Tuesday, June 26, 2012

KUJIPANGA UPYA

Watu wasiokata tamaa; watu wanaoamini kuteleza sio kuanguka; watu wanaoamini kushindwa kufikia malengo kunatoa nafasi ya kujifikiria upya juu ya mwenendo wao, marafiki, mazingira n.k ndio wanaofanikiwa.

Katika mataifa makubwa kama Marekani, mataifa yenye fursa nyingi za kufanikiwa; mataifa ambayo yamelegeza sera zao ili kumruhusu mtu afanye anachotaka, takribani 95% ya watu huwa wamefilisika kimaisha wakifika mika 65.

Inashangaza! Kuna watu huishi maisha yao ya ujana katika dimbwi la umasikini, wanakuja kupata mafanikio wakifika uzeeni, kwa upande mwingine, kuna watu wanaofurahia maisha yao ya ujana, ili hali wakifika uzeeni huishi maisha duni kabisa.

Kushindwa kufikia malengo ndani ya muda fulani haimaanishi mtu husika ana bahati mbaya, si nadhifu, hajasoma n.k, bali ni kwa sababu kuna mahali fulani na kwa namna fulani nuru yake imezimika.

Kuzimika kwa nuru kunampa mtu udhaifu. Udhaifu huo unatumiwa na matapeli, waganga wa jadi, watu wanaojiita 'manabii' n.k kumtapeli mtu kwanza kifikra na baadaye kipato kidogo alicho nacho.

Nuru (dhamira) ya mafanikio imetunzwa kwa makini katika ubongo, imetunzwa sehemu salama, kwa bahati mbaya mtu husika kwa kushirikiana na wawezeshaji wengine huizima bila ya yeye kujua.

Ikiwa kama nuru imejeruhiwa, inapaswa kutibiwa haraka sana, kabla ya ugonjwa wa kutothubutu kusonga mbele kumkumba mtu na kumsababishia 'kifo'.

Kuna misemo ya Waswahili kama: mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe, (japo kwa sasa, mtaji wa masikini ni akili yake mwenyewe), ndondondo si chururu, kimfaacho mtu chake, heri shika kenda kuliko kumi nenda rudi, n.k

Misemo yote kama hiyo inalenga kutoa ujumbe kwamba, nguvu na jitihada za mtu binafsi ndizo zinazomfanya asonge mbele, hasa katika ulimwengu huu wa ushindani. Jitihada za mtu ndio nishati ya kweli inayoweza kumvusha mtu katika kipindi kigumu katika maisha. Haijalishi mtu ana elimu kiasi gani, kama asipodhamiria kufanya kazi, yote ni bure kabisa!

Hivyo basi, baada ya mtu kuyumbishwa anapaswa kujitafakari. Kujitafakari ni rahisi ikiwa mtu ataamua kutulia mahali tulivu, huku akitafakari kwa kujiuliza maswali "nilifanya nini? Kwa nini nilifanya hivyo? Kuna nafasi zipi sikizitumia? JE NITAFANYAJE ILI NISONGE MBELE?" n.k

Baada ya tafakari, mtu husika atakuwa amepata msingi imara wa kuonga mbele huku akikwepa makosa aliyoyafanya au watu waliyoyafanya wenzake na ambayo yalichangia kumwangusha.
Mtu asiangalie alipoangukia, bali aangalie alipojikwalia.

Mafanikio ni lazima, mafanikio hawezi kujipanga baada ya au kuona dalili za kukwama au kukwama.
MAFANIKIO NI LAZIMA! BINADAMU HAKUUMBA KUSHINDWA. NI LAZIMA MIMI KUFANIKIWA

Monday, June 18, 2012

MBINU ZA KUWINDA AJIRA (3)

5. KUPATA AJIRA YA KUDUMU.
Ni vigumu kupata au kuwa na uhakika wa kupata ajira ya kudumu, hususani katika taasisi binafsi. Hata hivyo, kuna watu wachache waliomudu kuwa na uhakika wa kufanya kazi katika kampuni au taasisi husika kwa muda mrefu; hata kuwa mtu muhimu sana katika eneo la kazi.

Ili kuwa na uhakika wa kufanya kazi kwa muda mrefu, mtu husika anapaswa:

(a) Kujiendeleza katika fani husika.

Kujiendeleza kitaaluma ni muhimu sana. Kujiendeleza kunaweza kwa kuhudhuria semina, kusoma vitabu, kuhudhuria makongamano.
Watanzania wengi hawapo tayari kulipia gharama zao binafsi ili kujiendeleza; hawapo tayari kununua na kusoma vitabu, kulipia na kuhudhuria makongamano au semina n.k. Hivyo hujikuta wakidumaza fani zao na utendaji kazi wao.

