Monday, October 31, 2011

NYAKATI KATIKA MAISHA

Mtu anapaswa kufahamu ya kwamba katika kukua kwake lazima apitie nyakati/ hatua tofauti. Ili kufahamu hilo mambo manne yanahitajika kueleweka kwa kina, mambo hayo ni yafuatayo.
Maisha ni bustani.
Maisha ni bustani ambayo ina maua mazuri (muelekeo chanya). Kama mtunza bustani (mtu husika) asipofanya jitihada kuondoa magugu (mawazo hasi) maguugu hayo huua maua.

2) Kila tendo lina matokeo.
Katika maisha kama mtu asipokuza kipawa alichopewa na Mungu vyema na kama mtu asipochukua hatua za makusudi kipawa chake kitatoweka.

Kwa kila analowaza na kutenda mtu lina madhara (ya kukuza au kudidimiza ) kipaji chake. Kama mtu akikaa kimya, ulimwengu humchagulia na daima humchaguila mabaya

3) Kila kitu kina wakati.
Maisha yana nyakati/ hatua, nyakati/ hatua ziko katika mtiririko. Nyakati zinadumu kwa kipindi cha miaka 20 -25. Kama mtu atashindwa kumudu changamoto za wakati haua fulani, mtu huyo atakuwa na kipindi mgumu sana mbeleni.

4) kuna kani mbili katika ulimwengu.
Takribani vitu vyote vinavyotokea katika maisha hutegemea nguvu za binadamu. Kila anchofanya binadamu huzaa wema au ubaya. Wema au ubaya ndio matokeo ya kazi za binadamu.

Hatua Anazopita Binadamu Katika Maisha

1)
Wakati wa elimu
Hii ni hatua ya kwanza, hatua hii huanza mwaka 0 mpaka 20 - 25. Katika hatua hii binadamu hujifunza misingi na kanuni muhimu za maisha. Mtu hujifunza kwa kusoma, kuandika, kuhesabu, kufikiri na kufanya maamuzi.

Mtu hujenga taswira binafsi, kujiamini, imani, woga, ujasirii n.k. Mtu hupata elimu/ ufahamu kutoka kwa wazazi/ walezi, waalimu, au mtu yeyote aliye karibu.
Kama hatua hii itajengwa kwenye misingi imara ya ukweli, uungwana, nidhamu, upendo, n.k hakuna kitakachomshinda mtu maishani.

2)
Hatua ya hisia na mihemko.
Hatua hii ya pili huanza miaka 20 - 25 mpaka miaka 40 - 50. Katika hatua hii mtu huanza kukumbana na changamoto za maisha, channgamoto za utu uzima kama mapenzi, vilevi, kazi n.k. Watu wengi huangusha/ kushindwa na hatua hii. Katika hatua hii tabia zinaweza kumjenga au kumbomoa mtu.

Wanaume huangushwa na hisia zinazoletwa na ulevi, mapenzi, kutaka kutawala n.k. Ili hali wanawake huangushwa na hisia zinazoletwa na kutaka kupata utulivu wa kimapenzi (kupendwa)

Ili kumudu hatua hii mtu anapaswa kujenga programu ya kipato, programu ambayo itamhakikishia mapato hayazidi matumizi. Mipango yote ya pesa ibajetiwe, kuwe na fungu la matumizi ya kawaida na la uzalishaji (uwekezaji au kukuza kipato). Mtu atumie fursa zinzotolewa na makampuni kama kununua hisa, biashara ya mtandao, kununua fedha za kigeni n.k ili kumhakikishia kipato siku za baadaye.

3)Hatua ya kuwa na nguvu.
Hatua hii ya tatu huanzia miaka 40 - 50 mpaka 60 - 65. Katika hatua hii mtu hufikia hatua ya hali ya juu ya mafanikio au kushindwa.
Mtu huonyesha kumudu au kutomudu mbinu za kufanikiwa.

Changamoto kubwa katika hatua hii ni kuchagua kuwa mwema au mbaya. Watu hulazimika kurudia masoma ambayo hawakuyamudu katika hatua za nyuma. Hupata changamoto ya kukabiliana na misukosuko ya kimaisha ambayo inahitaji nguvu nyingi na suluhu la haraka.

