Monday, November 28, 2011

AZMA KATIKA MAISHA

Azma ni jumla ya mambo yote ambayo mtu anataka maisha yake yawakilishe. Azma ya mtu huendana sambamba na fani (kazi) ya mtu husika.
Ikumbukwe ya kwamba kinachoangaliwa na jamii (watu wengi) si wingi wa miaka aliyinayo mtu au uzoefu bali, ni mchango wake katika maisha ya jamii husika.

Maswali ya msaada (mwongozo) anayopaswa mtu kujiuliza wakati anapoamua azma ya maisha yake katika jamii yoyote ile.
1) Je nataka maisha yangu yaweje?
2) Je naishi maisha sahihi?
3) Je nafanya nini ili kufanikisha maisha sahihi?
4) Je nafanya nini kila siku ili ndoto zangu zitimie?
5) Je nimetoa mchango gani kwa jamii?
6) Je mchango niliotoa kwa jamii ni sawa na jamii ilivyoniwezesha?
7) Je maisha yangu yatajizatiti kwa lipi?
8) N.k

Vigezo Saba Wakati wa Kujenga Azma.

1) Kamilifu.
Mtu anapaswa kutazama vitu kama vitakavyokuwa, na si kama vinavyoonekana.
Kutazama kwa mapana na marefu juu ya kila wazo au lengo alilonalo mtu. Mtu anapaswa kutazama huku akiangalia baadaye, je anachowaza kitafanikiwa?
"Daima tazama juu nawe utakuwa juu"

2) Kuwa na mwanga.
Azma ya mtu lazima itazame mbele, mbele ya ombwe na mbali na upeo wa macho. Mtu anapaswa kujifunza jinsi ya kuitikia, kukumbuka na kukubali "ndoto".
Mwanga huu ni mapokeo ya juu na ya ki-ujasiri. Mtu anayo mamlaka ya kutengeneza taswira kutoka kwenye mawazo aliyonayo kupitia mwanga huu.

3) Kudumu maishani.
Azma ni taswira ya mtu inayowakilisha majukumu ya mtu katika ngazi tofauti-tofauti alizonazo katika jamii. Majukumu aliyinayo mtu yanapaswa kudumu hata kama mwanzilishi hayupo duniani. Sifa hii imewafanya watu wengi wailioondoka duniani kukumbukwa mpaka kesho. Mfano; Martin Luther King Jr, Mwl J K Nyerere n.k

4) Kunufaisha kila mtu.
Azma inayolenga kumnufaisha mtendaji ni ishara ya wazi ya ubinafsi wa hali ya juu, ubinafsi unaotishia usalama na uhai wa jamii.
Azma inapaswa itazame watu wote katika jamii, inufaishe makundi yote ya wanajamii kuanzia; watoto, vijana, wazazi, wazee n.k.
Mfano, je biashara, taaluma n.k yangu ni kwa ajili ya nani?

5) Kushawishi.
Azma inapaswa wakati wote ishawishi imani na uwezo wa mtungaji. Inapaswa imshawishi mtu kufanya kila jitihada zilizo halali lili kutimiza azma husika.
Mfano, kama mtu anataka kuwa mfugaji wa kuku, azma ya kufuga kuku imshawishi atafute msaada kutoka kwa wafugaji, wataalamu wa mifugo n.k ili kufuga kuku kwa ufanisi na si kwa mazoea.

6) Kuchoma.
Azma ya mtu iwe kama moto, moto unaochochewa na imani ya kufanikiwa. Imani ya kufanikiwa huwa kama moto unaoamsha hisia na uwezo wa akili pamoja na misuli kana kwamba, mtu anakuwa na ujasiri na uthubutu juu ya vikwazo vyote vya kibinadamu.

7) Kuwa na manufaa.
Azma ya mtu inapswa kutimiza matakwa ya jamii na dunia kwa ujumla. Iwe na uwezo wa kukabili na ktoa suluhu dhidi ya changamoto zinazomkabili binadamu kwa wakati husika.
Azma inayolenga kuondoa adha kwa jamii hupata msaada kutoka sehemu mbalimbali duniani. Mfano, je azma yangu ya kufungua mradi wa kilimo itapunguza tatizo la ukosefu wa ajira katika jamii yangu?

