Monday, March 26, 2012

JE PESA NI KILA KITU?

Je ili kupata takribani kila kitu mtu anachotaka, ianampasa mtu kuwa na pesa? Jibu ni NDIO, na hiyo ndio sababu inayowafanya watu watafute pesa kila wakati; iwe usiku au mchana. Watu wamepewa majina mengi kama; mafisadi, wezi wa kalamu, matapeli, n.k kutokana na harakati zao za kusaka pesa. Huku pesa ikipewa majina kama; mkwanja, mapene, mawe, noti...

Kutafuta na kumiliki pesa nyingi ndi
o lengo la watu wengi. Hii haibadili ukweli kwamba watu hawapati pesa za kutosha kukidhi mahitaji yao; hata ya kila siku. Ikiwa pesa hazitoshi, je ni lazima kutafuta pesa?

Ukiwaza kwa kina utagundua kwamba, hakuna binadamu anayetaka pesa. Watu wanataka bidhaa au huduma, na wala si pesa. Hivyo, watu wanatafuta pesa ili kununua bidhaa au huduma kwa ajili ya kukidhi mahitaji; ili kukidhi mahitaji yasiyokwisha.

Kuelekeza mawazo na jitihada nyingi katika kutafuta pesa kumewafanya watu wasitafute njia mbadala za kukidhi mahitaji yao. Watu wanaamini pesa ndio kila kitu, hata wanasahau sababu za kutafuta pesa. Kuna baadhi ya watu wanatafuta pesa ili kuwa na 'usalama' na furaha, vitu ambavyo haviitaji pesa.

Kutaka pesa nyingi kumewafanya watu kuwa watumwa wa pesa, kumewafanya watu wachague au waache fani zao za awali na kukimbilia kwenye fani zenye uhakika wa pesa nyingi ili kununua furaha, bila ya kujali hatari (athari) zinazohusiana na fani husika.

Takribani watu wote maarufu na waliofanikiwa walielekeza nguvu zao kulinganana na vionjo (hobby) vyao, na wala si kufuta wingi wa fedha. Waliboresha vipaji vyao, na vipaji vyao viakawaletea pesa, heshima, furaha na usalama.

Ikiwa mtu anataka kupata mafanikio maishani, anapaswa kujiuliza; JE NINAHITAJI NINI HASA?
Ili kujibu swali hilo, mtu anapaswa kuandika vitu vyote anavyotaka kufanya au kuwa navyo bila ya kujali gharama. Wakati huo mtu husika akiwa mkweli dhidi ya nafsi yake; juu ya uhitaji wa bidhaa au huduma husika. Kisha mtu apitie tena orodha yake kwa kina huku akikadiria gharama.

Kwa kufanya hivyo kutamfanya mtu kutosema 'nahitaji maisha bora', bali atakuwa na malengo mahususi; kama nahitaji gari aina..., nahitaji nyumba iliyo na..., nahitaji elimu ya... n.k. Mtu atakuwa na malego ambayo, kama akielekeza nguvu ipasavyo, atakuwa na 'maisha bora'.

Kuwa malengo mahususi kunamfanya mtu kujua kiasi gani cha pesa anachohitaji, pia kujua mbinu mbadala anazohitaji ili kutimiza lengo husika.
Mbinu mbadala kwa kila jambo ni muhimu sana, kwani kuna baadhi ya mambo hayahitaji pesa, bali ufahamu, ushauri..... ambao unaletwa na mahusiano mazuri baina ya mtu na jamii yake.

Monday, March 19, 2012

KUUSHINDA WOGA ULIOPINDUKIA

Woga wa kupindukia (kupitiliza) ni hali ya mtu kuogopa na kujitenga na watu muda wote. Watu wenye woga wa kupindukia hukwepa kujihusisha na wageni n.k. Woga wa kupitiliza huwakosesha watu faida na nafasi za kujifunza kutoka kwa jamii yao.

