Maneno ya heshima, yaliyotamkwa kwa ufasaha huamsha hisia na kufanikisha tafakari. Ili kufanikisha mazungumzo; mazungumzo ya siku kwa siku, mzungumzaji anapaswa kupanga mawazo yake kabla ya kuanza kuzungumza.
Mbali na hilo; yafuatayo ni muhimu kuzingatiwa:
1) Kujipanga.
Ni vyema kupanga mawazo au hoja kabla ya kuanza kuzungumza. Mzungumzaji anapaswa kuweka mawazo ya msingi mwanzoni; na yawe katika mtiririko. Hii hufanikisha ufahamu kwa upande wa pili.
2) Kukaa kimya.
Kama mzungumzaji anahisi atakayosema yatamkwaza mtu; kama mzungumzaji anayo hasira ni bora akae kimya. Maneno ni kama mawe, pindi yanaporushwa hayazuiliki. Mzungumzaji asitishe anayokusudia kusema mpaka hali itakaporuhusu.
3) Kuwa muungwana.
Mtu (mzungumzaji) anapaswa kujenga tabia ya kutoa hoja kwa lugha ya upole. Kuonyesha uungwana na heshima dhidi ya upande wa pili; hufanikisha mazungumzo kwa urahisi pia, kuleta muafaka.
4) Kuepuka maneno "haijatokea" na " ni kawaida".
Kauli nyingi zinazoundwa na maneno hayo huwa hazina ukweli; pia ni vigumu kuzithibitisha. Maneno hayo hujenga jazba na hutatiza mawasiliano. Mfano, "ni kawaida yako kunihadaa", "haijatokea ukakubali mawazo yangu", n.k
5) Kusifia.
Ingawaje mzungumzaji anaweza kukinzana na hoja; lakini si 100%. Mzungimzaji anapaswa kutambua umuhimu wa mada; na ambao unafanya upande wa pili kutetea. Kisha mzungumzaji aanze kwa kuunga mkono au kusifia; na baadaye kutoa hoja zake za kukinzana.
Kwa mfano, "ni kweli kabisa! Lugha na historia ni vielelezo kwa taifa lolote lile, lakini vitu hivyo havichangii kukuza uchumi wa taifa. Kwani hata siasa, amani n.k havitegemei lugha au historia bali uchumi wa nchi husika".
6) Kukubali udhaifu.
Mzungumzaji asiongee kwa kujiamini hata akasahau madhaifu yake au alipokosea. Kuongea kwa kupitiliza hufanya upande wa pili kuhisi unashambuliwa; hivyo unaweza kupata jazba na hatimaye kuanzisha vurugu.
Mawasiliano bora yanapaswa kuleta au kukuza maelewano; wakati mwingine upande mmoja unaweza kutoridhika kutokana na kukubali haraka. Hali hiyo inaweza kuondolewa kwa:
1) Kutokimbilia kusema "Ndio"
Watu hukubali ilimradi yaishe. Kama mtu anahisi anao wasiwasi anapaswa kusema " nipe muda kidogo ili nifikiri juu ya hilo". Hivyo kupata muda wa kutafakari na kutoa jibu sahihi.
2) Kueleza hali halisi.
Kama mtu hana ujasiri wa kukataa; anapaswa kuleza hali aliyonayo, au changamoto zinazomkabili. Hii husaidia kupunguza upinzani pindi atakaposema "Hapana".
3) Kutoa mapendekezo.
Kama mtu yupo katika wakati mgumu; au akatae au akubali ombi la kushiriki jambo fulani, anapaswa kutoa mbadala au majina ya watu wanaoweza kufanya shughuli husika kwa ufasaha.
4) Kutolumbana.
Kama moyo na nafsi vinamwambia mtu asema "Hapana", basi asianzishe malumbano ikiwa kutotoa kwa kina sababu za kukataa; hususani kama alikwisha kueleza hali aliyonayo.
Kama upande wa pili unasisitiza au kuendekeza malumbano; mzungumzaji atumie busara. Mfano anaweza kusema "Tafadhali, nawasihi msinihinikize ili nilumbane, malumbano hubomoa misingi. Jibu langu ni HAPANA"
No comments:
Post a Comment