Monday, April 9, 2012

MISINGI YA THAMANI YA MTU

Kila anachofanya mtu maishani au kuongea kinaakisi jinsi mtu anavyohisi, kile anachotamani, kile anachoamini ni stahili yake na jinsi gani anajali thamani yake popote pale alipo.
Kupata bahati, kuungwa mkono, kupata changamoto n.k ni matokeo ya jumbe zinazotolewa na mtu husika.

Thamani ya mtu inajengwa na mtu mwenyewe pale awapo; iwe kazini, kitaaluma, n.k. Ili kukuza na kuimarisha thamani ya mtu, yafuatayo ni muhimu:

1. Kujiheshimu.
Mtu anapaswa kujiheshimu (kuwa na adabu). Kujiheshimu kunahusisha akili, mwili na nafsi. Kujiheshimu hujidhihirisha jinsi mtu anavyovaa, anavyotembea, anavyowasiliana, anavyopanga mambo ya siku kwa siku n.k

2. Kujisafisha.
Mtu anapaswa kuwa na nafsi inayobubujika kama chemchemu. Nafsi ya mtu inapaswa kububujika upendo; upendo utakaomweka mtu mbali na chuki, kisasi n.k. Upendo ndio unamfanya mtu aombe msamaha kwa dhati na kujutia mabaya aliyowafanyia wenzake.

3. Kujipenda.
Kiungo muhimu katika ustawi wa mtu ni kujipenda. Watu wanaojipenda huwa na fikra na nyoyo nyepesi; huwaza chanya na kuvuta bahati.

Kujipenda na kutambua thamani yake humfanya mtu kufikiri madhara ya matendo yake na kuchukukua hatua stahiki. Kujitambua ndiko kunakomfanya mtu kuwaza madhara ya vipodozi, kukuza viungo, ulevi wa kupindukia, kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa n.k.

4. Kuchuja mawazo.
Mtu hujengwa na mawazo; mtu huishi kadiri awazavyo. Kitu kinachowatofautisha watu ni jinsi wanavyochuja na kufanyia kazi mawazo wanayoyapata kupitia milango ya fahamu.

Mtu hutenda mabaya ikiwa aliruhusu na kuhifadhi mawzo mabaya, vivyo hivyo, mtu hutenda mema ikiwa aliruhusu, kuhifadhi na kuchambua mawazo kwa mtizamo chanya.

5. Kuwasoma watu.
Njia bora ya kupata mafanikio ni kusoma kutoka kwa watu; kusoma jinsi watu walivyofanikisha mafanikio na thamani yao; jinsi walivyozishinda changamoto.
Mtu anapaswa kuwatafuta na kuwa karibu na watu wanaojiamini; kuwasikiliza (kusoma maandiko yao) na kufuatilia jinsi wanavyotenda.

6. Kuchagua vishawishi.
Ni muhumu sana kwa mtu kuwa makini na kile kinachomfanya achukue aina fulani ya maamuzi. Mtu anapaswa kuruhusu vishawishi vinavyompelekea kufanya maamuzi yanayojenga na si kubomoa.

Vishawishi vinaweza kuwa kauli za watu, mienendo ya watu n.k. Vishawishi vinapaswa kusaidia kuondoa au kupunguza changamoto za kimaisha kwa mtu au jamii husika.

7. Kuepuka mizani.
Mtu anapaswa kuwa makini sana pale anapo-oanisha mafanikio yake na ya mtu mwingine. Ni bora kujipima kupitia malengo; japo jamii haiwezi kufanya hivyo. Mara nyingi watu wanaolinganisha mafanikio yao na yale ya wengine huishia kukwazika na kujishusha thamani yao.

Mafanikio ya mtu si mizani sahihi kwa kuwa mtu (mizani) husika anaweza kupata mafanikio haraka kupitia misaada, bahati, kupata changamoto nyepesi n.k

No comments:

Post a Comment