Monday, November 21, 2011

MALENGO

Malengo ni kama mstari unaotoa mwelekeo (dira) wa mahali anapotaka kufika. Malengo humpa mtu sababu za kujiamini, hususani kama yakitimia.
Kujenga tabia ya kuweka lengo humfanya mtuasonge mbele kuelekea kokote atakako.

Aina Za Malengo.
1) Malengo ya muda mfupi.
Malengo haya ni ya karibu. Huwakilisha mahitaji yanayopaswa kutekelezwa ndani ya muda mfupi, bila hata kutumia nguvu na rasilimali nyingi.
Malengo huchukua kati ya siku moja hadi tisini ili kutimia.

2) Malengo ya kati.
Malengo haya hutegemea malengo ya muda mfupi ili yatimie. Hutegemea nguvu kiasi ili kutimiza malengo ya muda mfupi. Malengo haya huchukua kati ya siku tisini mpaka miaka miwili ili kutimia.

3) Malengo ya muda mrefu.
Malengo haya hutegemea/ huhitaji vitu vingi ikiwamo muda na rasilimali nyinginezo. Huendana na fani ya mtu. Malengo haya huhitaji mikakati na rasilimali nyingi, pia kukamilika kwa malengo ya muda mfupi na wa kati.
Malengo haya huanzia miaka miwili na kuendelea.

Malengo yanaweza kuwa edelevu au pinzani.
Malego endelevu ni yale ambayo hutekelezeka hatua kwa hatua, huanzia na hali aliyo nayo mtu, huchochewa na mafanikio ya kila hatua ya ya mafanikio.
Kwa upande mwingine malengo pinzani ni yale ambayo hutaka mafankip ya ghafla, hukinzana moja kwa moja na hali aliyo nayo mtu.
Kwa ujumla, malengo endelevu hutekelezeka kwa urahisi yakilinganishwa na malengo pinzani
Sifa Sita za Malengo Yanayotekelezeka.
1) Kuandikwa na kushirikisha.
Kila lengo linapaswa liandikwe katika sentensi mbili au tatu. Malengo yaandikwe kwa lugha fupi na fasaha ili mtu aweze kukumbuka mara kwa mara.

Mtu anapaswa kuwashirikisha watu/ mtu ambaye anaelewa na kuamini katika lengo fulani. Mfano mfanyabiashara, mwalimu, daktari n.k. Ushirikishaji hulazimisha uwajibikaji, huleta ushirikiano, pia humsaidia mtu kupata msaada na faragha wakati wa kipindi kigumu.

2) Halisia na kufikika.
Malengo yanapaswa kuwa halisia na yenye kufikika. Ili lengo liwe halisia na lenye kufikika linapswa kuwekwa kwa kuangalia maendeleo aliyofikia mtu na rasilimali (viwezeshaji) alizo nazo mtu kwa wakati anapopanga. Watu wengi kuweka malengo bila kuangalia viwezeshaji kama ushauri, fedha n.k, hali hupelekea utekelezwaji duni wa malengo.

3) Kukubali mabadiliko.
Mtu anapoanza kutekeleza lengo husika, vikwazo na vizuizi huibuka kutoka pasipotegemewa. Lengo linapaswa kukubali mabadiliko pindi hali inapobidi.
Kwa mfano mtu anaweza kubadilisha aina ya biashara ndani ya muda husika kwa sababu kukosa fedha, kupatwa na ugonjwa n.k.

4) Kupimika.
Malengo ni matunda mtu anayoyarajia kupata kutokana na juhudi zake katika uwekezaji. Malengo yanapaswa yawekwe sambamba na vipimo ili kuweza kufuatilia utekelezaji. Vipimo vinapswa kuwa hatua kwa hatua, hii itasaidia kugundua wapi na vipi maboresho yafanwe kuligana na hali husika.

Watu huweka malengo bila vipimo hatimaye madhaifu mazito na yasiyorekebishika huonekena baada ya muda na rasilimali nyingiezo kutumika. Hali hii ianapelaea hasara isiyozuilika.
Kuwa na lengo bila kipimo ni sawa na kutembea njia ndefu inayoelekea mji fulani pasipo kujua ina uerfu gani.

