Monday, May 28, 2012

FAIDA ZA KUTAFAAKARI JUU YA KIFO

Kwa mtu kuamua kuwaza juu ya kifo chake ni jambo zuri, tafiti zimethibitisha hivyo tofauti na mitizamo ya watu.
Watu wengi huogopa sana pindi wanapoona jeneza au kupita makaburini au kusikia juu ya msiba. Hivyo kujikuta wakitafakari juu ya maisha yao.

Kuna baadhi ya mitizamo hasi ya kwamba mtu anayetafakari juu ya hatima yake, na kuongea hakawii muda mrefu bila ya kufariki. Baadhi ya watu huenda mbali zaidi na kusema ya kwamba mtu anayekaribia kufa huona baadhi ya dalili ndani ya siku arobaini kabla ya kifo chake, hivyo kumfanya aongelee kufa.

Kuna faida nyingi sana kwa mtu anayamua kutafakari kwa kina juu ya kifo chake na jinsi mambo yatakavyokuwa baada ya kifo chake. Miongoni mwa faida hizo ni:

a) Kumfanya mtu ajione sawa na wengine.

Watu wenye mali nyingi, hadhi n.k hujisahau. Pindi wanapohudhuria misiba hupata nafasi ya kujishusha, hivyo kujiona hawana tofauti kubwa na wale wanaowazika, kwani hao wanaowazika hawakupenda kufa, pia wao hawajui kwa nini wapo hai na watakufa lini. Hivyo kuimarisha uhusiano baina yao na jamii.

Pia kwenye ibada za mazishi viongozi wa dini hupata wakati wa kuhamasisha watu waishi kwa upendo ili apate mapumziko mema baada ya maisha ya duniani.

b) Kusaidia kuimarisha afya.

Watu hukata shauri na kwenda hosptali au vituo vya afya ili kupata kuchunguzwa afya zao (mfano kupima VVU, malaria n.k) baada ya kuambiwa madhara ya matendo yao au hatari zinazowasonga, kiasi cha kutishia uhai wao.

Pia watu huchukua tahadhari kama kufanya mazoezi, kubadili mfumo wa vyakula n.k ili kupunguza uwezekano wa kupata matatizo kama shinikizo la damu, kisukari n.k.

c) Kuandika mirathi.
Kuwaza juu ya kufa humfanya mtu kuandika mirathi au kuweka utaratibu mzuri wa ugawanyaji wa mali anazomiliki.

Pia huwafanya wazazi kuwajengea watoto wao misingi ya utunzaji na ukuzaji wa mali za familia, hususani kwa familia au watu wasio na uwazi kwa watoto au ndugu zao juu ya idadi na ubora wa mali wanazomiliki.

Kila nafsi itaonja mauti! Hivyo kila mtu anapaswa kutafakazi, je matendo yake yanashabihiana na mapenzi ya Mwenyezi Mungu?

Wakati wa kurudi kwa Muumba hakuna nafasi ya kubeba hata sehemu kidogo ya mali mtu alizozalisha au kwa mabavu au kwa njia njema. Kila mtu anapaswa kuwa mfumo wake wa maisha utakaodumu hata baada ya kifo chake. Kwani mtu hufa lakini matendo na mwenendo wake mwema humweka hai na kubaki kama ua katika jamii alimoishi.

Monday, May 21, 2012

KANUNI ZA KUKUZA MALI

Kuna kanuni kuu nne zinazomwezesha mtu kupata mali au pesa, kuweza kuwa na uhakika wa kipato kwa muda mrefu katika kila uwekezaji.
Kanuni hizo ni kanuni ya mapato, kanuni ya matumizi, kanuni ya kuweka akiba na kanuni ya uwekezaji uchambuzi wa kanuni hizo ni kama ifuatavyo:

1. Kanuni ya mapato.

Kila aina ya kipato (iwe pesa au mali) hutengenezwa kwanza katika fikra.
Ili kupata kila kitu kunahitajika mbadilishano wa mawazo baina ya mtu na mtu au baina ya mtu na mazingira.

Kuna njia nyingi za kupata kipato au rasilimali yoyote ile. Miongoni mwa njia hizo ni; kuomba kutoka katika taasisi za fedha kama benki, kuomba msaada kutoka kwa ndugu au jamaa, kudunduliliza kidogo kidogo, kuomba msaada kutoka katika taasisi zinazokuza uwezo wa makundi ya watu kama vijana, wajane n.k

Ukubwa au ubora wa kipato hutegemea ubora wa mawazo na kiasi cha ushawishi alicho nacho mtu. Ikumbukwa ya kwamba si rahisi kwa mtu kuchangia kwa hali au mali juu ya kumwezesha mtu mwingine, hususani asiye na uhusiano naye.

2. Kanuni ya matumizi.

Bila ya matumizi hakuna mapato. Hakuna cha bure kamwe! Kuna aina kuu mbili za matumizi, nazo ni matumizi ya kawaida na matumizi ya uzalishaji (uwekezaji).