4)
Hatua mgando.
Hatua hii huanza mika 60 - 70 mpaka 100 na kuendelea. Mtu huchanganua alichofanya na kuvuna katika kuishi kwake, hutafuta mbinu za kufanya matunda ya kazi zake yadumu milele hata milele.

Mtu hutaka kuona kazi za mikono yake hazifi na ndoto zake zinadumu daima. Hali hiyo husisimua nguvu za nafsi, mwili na akili kwa kiwango cha juu. Mtu haogopi wala kutishwa na changamoto zinazomkabili na yuko tayari kufa akipigania anachotaka.

MIAKA ILIYOTUMIKA NI YA WASTANI KWA WATU WALIO WENGI, KWA BAADHI YA WATU BAADHI YA HATUA HUCHUKUA MIAKA MICHACHE SANA LAKINI WATU WOTE HUPITIA HATUA ZOTE.

Monday, October 24, 2011

NJIA 12 ZA KUKUZA TASWIRA BINAFSI

Ili kukuza na kuimarisha taswira binafsi, inampasa mtu kutumia njia zifuatazo wakati wote wa maisha yake hata kama atapata mafanikio mapema.

1) Kuwa mwaminifu.
Yapasa mtu kuwa mwaminifu, uaminifu unaoanzia moyoni. Yapasa kuweka nadhiri ya uaminifu kati ya nafsi ya mtu na yale ayatakayo (malengo).

Hii itamfanya mtu kuwa makini wakati wote anapohusiana na jamii inayomzunguka, vitendea kazi, na mazingira husika.
Ili kuona ukuu na umuhimu wa kutofanya makosa ya kizembe.

2) Kujenga taswira.
Taswira ni ramani au picha ya yale mtu ayatakayo, ni hatua ya kwanza katika uumbaji.
Taswira ya matarajio inaweza kujengwa kwa kusoma, kujihusisha na watu wanaoona vyema mbele na ambao wanaoweza kukuza ufahamu.

3) Kupumzika.
Kupumzika ndio moja ya njia sahihi ya kupunguza/ kuondoa msongo mawazo.
Mtu anaweza kupumzika kwa kwenda mazingira taofauti na yale aliyoyazoea, kuomgea na watoto wadogo n.k

Msongo mawazo hupunguza nishati na kinga ya mwili na kupelekea ugonjwa. Ugonjwa unashusha / unapunguza makadirio ya mafanikio.

4) Kuwa na imani ya ushindi.
Imani a ushindi ni hisia kali anayokuwa nayo mtu juu ya kukamilisha kitu fulani na kuona matunda yake.

Imani ya ushindi huonyeshwa na jinsi mtu anavyoongea, anavyotenda na anavyoishi.
Imani ya ushindi huvuta hisia za watu, watu huwa tayri kutoa msaada wa hali na mali ili kufanikisha malengo ya mtu husika.

5) Kujenga tabia njema.
Tabia na mienendo hukua na kuimarika baada ya muda mrefu, baada ya urudiaji wa mara kwa mara kwa mara.
Tabia jema ni zle zinazopelekea: afya njema, mapumziko sahihi, mlo kamili, mazoezi ya mwili na uwazaji sahihi.
Mtu hujenga tabia, tabia humjenga mtu.

6) Kuamua kuwa na furaha.
Kuwa na matarajio mazuri kila siku, kutarajia kila siku kuwa ya furaha huamuliwa pindi mtu anapoamka na kutaka kufanya kila kitu kwa amani.

Kudhamiria mema na mazuri wakati wote. Kama mtu atdhamiria kila siku kuwa njema, basi mtu huyo hujenga usumaku na mema aliyoyatarajia.

7) Kujivua gamba.
Gamba ni hali inayomjenga na kumlinda mtu dhidi ya watu wengine.
Lengo lake ni kuficha hali halisi ya mtu husika.
Ni kama uigizaji kana kwamba mtu anavaa husika usio wake. Mfano masikini kutumia pesa kidogo alizopata na watu matajiri na maarufu ili kuficha umasikini.

8) Kuwa na hisani.
Lazima kutambua hali halisi, matatizo na mahitaji ya wengine, na kuwa tayari kutoa msaada.
Mtu anapaswa kusaidia wenzake ambao hawajafanikiwa baada ya kupita hatua kulani ya mafanikio.
Kufanya hivyo humweka mtu karibu na Muumba na huinua utu wa mtoaji na mpokeaji.