Woga wa kupitiliza hujidhihirisha katika katika mazingira yafuatayo:
¤ Kukwepa mikutano.
Watu hawa hukwepa kadiri iwezekanavyo ili wasihudhurie mihadhara au sherehe za pamoja.
¤ Upweke.
Woga wa kupitiliza humfanya mtu atumie muda mwingi akiwa pekee (faragha), au kutoka jasho, kutetemeka n.k anapotakiwa kuzungumza hadharani.
¤ Kutowasiliana hadharani.
Woga wa kupindukia hupelekea mtu kupata kigugumizi, kutetemeka n.k wakati wa kuongea. Hali huwa mbaya pale mtu anapotakiwa kufafanua kwa umma jambo linalohusu utendaji kazi wa ofisi au kada yake.

Suluhu Dhidi ya Woga Uliopitiliza

Woga wa kupindukia unahusishwa sana na sababu za kibaiolojia (kurithi). Suluhu ipo ikiwa mtu ataamua kwa dhati. Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitumikazo:

1. Kutambua kiini.
Mwathirika anapaswa kutambua mazingira au hali inayopelekea woga. Kama chanzo cha woga ni kudai haki, mtu husika anaweza kutafakari madhara aliyopata yeye au jamii yake kwa yeye kukaa kimya.

2. Kuweka mkakati.
Baada ya kugundua kiini cha tatizo, mtu anapaswa kuweka mpango mkakati ili kuondoa tatizo. Mpango mkakati unaweza kuhusisha kubadili tabia, marafiki, maeneo ya kupumzika (vijiwe) n.k.

Kwa mfano, kama mtu anaogopa kujihusisha na jinsia tofauti, anaposwa kujihusisha na marafiki, ndugu n.k wenye ujasiri wa kuhoji bila kujali jinsia pinzani.

3. Kujipa changamoto.
Japokuwa ni ngumu kwa siku za awali, ili kupata mafanikio ya haraka, mtu anapaswa kujipa changamoto (mazoezi) kwa kufanya kazi inayomfanya mtu ahusiane mara kwa mara na watu wa aina mbalimbali.

Mtu anaweza kujitolea kwenye taasisi au shirika fulani kwa muda fulani.
Pia mtu anaweza kuongea bila ya kufikiri bila ya kufikiri mtu mwinine atajibu vipi? Mazoea humfanya mtu aondoe hofu.

JIPIME.
Jibu N kama jibu ni NDIO na H kama jibu ni HAPANA kwa maswali yafuatayo:

1. Je upo tayari kuzungumzia jambo linalokufurahisha katika kundi la marafiki zako?
2. Je unaweza kuanzisha mawaliano na mtu usiyemjua?
3. Je huwa unatetemeka, kutoka jasho au kupata mapigo ya moyo unapotakiwa kuongea hadharani?
4. Je mtu akitaja jina lako kwa sauti huwa unashtuka?
5. Je huwa huna raha ukiwa karibu na mtu wa jinsia tofauti, ambaye hujamzoea?
6. Je unaweza kurudisha mali yenye kasoro baada ya kununua?
7. Je huwa unashindwa kutetea hoja yako pale inapopata upinzani?
8. . Je mtu akikupita kwenye mstari wa huduma, unaweza kumwambia alivyofanya si halali?
9. Je huwa unalaumu pale mtu anapokuita (anapokupigia simu) wakati usio sahihi, kama usiku wa manane?
10. Je unaweza kudai salio (chenchi) pale muuzaji anapokupunguzia?
11. Je unaweza kukopa fedha ili kukamilisha manunuzi?
12. Je unaweza kukataa bidhaa pale mhudumu anapokuletea bidhaa ambayo hujaagiza?
13. Je huwa unajitenga katika mikusanyiko ili kukwepa malumbano?
14. Je kama mtu anavuta sigara hadharani, na moshi wa sigara unakukwaza, unaweza kumwambia?
15. Kama mchuuzi (mmachinga) akikuletea bidhaa nyumbani, eneo la kazi n.k huwa unanunua hata kama bidhaa husika haina umuhimu?

Ufafanuzi:
¤ kama majibu ya N ni kati ya 1 mpaka 5, hamna tatizo la woga
¤ kama majibu ya N ni kati ya 5 mpaka 10, kiwango cha woga ni wastani, japo ni muhimu kuchukua tahadhari.
¤ kama majibu ya N ni zaidi ya 10, kiwango cha woga ni cha hali ya juu. Mikakati madhubuti na ushauri utekelezwe haraka iwezekanavyo ili kupunguza madhara.