Matumizi ya kawaida ni matumizi yote yasiyolenga kuongeza kipato (mtaji) hata kidogo. Matumizi hayo ni kama kununua nguo, chakula, vinywaji na vitu vyote vinavyohisana na kukidhi mahitaji ya mara kwa mara ya binadamu.

Aina ya pili ya matumizi ni matumizi ya uwekezaji (kukuza kipato). Haya ni matumizi yote yanayohusiana na kuongeza (kuzalisha) mali; kuzalisha mali iwe kwa muda mfupi au mrefu. Matumizi haya ni kama; kununua hisa, kununua bidhaa ili kuuza, gharama za kulima au kufuga ili kuuza n.k

3. Kanuni ya kuweka akiba.

"Matumizi bila akiba, pesa zitatukimbia", pia haba na haba hujaza kibaba. Kwa baadhi ya watu walio wengi suala la kuweka akiba ni ngumu sana. Ugumu huo hujidhihirisha pale mtu 'anapokula mpaka mbegu'.

Watu wengi na mbao ni masikini hawatoweza kupata mafanikio endelevu kwa kuwa hutumia pesa au rasilimali nyinginezo bila ya kufikiri kesho itakuwaje. Humwachia Mungu kila jambo, hata yale mambo ambayo Mungu aliyowapa mamlaka na uwezo wa kuyatatua.

Ili kupata na kutunza mtaji mtu anapaswa kutunza kati ya 25% na 30% ya kipato chake chote, hususani pesa au bidhaa zinazoweza kubadilishwa na pesa kwa urahisi.

Utaratibu wa kutunza (kuweka akiba) humfanya mtu kuwa na nidhamu juu ya kila rasilimali anayoipata. Kuwa na akiba pia humfanya mtu kuwa na utulivu na kufikiri zaidi juu ya kuimarisha kile alichokipata. Kuweka akiba huwa ngumu kwa baadhi ya watu kwa kuwa hawana MALENGO.

4. Kanuni ya uwekezaji.

Tumia pesa zikuzoee, na pesa huzaa pesa ni baadhi ya sentensi chache zinazoweza kueleza dhana mzima ya uwekezaji kama mhimili wa nne wa utajiri.

Uwekezaji huja baada ya kuweka malengo na kukusanya pesa au rasilimali kwa ajili ya lengo husika. Matumizi kwa ajili ya uwekezaji yanapaswa kuelekezwa kwenye lengo husika na kwa makini ili kuhakikisha hakuna ufujaji wa mali.

Ili kuwa makini katika matumizi ya uwekezaji, mtu anapaswa kujiuliza, je natumiaje rasilimali zangu sasa hivi ikilinganishwa na lengo husika?

Watu hupata faida kidogo au isiyoridhisha kwa kuwa; wanaogopa kuwekeza katika miradi inayochukua muda mrefu ili kupata faida au hawana mitaji, au huwekeza kwa kufuata mkumbo n.k. Hivyo watu wengi wakigombania fursa chache za kuwekeza na hivyo kusababisha ukosefu wa soko kwa bidhaa walizozalisha.

Kunahitajika kufanya kazi kufa au kupona ili kuhakikisha uwekezaji unazaa matunda yaliyokusudiwa.
HAKUNA ALIYEZALIWA AKIWA TAJIRI, KILA MTU HUSUSANI MIMI NINANAWEZA KUWA TAJIRI.

Monday, May 14, 2012

KUMUDU UVUMILIVU

Mafanikio yoyote yale huja baada ya uvumilivu, kwani hakuna cha bure, pia bure ni ghali. Si rahisi kumudu changamoto na hata kufikia mafanikio, bila ya kuwa na zana sahihi.
Miongoni mwa zana zitumikazo ni zifuatazo:

a) Kuwa na hamu.

Kumudu makali ya changamoto huweza kufanikiwa ikiwa mtu husika anayo hamu kutoka moyoni, kuwa na hamu ya mafanikio husika; anayo dhamira ya dhati itokayo katikati ya moyo wake, wala si itikadi za watu wakaribu. Hamu ya mafanikio hujijenga katika akili, kisha kumpa mtu husika sababu za kusonga mbele; kusonga mbele ili kukabili kile kinacho waangusha wengi.

Kwa mfano; jinsi atakavyosherekea kuhitimu masomo, jinsi atavyoweza kuonyesha kwa matendo ya kuwa hakuna lisilowezekana, tafrija ya kuwa na makazi ya kudumu n.k.

b) Kuchambua mikakati.

Ili kukabiliana na changamoto, mtu husika anapaswa kuchambua kwa makini mikakati (njia) anayotarajia kupita au kutumia.

Uchambuzi wa kina juu kila hatua, na ambao utahusisha vikwazo vya hatua husika humsaidia mtu kuona kwa ufasaha ni nini cha kufanya wakati gani, kwa nini na jinsi ya kukabili vikwazo vitokanavyo. Kwa mfano; ili kuanzisha kilimo mtu anapaswa kujua; sababu ya yeye kulima, mahitaji ya kilimo kwa ujumla, mahitaji ya zao husika, soko la zao husika n.k

c) Kuchukua hatua.