9) Kuimarika kutokana na makosa.
Makosa ni masomo kimaisha kwa wenye busara.
Mtu anapaswa kujifunza kupitia makosa ya wengine (ili asianguke walikoanguka wanzake) na sio kufanikiwa kwao.

Pia kujifunza kupitia makosa aliyoyafanya mtu kwa uchambuzi wa kina ili kupata sababu za kukosa.
Kutumia makosa (yako na ya wengine) kama njia kuelekea mafanikio.

10) Kukubali udhaifu.
Kama mtu hatakubali udhaifu alionao kamwe hawezi kuushinda. Mtu asipokubali madhaifu yake hawezi kujua chanzo chake na hawezi kuchukua hatua za makusudi ili kuweka mambo sawa. Kutokubali kushindwa lili kujipanga zaidi hukuza ukubwa wa tatizo.

11) Kujikubali.
Kama mtu hatajikubali/ kuikubali hali yake au mtu atajifananisha na watu wengine, basi mtu huyo hutaka kujitenga na hali yake, nguvu zake na hisia zake.
Mtu ambaye hujikataa (hujisaliti) hawez kujua yeye ni nani na ana thamani gani.

12) Kuendelea kukua.
Maisha ni mchakato wa kupitia furaha, huzuni, magumu, changamoto n.k
Mtu anapaswa kukua kwa kpitia uelewa wa kina na uthubutu wa kufanya maamuzi, hasa maamuzi magumu (maamuzi yanayoamua mustakabali wenye heri) wakati wa changamoto.

Wednesday, October 19, 2011

TASWIRA BINAFSI

Taswira binafsi ni jinsi mtu anavyojifafanua mbele za watu. Ni picha ya mtu binafsi anayoionyesha mbele ya watu wengine. (mimi ni nani?).
Taswira binafsi inampa mtu uwezo wa ktoa, kupokea na kukabiliana na changamoto za kimaisha.

Taswira binafsi inayojengwa kwenye misingi ya woga, wasiwasi, kutokujiamini n.k huonyeshwa kwa hisia hasi.
Taswira binafsi iliyojengwa kwenye misingi ya upendo, heshima, imani, uelewa n.k huonyeshwa kwa hisia chanya.

Vitu Vinavyoathiri Taswira Binafsi

Kuna viti vitatu vikuu vianavyoathiri taswira binafsi ya mtu.
1) Mawazo na hisia wakati wa utoto.
Katika miaka saba ya kwanza, watoto hujenga mfumo wa kuthaminisha na ambao huongoza maisha yao yote.

Watoto hupenda na kutafuta mafundisho mazuri, mawazo mazuri, hisia nzuri na mienendo chanya.
Kwa bahati mbaya, hawana kinga dhidi ya mawazo mabaya, mafunzo mabaya na mienendo hasi.
Kwa kutokuwa na uwezo wa kuzia maovu, mawazo na matendo ovu huwatawala na kudumaza ukuaji wa taswira binafsi iliyo bora.

2) Mazingira
Mazingira yana mchango mkubwa sana, kwani ndio chanzo cha uthibitisho wa yote mtu aliyojifunza utotoni.
Mtu anapokuwa katika mazingira fulani kwa muda mrefu huchukua/ kufanana na tabia za mazingira husika.

Kamataswira ya mtu inakinzana na mazingira husika, kuna machaguo matatu:
¤ kubadilisha mazingira
¤ kubadilisha taswira binafsi
¤ kuondoka katika mazingira.

3) Makundi.
Makundi huleta ufanano. Makundi chanya husaidia kukuza taswira binafsi kwa; kuchambua mambo kwa kina, kukuza uelewa, maana n.k
Makundi hasi hudumaza taswira binafsi ya mtu kwa; kuzuia kutafuta habari, kuzuia kufikiri, kusistiza "haiwezekani" n.k.

Tabia Tano za Watu Wenye Taswira Binafsi Iliyo Duni.

Watu wenye ufinyu wa taswira binafsi ni wengi, kwa bahati mbaya zaidi wengi wao ni vijana.
Watu hawa wana/huonyesha sifa zifuatazo.

