) ni mbolea/mtaji katika jihada za binadamu za kujiletea maendeleo.