Monday, March 12, 2012

KUSHINDA HISIA ZA KUTOKUKUBALIKA

Kukataliwa ni hisia kali zinazomkabili mtu na kumfanya aamini hakubaliki miongoni mwa wengine. Hali hii inaweza kumkabili mtu kwa sababu za kijamii (tofauti ya rangi), migogoro ya kifamilia (hususani ya mahusiano), tofauti za kimtazamo, tofautu za kimadaraja (aliye nacho na asiye nacho) n.k

Hisia za kukataliwa, bila ya kujali kisababishi, hupelekea madhara makubwa kwa mtu husika kama:
¤ hupelekea ugomvi wa nafsi;
¤ kuvunja mahusiano baina ya mtu na jamii yake;
¤ kupunguza ufanisi kwa kushindwa kuelekeza nguvu kwenye kazi;
¤ kushuka kwa kinga ya mwili hivyo kupelekea maradhi ya mara kwa mara.

Jinsi ya Kuepuka Kukataliwa.
1. Kuzuia mawazo ya kukataliwa

Mtu anapaswa kukuza hisia (mawazo) chanya dhidi ya wengine, hususani wapinzani wake. Mikakati itumikayo ni kama; kutathmini sababu za kutokukubalika, kutathmini uhalisia wa mambo yanayoleta tofauti, kuamini kuna suluhu ya kudumu, n.k.

Mikakati hatarishi ni kama; kukataa kuwasiliana na mpinzani, kuamini 'mimi' ni sahihi, kuamini kwamba mtu husika hana bahati ya kukubaliwa, kukumbuka mabaya mtu aliyofanyiwa n.k

2. Kuepuka mazingira ya upweke.

Ikiwa baada ya ugomvi, mtu ataamua kukaa mazingira tulivu kwa muda mrefu, hupelekea chuki na kutaka kulipiza kisasi. Ili kuepuka upweke, mtu anapaswa kujihusisha na makundi ya watu (marafiki) ambao watatoa ushauri juu ya upatanisho.

3. Kujipa majukumu.

Mtu anapaswa kupanga majukumu ya siku kana kwamba siku nzima (na siku zote) inakuwa na majukumu. Majukumu yahusishe mawasiliano ya mara kwa mara baina ya mtu husika na wengine. Kuwa na muda siokuwa na matumizi huruhusu mtu kukumbuka maovu mtu aliyofanyiwa hapo awali.

4. Kusamehe na kusahau.

Mtu anapaswa kujitahidi kadiri ya nguvu zake zote kusamehe na kusahau maovu aliyofanyiwa na jamaa zake. Ikiwa kama mtu anataka kuishi kwa amani na upendo, kisha kukuza uhusiano anapaswa kusamehe kwa moyo wake wote makosa yote aliyowahi kufanyiwa.

5. Kutaka suluhu.

Baadhi ya watu husubiri upande wa upinzani uchukue hatua za kuleta suluhu. Hali huwa mbaya sana ikiwa kama kila upande utakaa kimya na kusubiri upande wa pili utake kurekebisha tofauti. Mtu anapaswa kujiuliza, je kukaa kimya huleta suluhu? Na je nitakaa kimya mpaka lini huku nikisubiri suluhu ije?

6. Kumsaidia mpinzani.

Ikiwa kama mtu ataamua kuchukua hatua na kubebe 'mzigo' unaomkabili mpinzani wake, atakuwa ameonyesha ubinadamu wa hali ya juu sana. Hivyo, mpinzani ataona hakuna haja ya kuendekeza vita. Kwani kana asingeekuwa mpinzani wake kutoa msaada wa hali au mali, basi angeweza kuangamia.

7. Kumwomba Mungu.

Ikiwa mtu anapata ugumu wa kusamehe na kusahau, kuanzisha mazungumzo ya upatanisho n.k anapaswa kumwomba Mungu kulingana na imani yake. Kumwomba Mungu husaidia kupata ujasiri utaovunja mizizi ya shetani. Kwani shetani hapendi amani miongoni mwa watu walio sura na mfano wa Mungu.