1) Kukwepa majukumu.
Watu hawa hukwepa kuchukua majukumu yao, hukwepa wajibu au matokeo ya yale waliyoyafanya.
Kwa mfano, mvulana anaposababisha ujauzito na kuamua kumsaliti msichana husika.

Kama mtu asipochukua majukumu yake, kamwe hawezi kubadili hali aliyonayo hata kama anaichukia sana. Mfano, mtu hawezi kupata mafanikio ikiwa ataacha kufanya kazi kwa bidii na kubaki kuilaumu serikali tu.

2) Kukimbia changamoto.
Mtu anapokumbana na changamoto, kuna machaguo matatu; kupambana, kusahau, na kukimbia.
Mtu mwenye ufinyu wa taswira huamua kukimbia changamoto husika. Mfano, kijana anapoamua kukimbia nyumbani baada ya kutofautiana na wazai/ walezi.

Mtu ataimarika kama tu! Atakabiliana na changamoto husika. Kukubali na kukabili changamoto huleta ujasiri na imani na kumwezesha mtu kukabliana na changamoto nyingi zaidi.
Je mtu atakimbia chanagamoto ngapi ili afanikiwe?

3) Kukosoa muada wote.
Watu wenye upumgufu wa taswira hutafuta mtu/watu wa kukosoa pindi makosa yanapotokea.
Watu hawa hukosoa kila kitu bila hata kuonyesha chembe ya kujenga, uungwana, heshima n.k.

Kukosoa kwa chuki hubomoa sio tu mkosolwe bali hata mkosoaji.
Kukosoa kunakojenga huambatana na upendo, heshima, utu n.k. Husaidia kujenga na kuimarisha watu wenye mapungufu. Huwafanya watu (mkosoaji na mkosolewaji) wakubalike katika jamii husika.

4) Husubiri watu watoe suluhu ya changamoto.
Watu wenye taswira binafsi duni hukaa na kusubiri rafiki, ndugu n.k watoe suluhu ya changamoto zinazowakabili. Kwa mfano, kijana anasubiri wazazi wamtafutie kazi.

Kama mtu atasubiri watu wampatie majibu ya changamoto zinazomkabili, mtu huyo kamwe hawezi kukua na kuimarika kwani kufanikiwa au kutaofanikiwa kunamuimarisha mtu.

5) Kupuuzia mambo.
Watu hawa huishi kana kwamba kila kitu ni sawa (OK!). Hujisahaulisha changamoto zinzowakabili. Huona hakuna haja ya kuwaza mbinu mbadala ili kuboresha hali husika. Huamini kila kitu ni sawa na inatosha, hakuna haja ya kuumiza kichwa zaidi.

Mfano, mtu anagundua amekosea moja ya hatua katika kufanya kitu fulani, kisha anajisemea haina tatizo, hata fulani alikoesea n.k. Hachukui hatua ili kurekebisha hatua husika hata kama anao uwezo wa kufanya hivyo.

Monday, October 10, 2011

SIRI RAHISI INAYOWASHINDA WENGI

Je, unayotabia ya kuandika malengo na kuyafanyia kazi? Kujiwekea malengo ndio mbinu kuu na sahihi ya kufikia mafanikio yoyote yale! Mbinu hii hutumika katika katika mipango yote, ya muda mfupi na muda mrefu. Kuandika matarajio ni kama kuchora ramani ya njia kuelekea kule mtu anakotaka kufika.

Kuandika malego kumewafanya watu wa kawaida kuwa watu mmarufu na muhimu katika jamii, vivyo hivyo kutoandika matarajio kumeshusha vipawa vya watu wenye uwezo.
Watu wengi wanajua ya kwamba kuandika malengo yao ni hatua muhimu kuelekea kwenye mafanikio yoyote yale lakini hawafanyi hivyo.

Kazi ngumu na yenye manufaa ni "kuamua". Inahitajika nguvu kidogo kufamya mambo makubwa lakini inahitajika nguvu kubwa kuamua mambo makubwa. Kufanya maamuzi ni kazi ngumu na inaathiri maisha ya watu wote. Kuwa mtu sahihi hutegemea maamuzi sahihi.