(b) Kujitolea

Kuna wakati mgumu katika maisha; wakati ambao mtu analazimika kutafuta kazi huku hajui aazie wapi.
Katika kipindi kama hicho mtu anapaswa kutafuta mahali atakapofanya kazi kwa muda kama mfanyakazi wa kuijtolea huku akipewa malipo kidogo kama nauli.
Kujitolea kufanya kazi kutamfanya mtu apate 'mitandao' ya ajira, kumwondolea msongo mawazo, kuongeza maarifa n.k. Kufanya hivyo kutamsaidia mtu kupata ajira ya kudumu kwa haraka.

(c) Kuunda mitandao

Watu wengi hupata kazi kutoka kwa watu wanaofahamiana nao. Kupata ajira kunahitaji kufahamika zaidi ya kuwa na uweledi katika fani husika.
Mtu anapaswa kuwa na kundi la marafiki katika nyanja tofauti tofauti za maisha, na marafiki wenye madaraka na ushawishi tofauti ambao watamuuunganisha na nafasi za ajira wakati wiowote anapotaka ajira.
Kutoka hatua moja kwenda nyingine kuna mlango. Mlango huo ni mtu na hufunguliwa na mtu.

(d) Kukwepa mawazo hasi.

Mawazo hujenga! "Awazalo mjinga, ndilo litakalomtokea". Ikiwa kama mtu atapokea na kuhifadhi mawazo hasi, ajue anajidumaza. Mawazo chanya huongeza rutuba katika ukuaji wa mtu.
Kwa bahati mbaya, binadamu tumezungukwa na mawazo hasi takribani kila tuishipo. Adui mbaya ni yule anayedhamiria kwa makusudi kumvunja mtu nguvu/ hamasa mtu mwingine.
Undugu huja bila uchaguzi, ila marafii huchagulika. Ikiwa mtu ameambiwa na mtu mmoja 'HUTOFANIKIWA' anahitaji watu kumi na sita kumwambia 'UTAFANIKIWA' ili kumrudishia hari.

(e) Kuheshimu kanuni na masharti.

Kwa watu wenye kazi wanapaswa kufanya kazi wa mujibu wa kanuni, miogozo na sheria za maeneo ya kazi. Kufanya kazi kwa misingi ya kanuni husaidia kupunguza migongano inayopelekea utendaji mbovu. Ni vigumu kufanya kzai kwa mujibu wa sheria, lakini inawezekana kupunguza uwezekano wa migawanyiko na makundi yanayofanya utendaji wa mtu kushuka na hatimaye kuondolewa kazini.

Monday, June 11, 2012

MBINU ZA KUWINDA AJIRA (2)

3. VYANZO VYA MAARIFA
Ili kupata kazi, mtu anapaswa kuwa tofauti na waombaji wengine wote. Ili kuwa tofauti, pamoja na mambo mengine, maarifa ni kitu muhimu. Kuna vyanzo vitatu vya maarifa:

3 (a) Elimu ya Darasani.
Hii ni elimu mtu aipatayo kutoka kwa Wakufunzi rasmi, katika mazingira ya shule; elimu itolewayo katika mfumo rasmi wa elimu. Kwa mfano, Sekondari, Vyuo vya Ufundi n.k. Elimu hii ni ya kufuta ujinga, kwani inao mchango kidogo sana katika kufanikiwa kwa mtu.

3 (b) Elimu ya mitaani.
Hii ni elimu itoknayo na mwingiliano wa mtu na jamii anayoishi. Kwa mfano; kuhudhuria makongamano, kuwasikiliza watu waliofanikiwa, kufanya majadiliano n.k. Elimu hii humpa mtu maarifa sahihi ya kukusanya na kutumia rasilimali zinazomzunguka kwa ufasaha zaidi. Elimu hii ndio iliyowawezesha watu wengi kupata mafanikio.

3 (c) Elimu ya vitabuni.
Elimu hii hutokana na kusoma vitabu vyenye mlengo chanya. Vitabu vinamwezesha mtu kupata mawazo na ushauri kutoka kwa watu maarufu na waliofanikiwa; ambapo isingelikuwa watu hao waliweka mawazo yao katika vitabu, ingekuwa vigumu sana hata kusalimiana nao.

Kupitia vitabu, mtu anapata kujua watu maarufu walifanikiwaje kufanya biashara, kuajiriwa, kuongoza n.k, hivyo na yeye achukue uamuzi gani kulingana na hali inayomsonga.
vyanzo vote ni bora; ila Elimu ya darasani na elimu ya mitaani ni vyanzo sahihi zaidi vya maarifa, kwani ni vya urahisi na uhakika, na vinaelezea hali halisi ya maisha.

4. KUFAHAMU MAHITAJI YA MWAJIRI.

Kabla ya kwenda kuomba kazi kwenye taasisi au shirika (ikiwa kama kazi haikutangazwa), mtu anaweza kufanya uchunguzi juu ya ndoto, mikakati na changamoto zinazoikumba taasisi husika. Kila mwajiri anatafuta:

4 (a) Mtu atakayeongeza thamani kwenye kampuni..
Waajiri hutafuta mfanyakazi atakayeongeza ubora wa huduma au bidhaa huku akipunguza changamoto zinazoikabili kampuni. Waajiri wanataka watu waoweza kuiokoa kampuni isiangukie kwenye msukosuko wa kiuchumi.

