Upo uhusiano mkubwa sana baina ya namna mtu anavyofikiri na jinsi anavyoishi. Kushindwa kwa mtu hakutegemei nguvu yoyote aliyonayo isipokuwa ufahamu wa mtu husika.
Kuanguka kwa mtu hakutegemei idadi ya maadui aliyonao, isipokuwa aina ya mtazamo aliyonao. Kurudi nyuma kwa mtu (kiuchumi, kijamii n.k) hakutegemei historia aliyowahi kuwa nayo mtu husika, isipokuwa uendekezaji wa mawazo ya kushindwa.
Binadamu huongozwa/hujengwa na mawazo, mawazo ambayo yanapatikana katika mazingira husika.
Kwa kawaida mtu anapoona, anaposikia au jambo linapomtokea yeye mwenyewe, akili yake humpa tafsiri tofauti-tofauti juu ya jambo husika. Fikira hizo zinampa mtazamo fulani (- au +) katika maisha yake.
Mawazo hayo, baada ya muda huwa yanajitokeza katika maneno yake na hata katika matendo yake. Hivyo mtu huzugumza kufanikiwa au kutofanikiwa na baadaye kukifuatiwa na matendo.
Ni sawa na kusema kufanikiwa au kutofanikiwa ni suala la kimtazamo kuliko kuwa nacho au kutokuwa nacho.
Mifano ya kufanikiwa ni kama kuwa na; marafiki, upendo maadili mema n.k. Kwa upande mwingine kutofanikiwa ni kama kuwa na; huzuni, umasikini, maadui, n,k. Mawazo ndiyo asili ya hali inayoonekana kwa nje.
Kuna mifano michache:
¤Mark (26) aliamini anaweza kufanya biashara lakini hajui pakuanzia. Siku moja alihudhuria semina yenye lengo la kujenga uwezo wa vijana juu ya ujasiriamali.
Mazingira ya ukumbi, ufasaha wa lugha kutoka kwa wahadhiri, mifano halisi kutoka kwa wajasiriamali wazoefu n.k viliamsha hari ya Mark juu ya kuanzisha biashara.
Kuanzia hapo, Mark akatafuta ushauri zaidi, akatembelea maduka ya jumla, akatafuta mtaji kutoka kwa marafiki zake kisha kuanzisha biashara ya kuuza viatu vya mtumba.
Biashara ambayo imebadilisha maisha yake na ya familia yake.
¤Halima (27) alitoka kwa chakula cha jioni na rafiki zake watatu aliosoma nao high school.
Walifurahia mazungumzo, mazungumzo yaliyohusu mambo na matukio muhimu katika maisha ya sekondari, chuo na hata kazini.
Katika maongezi na michapo na michapo, Halima akaoanisha maisha yake na yale ya rafiki zake ndani ya miaka nane. Hatimaye akaona ya kwamba rafiki zake wanabahati zaidi yake. Ghafla akakumbwa na huzuni ukifuatiwa na msongo wa mawazo na kukosa usingizi kwa siku kadhaa.
Mtu akitaka kubadili hali yake (ya uchumi, mahusiano, kazi n.k) anapaswa kudhibiti yote anayoyaona au kusikia juu ya hali yake ya sasa, pamoja na hayo anahohubiriwa na mazingira yanayomzunguka.
Ni lazima kuchuja kile kinachoingia akilini kupitia milango ya fahamu. Chujio lako liruhusu mawazo chanya tu! Mawazo chanya (furaha, upendo, ushirikiano n.k) ni mbolea/mtaji katika jihada za binadamu za kujiletea maendeleo.
No comments:
Post a Comment