Mtu anahitaji zana sahihi ili kufikia malengo. Zana hizo ni KALAMU na KARATASI. Watu wako tayari kutembea umbali mrefu ili kukwepa kazi ya kuandika, wanaweza kuwaza, kuongea n.k lakini hawako tayari kuandika.

Hii ni kwa sababu kuandika kunahitaji kuwaza kwa kina. Kama huamini, jaribu kuanika chochote ndani ya sekunde kadhaa bila ya ya kufikiri.

Kuandika kuna nguvu mara kumi zaidi ya kuongea. Kuandika kunaanmsha seli za ubongo zilizolala na kumlazimisha mtu afikiri kwa kina na kwa ufasaha.

Kama mtu hajandika malengo yake, basi afahamu ya kwamba hayuko makini (serious). Kuwaza bila kuandika hufutika baada ya dakika chache lakini kuwaza na kundika hakufutiki kamwe!

Kitendo cha kuandika unayotaka ni kama kuwasha sakiti ya umeme kunavyopelekea taa kuwaka, mashine kufanya kazi n.k. Nusu ya tatizo litakuwa limepatiwa ufumbuzi kama mtu ataandika mbinu anazoamini ndio sahihi na jinsi ya kuzitekeleza.

Kuandika huleta nguvu ya ajabu inayoondoa woga, inayoleta matumaini na ujasiri. Kuandika malengo kunamfanya mtu kuchukua hatua ili kuyafikia, hubadilisha mtizamo na muonekano wa mtu husika.

Kuandika malengo kunagharimu dakika chache, huokoa zaidi ya miaka ishirini ya kuwa na matrajio (ndoto).
Kuona malengo yaliyoandikwa kwenye karatasi kunagonga kengele inayomtaka na kumlazimisha mtu kufanya jambo lolote ili kufikia lengo/malengo.

Mtu anatakiwa kujiwekea lengo/ malengo machache ili iwe rahisi kuyafanyia kazi mfano; "nataka kuwa mwandishi", "nataka kuwa mfanyabiashara" au "nataka kuwa mkulima" n.k.
Lengo /malengo hayo yaandikwe na kuwekwa sehemu tofauti-tofauti ambazo ni rahisi mtu husika kuona na kusoma mfano; kitandani, mezani, jikoni, mfukoni n.k.

Kisha lengo/malengo yasomwe kila siku asubuhi na jioni (kabla na baada ya kulala), huku mtu husika akiwaza kufanya jambo lolote siku inayofuata ili kufikia lengo.
Mtu anahitaji kukumbushwa zaidi kuliko kufunzwa.

Mbinu nyingine zinazohusiana na kuandika malengo ni:
-kujiambia kwa sauti katika maeneo tulivu "nitafanikiwa"
-kuangalia mafanikio ya watu waliokuwa na lengo/malengo sawa
-kusoma machapisho ya watu waliofanikiwa mara kwa mara
-kuongea na watu sahihi na wenye malengo sawa
-kusoma machapisho juu ya lengo lako
-kusikiliza mihadhara, radio, CD n.k
kujihusisha na watu wenye mafanikio.

Monday, October 3, 2011

HATUA SITA ZA KUWA JASIRI

Watu wengi wana uwezo wa kufanya mambo makubwa na yenye kuleta mafanikio, wanakosa mafanikio kwa kuwa hawana ujasiri wa kuwaza na kufanya maamuzi.
Njia zifuatazo zinasaidia kuimarisha uwazaji na kuwezesha kuchukua hatua zitakazowezesha kufikia malengo.

Hatua Ya 1: Chukua Hatamu Ya Maisha Yako
Kujali kile watu wanachosema juu yako ni kuwapa nafasi watu wayaongoze maisha yako badala yako.
Kujali watu wanachowaza ni utumwa unaowakabili watu wengi. Wengi tumelelewa (kwa nia njema) tukijali mawazo ya wengine zaidi, kitu kinachopelekea kuwa katika maisha, kazi n.k yasiyo na furaha wala mafankio.

kutaka kuwaridhisha wengine wakati wote ni tatizo linaloanza utotoni ili kukubalika. Hali hii huimarika ukubwani kiasi kwamba mtu anakosa kujiamini na kutanguliza mbele kile wanachowaza wenzake na si matakwa au mahitaj yake. Hali hii hupelekea umasikinii wa mawazo na hatimaye wa kipato.