5) kufuatata muda.
Kunapaswa kuwepo muda maalumu katika utekelezwaji wa kila kipengele. Muda hutumika kupima ufanisi. Muda unaopangwa unapaswa uende sambamba na ujuzi, rekodi ya mafanikio ya mpangaji au ya watu anaojifunza kutoka kwao, viwezeshaji n.k

6) Kuwa na lengo mbadala.
Lengo la mtu ni hali anayoitaka mtu baada ya wakati fuani. Kuweka malengo ya ziada (mbadala) hutoa njia mbadala ikiwa hali itakuwa ngumu kiasi kwamba inazuia utekelezwaji ya lengo kuu.

Mfano mtu anapanga kuuza nguo, kama nguo zikidorora afanye biashara ya nafaka. Lengo mbadala linapswa litumie mtaji, maarifa au rasilimali nyinginezo zinazoendana na lengo kuu ili kupunguza gharama na usumbufu wakati wa kubadili.

WATU WENGI HUPANGA KUSHINDWA, NA SI KUSHINDWA KUPANGA.

Monday, November 14, 2011

KUWA NA FURAHA LEO UFAIDIKE LEO!

Leo ni siku ya siku ya kuacha kuishi kwa kutegemea kesho. Kwani leo ni siku ambayo hautaishuhudia tena katika maisha yako, hivyo unapaswa kuifurahia hata kama ni chungu kama shubiri au mwarobaini.

Watu wengi huairisha furaha zao wakisubiri malengo yao yatimie ndipo wafurahie. Baadhi ya watu husema watakuwa na furaha ikiwa tu:
¤ watapata kazi nzuri,
¤ watakapopata wapenzi wa maisha,
¤ watoto wao watakapokuwa wakubwa,
¤ watakapohitimu masomo,
¤ watakapostaafu kazi za ofisini,
¤ n.k.
Watu hutoa sababu nyingi kama hizo zinazowapelekea kuishi kwa huzuni, huzuni wasiyostahili.

Kwa kawaida lengo moja linapofanikiwa ghafla malengo mengine huibuka hivyo, kumfanya mtu kuishi akisubiri furaha maisha yake yote. Inafaa kupambana ili kuwa na maisha mazuri huku akifurahia kila hatua ya mafanikio anayopiga kuelekea hayo "maisha bora"

Mtu anapaswa kujua ya kwamba wakati alionao (siku, saa na dakika) hataushuhudia tena katika maisha yake, ikipita imepita.
Yaliyotokea kabla ya leo na yatakayotokea kesho ni vitu vilivyo nje ya akili ya mtu. Hali halisi ni ile mtu anayoishuhudia wakati husika, wakati ambao anawezakfanya jitihada ili kuleta mabadiliko katika maisha.
Jiulize kama usipokuwa na furaha leo je utakuwa nayo lini?

Kuna njia rahisi ya kumfanya mtu afurahie (siyo aridhike) na hali aliyonayo mayo ni KUJITAMBUA.
Mtu anapaswa kutambua hali ya uchumi yake, jamii yake na yale yote anayoshuhudia ikiwamo changamoto. Kuangalia mazingira yanayomzunguka, kusikiliza kwa makini sauti ya moyo wake na kila kinachoingia akilini mwake.

Kutambua pale mtu alipo hufungua akili na furaha huchukua nafasi ya huzuni. Huzuni inayoletwa na mtizamo hasi kuhusu jana na kesho. Kujitambua huleta hisia chanya na kuonyeha viwezeshaji, viwezeshaji ambavyo husaidia kufanikisha malengo kwa haraka.

Ingawaje mtu hana uwezo wa kuzuia ukweli wa yale anayoshuhudia lakini, anao uwezo wa kumiliki anachoshuhudia ili kimsaidie. Mtu anapaswa kuita furaha na ikaja haraka hata asivyotarajia.