Linapokuja suala la kuomba kazi, Watanzania wanamatizo makuu matano nayo:
¤ uwezo mdogo wa kuongea na kuandika lugha ya Kiingereza, kwani Kiingereza ndio lugha inayowaunganisha watu wengi;
¤ kutojiamini, Watanzania wengi hawawezi kutetea kile wanachokiamini kuwa ni sahihi hasa baada ya kupewa changamoto;
¤ kutoa huduma mbaya kwa wateja, kukosa kujua na kumudu mbinu za kuwahudumia wateja hufanya biashara nyingi kufilisika;
¤ kushindwa kujiwasilisha; watu wengi hawajui wavae nini, watembeeje, waongee nini na wapi n.k. Hili ni tatizo kubwa hata kwa viongozi;
¤ uwezo mdogo wa kutumia vifaa pamoja na sayansi na teknolojia. Takribani 3% ya Watanzania ndio wanaoweza kutumia huduma za mtandao wa Intaneti kama; barua pepe, nukushi, Facebook, Twitter, YouTube n.k

4 (b) Watu halisia.
Waajiri hawataki ubora wa vyeti au watu wanaoweza kujieleza bila ya matendo, bali watu wachapa kazi.
Waajiri hawataki watu wenye mipango anuwai, bali mipango inayotekelezeka.
Itaendelea.....

Monday, June 4, 2012

MBINU ZA KUWINDA AJIRA (1)

Changamoto ya ukosefu wa ajira ni kubwa, si kwa Tanzania tu bali hata kwa mataifa mengine. Takribani kila Taifa kuna idadi kubwa ya watu wanaopunguzwa kazini kutokana na mabadiliko ya teknolojia au ili kumudu gharama za uendeshaji, pia kuna wahitimu wengi kutoka vyuoni.

Hatari kubwa ni kwa wahitimu kutoka vyuoni kwa kuwa waajiri mengi humtaka mwajiriwa mtarajiwa awe na uzoefu wa miaka kadhaa katika kazi anayotaka kuomba.
Hivyo wahitimu wanapaswa kufanya kazi ya ziada kwani santuli (CV) zao hazina thamani, zote zinafanana.

Kutokana na kufanana kwa CV, mhitimu anapaswa kuhakikisha anajiuza, si kutegemea CV impatie kazi.
Mtihitimu anaweza kuijuza kupitia: (i) muonekano wake (ii) vionjo alivyo navyo (iii) hamasa na (iv) imani aliyo nayo juu ya kufanikiwa. Pia mtu anapaswa kuishi kadiri ya fani yake kama: kuvaa mavazi ya heshima, kuongea kwa ufasaha, kutekeleza majukumu (kuacha uvivu) n.k. Vitu hivyo ni bora zaidi ya elimu ya darasani.

2.0. MIKAKATI

2.1. Kuwa na Lengo.
Soko la ajira ni ngumu, pia linabadilika badilika kila wakati. Watu wanaohitaji kazi ni wengi kuliko nafasi zinazotolewa na soko la ajira.

Hivyo mtu yeyote anayetafuta kazi lazima awe na LENGO mahususi. Watu wengi, hata wasomi wa vyuo vikuu hawana malengo. Wahitimu wengi huwa wamejiandaa kitaaluma tu! Hawajiandai ili kupata misingi ya kukabiliana na changamoto maishani. Hivyo kupata changamoto nyingi katika kujikwamua kimaisha.

Katika mchakato mzima wa kazi, kuna makundi matatu ya watu; washindi, washindi wasiojitambua na wasiojitambua.

i) Washindi.
Watu hawa hupata kazi wanayoitaka, kipato wanachotaka na kufanya kazi katika mazingira wanayotaka. Watu hawa ni majasiri (hujiamini), hutumia rasilimali zao kwa makini, wapo tayari kumfuata mtu mwenye madaraka (mf Mkurugenzi) yeyote na kumweleza malengo na changamoto zao. Watu hawa nui wachache sana.

ii) Washindi wasiojitambua.
Watu hawa wana dhamira ya dhati ya kupata na kufanya kazi, wanatumia jitihada zao, wanajiamini kidogo (ni waoga), hutegemea kupata kazi zinazotangazwa magazetini n.k. Huwa hawapati kazi kwa haraka kwa kuwa hawapo tayari kusimamia malengo yao, pia hawaelekezi nguvu zao kwa makini.

iii) Wasiojitambua.
Watu hawa hawajui ya kwamba hawajui, yawezekana wamesoma, lakini hawajitambui; elimu yao hijawakomboa. Huwa wanaishi bora mradi wakiamini kupata kazi ni bahati, na bahati yao haijaifika. Ni waoga kupindukia. Humtegemea Mungu kwa kila jambo hata kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wao.
KUPATA KAZI KUNATAKA KUFAHAMIKA ZAIDI YA KUWA NA UWEZO WA DARASANI. Itaendelea......