Kabla ya kufanya chochote , jiulize, je unafanya kwa makusudio yako au ili kuaridhisha marafiki, ndugu n.k?
Kufuata mawazo ya wengine kunamfanya mtu kuwa; mtumwa, kunaua ubunifu na kumaliza nguvu za kutekeleza malengo binafsi, kunazuia mtu kwenda anapotaka, kufurahia anachotaka na hatimaye kukosa mafanikio anayotaka.

Hatua ya 2: Jitahidi Kuwa Tofauti
Karibu kila mtu anajitahidi kuwa sawa (sawa na marafiki, tabia, tamaduni n,.k) ili apate kukubalika katika jamii husika.
Inapasa mtu kuchambua mienendo yote kwa kina kujua kama "usawa" anaoutaka utaleta mafanikio au la!
Kama ni wa kufuata mkumbo, hatua za haraka zichukuliwe ili kuepusha utumwa au utekwaji nyara na mambo yatakayorudisha nyuma jitihada za kimaendeleo.

Hatua ya 3: Tazama Mbele
Ikiwa mtu atabaki kulaumu makosa aliyofanya awali, ajue anaua kujiamini na kushindwa kusonga mbele. Makosa ni mazuri (mtaji) kama yatachambuliwa ipasavyo (yakichambuliwa chanya au kama somo)

Kama mtu anataka kuwa jasiri, asichukue makosa kama makosa bali, kama masoma muhimu katika maisha. Hii itasaidia kujenga mustakabali wenye mafanikio.
Ili kufanikiwa haipaswi kukatishwa tamaa na idadi ya makosa. Kukosa ni muhimu ili kujua nini cha kufanya au kutofanya wakati fulani. kufanikiwa au kutofanikiwa ni suala la kimtazamo.

Hatua ya 4: Amini "Bado Sijachelewa"
Kuna watu wengi hawapendezwi na kazi wanazofanya kwa muda mrefu, lakini wanakosa ujasiri wa kuziacha kwa kuwa wanahisi wamechelewa kuanza au kujifunza fani/kazi nyingine.

Kama mtu analo lengo fulani, lakini anajikuta akijiambia "nimechelewa", njia pekee ya kuvua woga huo na kuvaa ujasiri ni kutouzingatia na kukabili kile anachokiogopa kwa nguvu zote.

Hatua ya 5: Kutojiwekea Ulinzi
Kuna wasomi wengi wamekosa mafanikio kwa kuwa kila wanachowaza kufanya wanawaza kwa tahadhari ya hali ya juu. Hali ambayo inawanyima uhuru.

Kuna watu wanaoweza kufanya biashara lakini hawana ujasiri wa kuthubutu, wanaogopa hasara kama kuwaka moto, kuibiwa n.k hivyo hutumia muda mwingi kufikiria juu ya kampuni za ulinzi, bima au tahadhari nyingine.

Ili kuepuka kujiwekea ulinzi uliopitiliza inapaswa kuthubutu. Kuthubutu yafutayo:
¤kuthubutu kuwa kuwa peke yako
¤kuthubutu kuwa na mtindo wako wa maisha na si kufuata mitindo ya kundi fulani bila sababu za msingi
¤kuthubutu kusoma na kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha fani husika
¤kuthubutu kuwa na mtazamo chanya na ujasiri wa kujaribu.

Hatua ya 6: Amini Utafanikiwa
Daima dumu! Kufanikiwa au kutafanikiwa kunategemea mtu anavyowaza na kuamini. Hivyo ili kuwa na ujasiri mtu anapaswa kuamini kwamba kuna kufanikiwa, huku akifanya mambo yanayopelekea mafanikio.

Ili kuvunja minyororo na utumwa wa mawazo "nitashindwa" yafaa:
¤kuchati chanya kimoyo-moyo
¤kujihusisha na watu wanaowaza kufankiwa au waliofanikiwa
¤kuwaza "nami" naelekea kufanikiwa
¤kuwaza "mimi" ni mshindi.

Mtu anapaswa kujishawishi yeye mwenyewe. Watu humshauri mtu juu ya kufanikiwa baada baada ya yeye binafsi kujishauri.