Monday, July 9, 2012

MBINU ZA KUPUNGUZA MAKALI YA MAJANGA

Hakuna mtu yeyote mwenye kinga dhidi ya janga lolote lile! Majanga huwakabili watu bila ya kubagua na mtu anapaswa kuyakabili bila ya kusita. Takribani mara zote majanga husababishwa na mahusiano ya kimapenzi, kazi, mabadiliko ya kiuchumi, ajali, mabadiliko ya afya n.k

Kiasi cha ukubwa wa janga au madhara yatokanayo hutofautiana sana; kikubwa ni kwamba kuna tofauti kubwa sana juu ya hisia na mbinu za kukabili janga husika. Kuna watu huwa na hisia chanya katika kuyakabili majanga (wanaamini watashinda), huku wengine husita, hukumbwa na hofu hatimaye hushindwa.

Ili kuweza kukabili janga na kuweza kupunguza ukubwa wa madhara, zifuatazo ni baadhi ya mbinu za kufahamu na kumudu:

a) Kuamini janga halikwepeki.

Kila mtu anapaswa kujua na kukiri ya kwamba kukumbana na changamoto tete katika maisha ni sehemu ya mapito ya kiumbe hai yeyote yule, hususani binadamu. Ikiwa kama mtu amekumbwa na hali ngumu anapaswa kujua kuna wengine wenye hali ngumu zaidi.

Kwa mfano, kama mtu amesalitiwa au kuibiwa mali zake anapaswa kujua ya kwamba kuna watu walio chini ya uangalizi wa daktari (ICU) ili kunusuru maisha yao au kuna familia zisizo na makazi wala chakula kutokana na mafuriko au maporomoko ya ardhi.

b) Kutolazimisha suluhu ya haraka.

Janga fulani linapotokea watu hufanya jitihada ili kuweka hali sawa ndani ya muda mfupi au haraka iwezekanavyo. Haishauriwi kusisitiza suluhu ya haraka, kwani takribani suluhu nyingi za haraka, zinazodhaniwa kuwa ni za kudumu hutuliza maumivu tu na hivyo kuongeza ukubwa wa tatizo nyakati za usoni. Suluhu nyingi za haraka hazina umakini.

Kwa mfano, kama mtu amesalitiwa kimapenzi, na akaamua kuanzisha mahusiano mapya ndani ya muda mfupi, mahusiano hayo mapya huleta madhara makubwa au kiafya au kiuchumi isivyotarajiwa.

c) Kutolaumu historia.

Muda mfupi baada ya adha fulani kutokea, watu wengi hujilaumu wenyewe au watu wengine kwa uzembe uliofanyika. Watu wengi husema "ningejua...ninge... Kauli kama hizo hazisaidii kitu chochote katika kuleta suluhu.

Hali kama hiyo huzuiowa kwa kubadili mawazo; kwa kuamini ukweli kwamba hakuna binadamu aliyekamilika, pia watu werevu hujifunza kutoakana na makosa wa wenzao, ikiwa makosa hatafanyika, kujifunza kutafanyikaje? Majanga hutumika kama kutoa somo kwa siku zijazo.

d) Kuangalia manufaa ya tukio.

Japokuwa majanga yote ni machungu,pia katika uchungu huo kuna chembechembe ndogo sana za utamu. Chembe hizo ndogo hugundulika baada ya kuchambua mkasa kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Baada ya uchambuzi wa kina, mhanga anaweza kujua uimara na udhaifu wake. Majanga huwa ni kipimo kuzuri dhidi ya mahusiano ya mhanga na jamaa zake wa karibu.

Kwa mfano, baada ya kufilisika kiuchumi, mhanga anaweza kujua nani ni rafiki, ndugu au jamaa wa kweli; kwani undugu ni kufaana na siyo kufanana. Majanga hutoa somo kwa watu wengine juu ya mienendo ya watu wao wa karibu.

e) Kuamini suluhu itapatikana.

Kama inavyosemwa, hakuna kinachodumu milele, kila kitu kitapita, hivyo basi, mhanga anapaswa kuamini ya kwamba hata machungu aliyonayo yatapita.
Uzoefu unaonyesha ya kwamba, majanga hutisha sana siku za mwanzo, baada ya muda fulani mhanga hupata ahueni na hatimaye, kutokana na juhudi, suluhu ya kudumu hupatikana. Kwa mfano, wakati wa ajali kabla ya huduma ya kwanza hali ni mbaya ikilinganishwa na wakati baada huduma ya daktari.

f) Kuepuka mjumuisho.

Janga huathiri sehemu fulani tu ya maisha ya mtu. Kupata msukosuko katika sehemu A ya maisha haimaanishi ya kwamba sehemu B nayo itapata msukosuko na kushindwa kufanya kazi.

Kwa mfano, mtu anapoenguliwa kazini huku familia yake na ndugu zake wakimtegemea, haimaanishi kwamba mrafiki na jamaa wengine watamsaliti; kwani watu hao hutoa ushirikiano (hutoa misaada au kutafuta kazi) ili kuhakikisha maisha yanasonga mbele. Hivyo haipaswi kuona ya kwamba janga fulani litafunga milango mingine.

No comments:

Post a Comment