Monday, March 19, 2012

KUUSHINDA WOGA ULIOPINDUKIA

Woga wa kupindukia (kupitiliza) ni hali ya mtu kuogopa na kujitenga na watu muda wote. Watu wenye woga wa kupindukia hukwepa kujihusisha na wageni n.k. Woga wa kupitiliza huwakosesha watu faida na nafasi za kujifunza kutoka kwa jamii yao.

Woga wa kupitiliza hujidhihirisha katika katika mazingira yafuatayo:
¤ Kukwepa mikutano.
Watu hawa hukwepa kadiri iwezekanavyo ili wasihudhurie mihadhara au sherehe za pamoja.
¤ Upweke.
Woga wa kupitiliza humfanya mtu atumie muda mwingi akiwa pekee (faragha), au kutoka jasho, kutetemeka n.k anapotakiwa kuzungumza hadharani.
¤ Kutowasiliana hadharani.
Woga wa kupindukia hupelekea mtu kupata kigugumizi, kutetemeka n.k wakati wa kuongea. Hali huwa mbaya pale mtu anapotakiwa kufafanua kwa umma jambo linalohusu utendaji kazi wa ofisi au kada yake.

Suluhu Dhidi ya Woga Uliopitiliza

Woga wa kupindukia unahusishwa sana na sababu za kibaiolojia (kurithi). Suluhu ipo ikiwa mtu ataamua kwa dhati. Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitumikazo:

1. Kutambua kiini.
Mwathirika anapaswa kutambua mazingira au hali inayopelekea woga. Kama chanzo cha woga ni kudai haki, mtu husika anaweza kutafakari madhara aliyopata yeye au jamii yake kwa yeye kukaa kimya.

2. Kuweka mkakati.
Baada ya kugundua kiini cha tatizo, mtu anapaswa kuweka mpango mkakati ili kuondoa tatizo. Mpango mkakati unaweza kuhusisha kubadili tabia, marafiki, maeneo ya kupumzika (vijiwe) n.k.

Kwa mfano, kama mtu anaogopa kujihusisha na jinsia tofauti, anaposwa kujihusisha na marafiki, ndugu n.k wenye ujasiri wa kuhoji bila kujali jinsia pinzani.

3. Kujipa changamoto.
Japokuwa ni ngumu kwa siku za awali, ili kupata mafanikio ya haraka, mtu anapaswa kujipa changamoto (mazoezi) kwa kufanya kazi inayomfanya mtu ahusiane mara kwa mara na watu wa aina mbalimbali.

Mtu anaweza kujitolea kwenye taasisi au shirika fulani kwa muda fulani.
Pia mtu anaweza kuongea bila ya kufikiri bila ya kufikiri mtu mwinine atajibu vipi? Mazoea humfanya mtu aondoe hofu.

JIPIME.
Jibu N kama jibu ni NDIO na H kama jibu ni HAPANA kwa maswali yafuatayo:

1. Je upo tayari kuzungumzia jambo linalokufurahisha katika kundi la marafiki zako?
2. Je unaweza kuanzisha mawaliano na mtu usiyemjua?
3. Je huwa unatetemeka, kutoka jasho au kupata mapigo ya moyo unapotakiwa kuongea hadharani?
4. Je mtu akitaja jina lako kwa sauti huwa unashtuka?
5. Je huwa huna raha ukiwa karibu na mtu wa jinsia tofauti, ambaye hujamzoea?
6. Je unaweza kurudisha mali yenye kasoro baada ya kununua?
7. Je huwa unashindwa kutetea hoja yako pale inapopata upinzani?
8. . Je mtu akikupita kwenye mstari wa huduma, unaweza kumwambia alivyofanya si halali?
9. Je huwa unalaumu pale mtu anapokuita (anapokupigia simu) wakati usio sahihi, kama usiku wa manane?
10. Je unaweza kudai salio (chenchi) pale muuzaji anapokupunguzia?
11. Je unaweza kukopa fedha ili kukamilisha manunuzi?
12. Je unaweza kukataa bidhaa pale mhudumu anapokuletea bidhaa ambayo hujaagiza?
13. Je huwa unajitenga katika mikusanyiko ili kukwepa malumbano?
14. Je kama mtu anavuta sigara hadharani, na moshi wa sigara unakukwaza, unaweza kumwambia?
15. Kama mchuuzi (mmachinga) akikuletea bidhaa nyumbani, eneo la kazi n.k huwa unanunua hata kama bidhaa husika haina umuhimu?

Ufafanuzi:
¤ kama majibu ya N ni kati ya 1 mpaka 5, hamna tatizo la woga
¤ kama majibu ya N ni kati ya 5 mpaka 10, kiwango cha woga ni wastani, japo ni muhimu kuchukua tahadhari.
¤ kama majibu ya N ni zaidi ya 10, kiwango cha woga ni cha hali ya juu. Mikakati madhubuti na ushauri utekelezwe haraka iwezekanavyo ili kupunguza madhara.

No comments:

Post a Comment