Watu wengi sana huwa na mikakati mizuri sana, bali hushindwa kuitekeleza kwa kuwa hawachukui hatua kwa wakati sahihi. Watu huogopa kuchukua hatua ili kukabili changamoto ingali bado ndogo, hatimaye kuwaangusha nyakati za baadaye.

Waswahili wanasema 'nyani akinyeshewa na mvua husema, nitajenga nyumba kesho' na kesho haitokei. Mtu asijipangie majukumu makubwa ndani ya muda mfupi. Kumbuka, mdogo mdogo ndio mwendo.

d) Kuhusiana na watu sahihi.

Kuwa na marafiki ambao hutia moyo; ambao wamefanikiwa; ambao wanayo ndoto ya dhati ya kufanikiwa husaidia kupata msaada wa hali au mali pindi changamoto zinapajitokeza.
Imeandikwa, "chagua mazingira sahihi kwa kuwa yatakuumba, chagua marafiki sahihi kwa kuwa utafanana nao".

e) Kuamini hakuna kushindwa.

Changamoto zinapaozidi haziashirii kushindwa, bali zinaashiria au mtu hakuchukua juhudi sahihi au hakuchukua njia sahihi, au ni hali ya kawaida ambayo lazima mwana-harakati yeyote aipitie.

Mtu asiangalie ni mara ngapi ameanguka, bali aangalie ni mara ngapi amesimama na kusonga mbele. Pia ifahamike kwamba maisha si lelemama.

f) Kuamini hakuna cha bure.

Katika ulimwengu huu wa utandawazi; ulimwengu wa ubepari; ulimwengu ambao kila kinachofanywa popote pale kinatarajiwa kuleta mapato; kila maamuzi yanahusisha madhara ya kiuchumi au kwa mtu au kwa taasisi au kwa Taifa husika. Hakuna fursa ya bure kamwe!

Kila mtu, taasisi au taifa hupigana ili kupata mafanikio, hivyo mgongano wa kimaslahi ni lazima utokee. Hakuna aliye tayari kutumia gharama zake ili kumshibisha mtu mwingine bure.
Mfano, kutokana na uhaba wa maeneo ya kufanyia biashara, mtu yupo tayari kutoa msaada ili iwe rahisi kushawishi na kununua eneo la biashara kwa bei nafuu sana.
NYANI MZEE AMEKWEPA MISHALE MINGI, VIVYO HIVYO, MTU MWENYE MAFANIKIO AMESHINDA CHANGAMOTO NYINGI.

Monday, May 7, 2012

UVUMILIVU

Waswahili wanasema "MVUMILIVU HULA MBIVU". Ikiwa kama mtu atavumilia kutenda yaliyo sahihi, mahali sahihi, kwa watu sahihi na kwa muda sahihi atapata matokeo sahihi.

Uvumilivu ni hali ya kutia juhudi kwa kile mtu anachoamini kitampa mafanikio chanya. Imani humpa mtu uvumilivu na kisha uwezo katika harakati za kutimiza malengo.

Ikiwa kama mtu hakupata matokeo chanya au matokeo hayakumridhisha, anapaswa kuangalia upya mbinu alizotumia na kisha kujaribu tena; kurudia kwa mbinu nyingine.
Kumbuka: baada ya taabu - faraja; na uchungu ukizidi ndipo kujifungua kunakaribia.

Imebainika kwamba, ikiwa mtu atakuwa katika mwenendo usiofaa kwa muda mrefu, mtu huyo hubadili mwenendo na kuwa mtu mwema, ikiwa tu kama alitia juhudi katika kubadili mwenendo.

Uvumilivu hutiwa chachu kwa maneno matatu ambayo ni; NINAWEZA, NITAWEZA na LAZIMA.

Uvumilivu huonyesha dhamira ya kushinda. Dhamira ya kushinda hutegemea mtizamo wa mtu ambao ni; ninaweza, nitaweza na ni lazima kufanya kitu fulani ili kuboresha maisha.

Ikiwa kama mtu atakumbana na changamoto (wakati mgumu), kana kwamba ikaonekana hawezi kupiga hata hatua moja kuelekea mbele, asikate tamaa, kwani baada ya mawimbi makali hali ya bahari huwa shwari, na pia mawimbi hayadumu milele.

Watu wanaovumilia huku wakitia juhudi hupata mafanikio pale ambapo wengi hushindiwa. Mtafutaji hachoki, anayechoka hatofanikiwa kamwe!.

Mtu anapasa kutumia mawe (changamoto) yaliyopo njiani ili kuimarisha msingi; ili kutengeneza nafasi za kufanikiwa. Mawe wanayoyakataa waashi ndio huwa mawe makuu ya pembeni.

Bila ya kupambana hakuna ukuaji; kama hakuna ukuaji hakuna ushindi. Tunu huimarishwa na uvumilivu unaoakisi matunda ya jitida husika.

Changamoto kubwa ya kukosa uvumilivu ni; kuogopa lawama, kuogopa kushindwa na kutochukua hatua sahihi kwa wakati sahihi.