ANGALIZO: kama mtu anataka kufanikiwa maishani, akwepe tabia saba ambazo watu dahifu huendekeza. Tabia hizo ni zifuatazo.
1. Kuwaza, kutamka na kutenda maovu.
Watu dhaifu huona kila kitu ni kibaya. Huwaza ubaya hatimaye huutamka na mwishowe huutenda. Watu hawa hulaumu kila kitu; hulaumu jua ni kali sana; mvua kwa kuwavurugia mipango yao; upepo kwa kuchafua nguo, nywele n.k.
Huhisi kila mtu anawapinga. Huona changamoto na si majibu. Hukuza ukubwa wa changamoto hata isitatulike. Huchukulia kushindwa ni kama janga. Hukata tamaa mapema na hawako tayari kurekebisha makosa yao. Ni vigumu mafanikio yao kuonekena, kwa kuwa hawako tayari kusonga mbele hasa wakati wa changamoto.
2. Kutenda kabla ya kuwaza.
Matendo ya watu dhaifu huongozwa na vionjo au hisia na wala si mawazo ya kina. Kama wakiona kitu kizuri kwa rangi au harufu wananunua bila ya kufikiria ubora au mbadala wake. Hutumia walichonacho mpaka kiishe kabisa! Hawawzi kuhusu kesho. Wapo tayari kutimiza furaha ya siku. Hawawazi kuhusu madhara ya matendo hatari kama; ngono zembe, ulevi wa kupindukia, matumizi ya sigara na madawa ya kulevya n.k. Wengi wao huwa waalifu kwa namna moja au nyingine.
3. Kuongea zaidi kuliko kusikiliza.
Hupenda kuanzisha mazungumzo, hivyo hujiingiza katika mazungumzo ili waonekane wao ni bora, hata kwa kusema uongo. Hawako makini na yale wanayoyazungumza. Kama wakishauriwa, hawapo tayari kusikiliza kwa kuwa hawapo tayari kukubali makosa au kushindwa. Huamii mawazo yao ni sahihi daima. Hawakubali mapendekezo kwa kuwa wanaamini hadhi yao itashuka.
4. Kukata tamaa mapema.
Watu wanaofanikiwa ni wale wanaochukua 'kuanguka' kama ngazi kuelekea kwenye mafanikio. Watu dhaifu hukata tamaa katika hatua za mwanzo, katika changamoto za kawaida. Mara nyingi watu dhaifu wapo tayari kuanzisha jambo au mradi ghafla, pindi hisia zinaposhuka hupata woga na kuacha mchakato mzima, hususani wanapokumbana na changamoto kidogo.
Watu hawa huacha kukamilisha wazo fulani, kisha kuanzisha lingine. Stori inakuwa kuanza na kuacha bila ya kukamilisha au kuona matokeo ya mawazo yao.
5. Kukatisha tamaa.
Watu dahaifu huponda mafanikio ya watu wengine. Badala ya kufanya jitihada ili wafanikiwe, hueneza uvumi na kujaribu kila mbinu chafu ili kuangusha wengine. Hawapo tayari kuomba ushauri kwa waliofanikiwa ili na wao wafanikiwe. Huona wanachofanya wenzao ni upuuzi au wanataka sifa au wanapoteza muda. Wanajua lakini hawazingatii ya kuwa ili kufanikiwa ni lazima kupata ushauri na mwongozo kwa waliofanikiwa kwa kupitia njia fulani.
6. Kupoteza muda wao.
Watu dhaifu hawajui ni nini cha kufanya baadaye. Hufikiria kula, kulewa, kuangalia TV au kukaa vijiweni wakipiga majungu wenzao. Hawatumii muda mwingi kuwaza na kutekeleza mawazo yao ili kuboresha maisha. Inafaa sana mtu aburudike (kubududika ni bora kwa afya ya akili na mwili) lakini huku mtu akichunga muda. Mtu anapaswa kuwa na muda mwingi wa kazi na kidogo wa burudani.
7. Kupuuzia mambo.
Kama kuna njia mbili za kufikia lengo (fupi na ndefu), watu dhaifu huchagua fupi yenye faida kidogo na kuacha ndefu yenye faida nyingi. Wanapenda maisha mazuri lakini hawapo tayari kutoka jasho. Hawapendi ukweli wa 'utavuna ulichopanda'. Watu wenye (au wanaotaka) mafanikio hawapuzi mambo; hufanikisha malengo yao kwa kujaribu; kwa kurekebisha makosa yao au ya wenzao ambao walishindwa kupita njia ndefu yenye mafanikio. Hawakati tamaa kwa kuwa wanaamini watu hufanikiwa pale wengine waliopshindiwa. Watapanda mlima uliowashinda watangulizi wao.
ANGALIZO: kama mtu anataka kufanikiwa maishani anapaswa kukwepa tabia saba ambazo watu dhaifu huziendekeza.
No comments:
Post a Comment