Kwa mfano, kama ntu anajikuta anawaza juu ya upungufu wa kiungo/viungo katika mwili wake, asitishe mawazo hayo na aanze kuamini mambo yatakuwa sawa ikiwa tu atapenda kwani, yeye si wa kwanza na wala hatakuwa wa mwisho. Wapo wengi, watu wengi wenye mapungufu makubwa lakini wamefanikiwa na kuwa watu muhimu katika jamii zao.

Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya uwazaji wa mtu na homa. Mwili huathiriwa hasi na mfadhaiko wa akili. Maumivu yoyote ya nwili ni taarifa ya kwamba kuna kasoro na inahitaji suluhu.

Homa huibuka kwa sababu ya kupuuzia taarifa za mara kwa mara zinazotolewa na akili kuptia mwili. Hali inapokuwa mbaya ndipo mtu huchukua hatua za kubadili anavyowaza na kuanza kutibu maumivu.

Mtu anapaswa kuwa makini sana kwa kile mwili unachomwambia, pia kufahamu ya kuwa mwili na akili hufanya kazi pamoja. Akili ndio inayochukua hatamu za kuongoza mwili, ndiyo maana mtu akiwaza visivyo hupata homa ghafla.

Kama mtu atakuwa na mawazo chanya, anayotiba ya uhakika dhidi ya huzuni na homa. Tiba zote hutegemea hisia na mtazamo wa mtu (furaha) ndipo zitoe matokea ya haraka. Mtu anavyohisi juu ya jambo fulani, mfumo wa neva hutoa ishara zinazoathiri mfumo wa kinga ya mwili.
Kumbuka njia (kinga) bora katika kuzuia homa au kupunguza makali ya homa hata kama mtu anatumia dawa ni kuiamuru akili iite furaha.

Monday, November 7, 2011

UPWEKE

Mtu mwenye upweke hukumbwa na hisia za woga, woga ambao unazorotesha hali ya afya. Mara zote woga hujikita kwenye mahusiano ya mtu binafsi, mahusiano ya mtu na mtu/jamii, kazi, uchumi, afya na mustakabali kwa ujumla.

katika hatua za awali upweke unaweza ukamkumba mtu bila ya watu wengine kufahamu. Upweke na msongo wa mawazo ndio vikwazo vikuu kwa afya ya akili.
Kwa bahati mbaya hali ya maisha ya nyakati hizi huchangia kwa kiasi kikubwa tatizo la upweke pia hukuza ukubwa wa tatizo.

Jinsi ya Kuzuia Upweke.

Dalili za upweke hazionekani kirahisi, huonekana wakati tatizo limekua kubwa. Njia zifuatazo zinafaa ili kuepusha hali ya upweke.

1) Kuzungumza juu ya changamoto.
Kuzungumza na mtu sahihi ni hatua muhimu sana katika kutatua changamoto. Inafaa kumtafuta mtu wa karibu na ambaye anao uzoefu juu ya changamoto husika.

Watu wanaoishi peke yao (wenye kujitenga na marafiki, jamaa n.k) wapo katika hali mbaya zaidi, inafaa mtu kuwa na mahusiano mazuri na wale wanaomzunguka. Mawasiliano mazuri hufanikisha mazungumzo juu ya changamoto na huakikisha suluhu sahhihi inapatikana.

2) Mapumziko.
Kukosa au kuwa na mapumziko hafifu hukaribisha upweke, hivyo mtu anapaswa kupanga na kutumia muda hata kama ni kidogo kupumzisha mwili na akili.

Kuna njia nyingi za kufanya mapumziko kama; kutembelea wagonjwa, kwenda maeneo ya mbali, kufanya kazi za bustani, kuogelea n.k. Inategemea na muda mtu alionao, gharama, mapendekezo yake n.k

3) Kupumua.
Zoezi la kupumua ni rahisi na lenye mafanikio ndani ya muda mfupi. Kupumua hutumika kuondoa chembe za uchovu na upweke katika mazingira yoyote yale.

Zoezi lenyewe ni, kuvuta pumzi ndani taratibu huku tumbo (na si kifua) limetanuliwa, kisha kutoa hewa taratibu, zoezi lirudiwe mara tatu au nne mfululizo na mara mbili au tatu kwa siku, kadiri ya mapenzi ya mtu.

