Dunia inafananishwa na uwanja. Uwanja ambao mchezo wa maisha unafanyika. Baadhi ya watu hufananisha mazingira ya kimchezo na harakati za binadamu. Maisha ni mchezo, na kama ilivyo kwa michezo yote (mfano mpira wa miguu) kuna makundi manne ya watu: wachezaji, mashabiki, wazururaji na washangaaji. Makundi hayo yanachambuliwa kama ifuatavyo.
1. Wachezaji.
Katika mchezo wowote, watu hawa ndio huvaa jezi na kuingia uwanjani, ndio sababu ya mchezo kuwepo. Hufanya mazoezi na kupammabana kwa kupitia changamoto zao au za watu waliowatangulia ili kupata tuzo. Hupokea tuzo au lawama kutokana na na matendo yao ya kishujaa.
Katika maisha, watu hawa huchukua jukumu la maisha yao, hujitoa mhanga katika kutetea kile wanachoamini ni sahihi. Hupata mafanikio, hata baada ya muda mrefu kupita. Hutumia muda wao mwingi kutafuta majibu juu ya changamoto zinazowakabili hata watakaposhinda 'ligi'.
2. Mashabiki
Hawa ni watazamaji wa mchezo. Hukaa kwenye majukwaa na kufurahia au kukwazika na jitihada za kufa au kupona zinazofanywa na wachezaji uwajani. Watu hawa ni sehemu ya mchezo au mafanikio ya wachezaji.
Katika maisha, watu hawa hukaa na kushuhudia jinsi wenzao wanapopambana ili kujiletea mafanikio. Hawapo tayari kutumia jitihada (hata za awali) ili kupata mafanikio walionayo wenzao. Miongoni mwao ( kwa kuvutiwa na mafanikio) hutaka kuingia katika kinyang'anyiro, lakini, pindi wanapokutana na changamoto kidogo hukimbia huku wakitoa vilio kama mbwa koko, wakiapa kamwe kutorudia tena. Hutoa sababu zisizo na msingi kama "ningepata.....ningefanya....". Wanaweza kuwa na wazo lakini, hawawezi kutetea wazo lao. Bali wanabaki kutoa mchango mdogo kwa wale wanaofanya jitihada kama vile kuwasaidia kazi ndogo ndogo, ushauri n.k
3. Wazururaji
Watu hawa pia huitwa washadiaji. Katika uwanja wa michezo, watu hawa hukaa nje ya uwanja; sehemu za maegesho ya magari huku wakisikia sauti za mashabiki wakiwapongeza au kuwazomea wachezaji (wakifurahia mchezo), wao sio sehemu ya mafanikio ya wachezaji au mchezo husika.
Katika maisha, watu hawa huitwa wavivu. Wanajua uwanja ulipo (sehemu ya kazi) lakini hawapo tayari kufanya jitihada kutafuta njia ya kufikia mafanikio. Watu hawa husimuliwa na 'mashabiki' juu ya habari za watu waliofanikiwa na kubaki kuwa wasikilizaji tu. Mara chache sana hutaka kuwa na mafanikio lakini, baada ya muda huona hamna haja ya kujitesa. Hivyo hubaki kuongea.
4. Washangaaji
Katika mchezo, watu hawa huwa mbali sana! Mbali kabisa na uwanja, hawajui hata njia au chochote kuhusu mchezo husika. Hawana hata wazo wala mipango ya kutafuta uwanja au habari za mchezo husika.
Katika maisha, watu hawa wamesongwa songwa na changaomto za kimaisha, wamekumbwa na upepo mkali na hawaoni mbele, hawajui hata waanzie wapi. Hawajui maisha gani ni sahihi kwao, japo wanajua maisha yao ni magumu. Hawajui wapewe nini ili wapate maisha bora au hata wakipewa hawawezi kusonga mbele. Wengi wao hawajui siku (tarehe) wala saa, hawajui nini watafanya siku inayofuata. Wanaishi kama ombaomba. Wanaishi kwa kutegemea miujiza ya Mungu.
JE WEWE UPO KWENYE KUNDI LIPI?
No comments:
Post a Comment