Monday, March 5, 2012

JINSI YA KUBANA MATUMIZI

Ubora wa matangazo, tabia ya mtu na kuwepo kwa bidhaa ndizo sababu zinazopelekea kuwepo kwa 'ulafi' nyakati hizi, hususani maeneo ya mijini.

Je kuwepo kwa bidhaa na huduma kwa wingi hupelekea furaha? Jibu ni HAPANA. Chunguzi zilizofanywa miongoni mwa vijana waishio miji mingi duniani, ikilinganishwa na wazee wao ambao hawakua na uwezo wa kumudu matumizi, zinaonyesha kwamba vijana wanayo furaha ndogo.

Je Jamii Itapata Faida Gani Ikiwa Itapunguza Matumizi?

1. Uhifadhi wa rasilimali. Rasilimali asilia zitatunzwa kwa kizazi kijacho ikiwa kutakuwa na matumizi endelevu ya huduma na bidhaa zitokanazo.
2. Mazingira safi. Uchafu utapunguzwa ikiwa kama kila mtu atatumia bidhaa na huduma kwa uangalifu.
3. Kukwepa mzigo wa madeni. Haitakuwa lazima kuchukua mkopo kila mara ili kugharamia matumizi ya kawaida. Hivyo, kupunguza utegemezi wa kifedha.
4. Kurahisisha maisha. Matumizi sahihi humfanya mtu ayaone maisha ni rahisi. Hivyo, kupunguza dhana ya maisha ni magumu katika fikra.

Mikakati ya Kupunguza Matumizi.

1. Kuweka vipaumbele.
Mtu anapaswa kuweka vipaumbele kulingana na matumizi ya fani, masomo, burudani n.k si kuyumbishwa na makundi. Vipaumbele viwekwe kwenye orodha kulingana na umuhimu wake.

2. Kuchambua matumizi.
Mtu anapaswa kufanya uchambuzi wa kina juu ya mahitaji ya wakati husika. Uchambuzi unaweza kufanywa kwa kujiuliza maswali kama; je ni lazima kununua bidhaa husika? Je hakuna mbadala wa bidhaa husika? Je kama nisingekuwa na fedha? n.k.

3. Kuwafikiria wengine.
Ni bora kununua bidhaa na huduma ambazo si tu zitamsaidia mnunuaji bali pia jamii ya wahitaji inayomzunguka kama; yatima, wajane, wazee, fukara n.k wanaomzunguka.

4. Kuepuka majina ya makampuni.
Yapasa kufanya uchambuzi kuhusu ubora na gharama, na si kununua bidhaa kwa kuwa imetengenezwa na kampuni fulani. Baadhi ya makampuni makubwa hutengeneza bidhaa hata zilizo chini ya kiwango, lakini hupata manunuzi makubwa kwa kuwa hufanikiwa kutangaza, kutoa punguzo la bei n.k

5. Kuahirisha matumizi.
Ni bora kusitisha ununuzi wa bidhaa au huduma isiyo na ulazima kwa siku, wiki au miezi kadhaa. Kusitisha manunuzi husaidia kufanya tafiti juu ya soko pia, husaidia kupunguza hamasa au ushabiki katika matumizi

6. Kupunguza matumizi ya kadi.
Mageuzi ya teknolojia yamewezesha watu kuwa karibu zaidi na fedha zinazohifadhiwa benki. Pia teknolojia imewezesha kufanya manunuzi kwa kutumia kadi za ATM.
Pia inashauriwa, kupunguza kiwango cha fedha za tahadhari mtu anazokuwa nazo popote aendapo.

7. Kuwalinda watoto.
Watoto ni sehemu kubwa sana ya jamii. Hivyo wanapaswa kusaidiwa kupunguza matumizi kwa:

(a) Kupunguza matumizi ya TV. Matangazo yanayoonekana kwenye TV huteka hisia za watoto. Hivyo, kuwafanya wanunue bidhaa hata bila ya wazazi/ walezi wao kujua.
(b) Kueleza ubaya wa matangazo. Watoto waelezwe ubaya wa kununua bidhaa kutokana na ushawishi wa matangazo.
MATUMIZI BILA AKIBA, FEDHA ZITATUKIMBIA..