4) Kula sahihi.
Tafiti zimeonyesha ya kwamba kufungua kinywa kwa protini huondoa mawazo yanayofanana na upweke. Kufungua kinywa kwa protini kukifuatiwa na wanga, matunda n.k. Pia maji ya wastani wa glasi nane (inategemea na mazingira na aina ya vyakula) kwa siku.

5) Kujjihusisha na kikundi.
Inapaswa mtu kuwa katika aina yoyote ya kikundi, hususani kikundi kinachotoa mwamko, kikundi cha wakulima, wakina mama wajasiriamali,
n.k.
Katika kundi mtu anapata uzoufu kutoka kwa watu mbalimbali jinsi ya kupambana na changamoto za kimaisha. Hii inajenga ujasiri dhidi woga wowote ule.

6) Kutafuta habari kuhusu changamoto.
Mtu anapaswa kutafuta habari kutoka vyazo tofauti pindi anapohisi mambo hayaendi sawa. Kuna ushauri mwingi na wenye kufaa kwenye vitabu, majarida, CD/DVD n.k.

Habari sahihi huondoa wasiwasi kuhusu changamoto za kiafya, kikazi n.k. Kwa mfano mtu anaweza kupata ukweli juu ya vidonda vya tumbo, shinikizo la damu, kisukari n.k kwenye mtandao wa intaneti.

7) Kujiamuru.
Kujisemea maneno ya kutia moyo kama "hakuna kitakachotokea", naelekea kushinda", "Mungu wangu nipe amani, "Mungu uniodolee woga n.k kwa sauti na mahali tulivu.

8) Kuzuia mawazo.
Mtu anapaswa kuzuia mawazo yanayoleta woga au yanayoendana na woga. Mfano, mtu kuhisi anaugonjwa usio na tiba n.k. Mawazo kama hayo yanaonekana mapema, hivyo ni rahisi kuyazuia kwa kuyakataa.

9) Kuukabili woga.
Mtu anapaswa kumudu mbinu za kumpa ujasiri pale anapokumbana na hali tata na yenye kutisha. Hali aliyonayo mtu hutegemea jinsi anavyowaza hususani wakati wa changamoto, kukifuatiwa na uumbaji wa picha na baadaye upweke huota mizizi.

JIPIME
Jibu "N" kama jibu lako ni NDIO na "H" kama jibu lako ni HAPANA.
1) Je mapigo yako ya moyo yanaridhisha?
2) Je kama mtu akitaka kukukopa unashindwa kujibu "hapana"?
3) Je unapata jazba kwa mambo yasiyo na faida?
4) Je ni vigumu kusema "hapana" kwa muuzaji"
5) Je huwa unapata hofu bila sababu za msingi?
6) Je unaogopa sana na hali hiyo inakuuzunisha?
7) Je rafiki akikukosea unaweza kumwambia alivyofanya siyo sahihi?
8) Je unakataa au kuahirisha mikutano/mialiko?
9) Je mara zote unahisi kutoridhika?
10) Je unaweza kuhoji au kudai haki/stahili yako?
11) Je kama hujafikia muafaka na mpinzani wako unakaa kimya?
12) Je ni mzito kufanya maamuzi?
13) Je hutaki kupokea sifa?
14) Je mara nyingi unakuwa na hofu?
15) Je una uthubutu?
16) Je unaweza kuendelea na mazungungumzo na mtu baada ya kutofautiana?
17) Je unahisi kutoweza kutatua matatizo yako?
18) Je kama mtu akikupa upendeleo, unaweza kuukataa?
19) Je mara nyingi unafanya kazi kwa shinikizo?
20) Je kama hujaelewa kitu unaweza kuuliza hadharani?

UFAFANUZI WA MAJIBU.
¤ kama "N" ni kati ya 0 - 7, hauko kwenye hatari ya upweke.
¤ Kama "N" ni kati ya 8 - 12, upo kwenye hatari na unapswa kuchukua hatua (za hapo juu) ili kuweka mambo sawa.
¤ Kama "N" zaidi ya 12, ni mpweke, unapaswa kuchukua hatua na pia kumwona mwanasaikolojia kwa msaada zaidi.