Monday, February 6, 2012

HUJUMA AFANYAZO MTU DHIDI YA NAFSI YAKE

Maria Robinson: "Hakuna mtu yeyote anayeweza kurudisha muda nyuma au kufuta historia ili aanze upya, ila mtu yeyote anaweza kuanza leo na kuandika ukurasa mpya wa mafanikio". Mtu yeyote anaweza kuanza mchakato wa kuboresha maisha yake wakati wowote ule, kama tu AKIDHAMIRIA kufanya hivyo.
Kwa bahati mbaya, watu huanza harakati za kupambana na maisha duni huku "wakikumbatia hujuma" dhidi ya nafsi zao. Hujuma hizo ni kama zifuztazo:

1. Kujihusisha na mtu au watu wasiosahihi.

Maisha ni mafupi sana, hususani ikiwa mtu anatumiwa kumnufaisha mwingine. Ikiwa mtu anahitaji msaada, atajenga mazingira ya kupata msaada. Watu wasiosahihi (wanyonyaji) hujenga mazingira ya kuwatumia wanyonge (maskini) ili kujinufaisha.

Watu hawa hujenga au kuimarisha uhusiani wakiamini tu! watapata msaada ili watimize malengo yao, huwatumia wanyonge kama ngazi, (mfano kuwapa msahara duni, kuwatumikisha zaidi ya uwezo n.k) bila kujali mustakabali wa afya n.k wa wanaowatumia. Mabosi hawa hawapo tayari kutoa msaada wa hali au mali ili kuwakwamua wafanyakazi wao.

Kwa hahati mabaya au kwa kujua au kwa kutojijua vibarua "huwaabudu mabosi hawa wanyonyaji na ambao huwatelekeza pindi wanapozeeka au kupata matatizo makubwa ya kiafya. Hatimaye vibarua huishia kuishi kama ombaomba wa kutupwa.

2. Kukimbia changamoto.

Ni vigumu sana mtu kukwepa changamoto zote zinazomkabili. Hivyo mtu anapaswa kusimama imara dhidi ya dhoruba za kimaisha. Watu hufanikiwa kwa kupitia changamoto moto moto. Kufanikiwa huwa ni matunda ya kukubali, kujifunza na kutatua changamoto zinazowakabili wakati wa kipindi chake chote cha maisha yao.

Watu hufanya hujuma dhidi ya nafsi au jamii kwa kukimbia changamoto bila ya kujua ya kwamba, changamoto zipo kwa ajili ya watu na watu ndio wao au bila ya kujiuliza, je watakimbia changamoto ngapi ili wafanikiwe?

3. Kujidanganya.

Mtu anaweza kumdanganya yeyote kaika dunia hii, lakini hawezi kujidanganya yeye mwenyewe. Maisha ya mtu huimarika pale anagundua na kuchangamkia fursa. Moja ya kitu kigumu ni kuukubali ukweli, ukweli ambao ni mlima ambao mtu anapaswa kuupanda ili afikie 'kilele' cha mafanikio.

Watu husaidiwa na mazingira au wale wanaowazunguka ili kujidanganya. Baadhi ya watu hujidanganya wana maisha mazuri ili hali hawajui au hawajapanga kesho au kesho kutwa yake itakuwaje, hawajafanya jitihada zozote kujikwamua.

4. Kujirudisha nyuma.

Baadhi ya watu (watu walio wengi) hawapo tayari kusimama mstari wa mbele huku wakipigania haki zao, hawapo tayari kusimama imara wakati wa kuwasilisha na kufafanua madai yao; huwaachia wawakilishi ambao si wahanga kupeleka hoja na kuwatetea (hata kwa mambo wanayoweza kuyafafanua wao wenyewe), wao hukaa na kusubiri taarifa za msuguano kutoka wa wanyonyaji kupitia wawakilishi.

Kwa bahati mbaya zaidi, baadhi ya watu huridhia haki zao zinyakuliwe wakiamini Mungu ndiye mtoaji. Kila mpiganaji anapaswa kuwa na roho ya kibinadamu, lakini asijishushie hadhi kwa kujiweka 'mkiani' au kijidharau.

5. Kufuata mkumbo.

Moja ya changamoto zinazomkabili mtu popote pale anapoishi ni kutaka kuishi maisha yake, maisha yasiyo na ushawishi kutoka kwa kundi fulani la watu katika jamii.
Kutokana na changamoto hiyo, watu hujikuta wakijidhulumu kwa kuiga maisha (kufuata mkumbo) ya watu waliofanikiwa wakiamini nao watafanikiwa au ili wapate kukubalika.

Watu wa ukweli ni wale wanaoweka vigezo vyao, kwa kuzingatia uwezo wao; vigezo wanavyoamini vitawatoa kimaisha. Vigezo au vipaumbele vitakavyowafanya wawe maarufu kwa mali, maelewano, mahusiano na jamii yao; si kwa mawazi, kuhudhuria klabu au vipodozi n.k

6. Kuogopa makosa.

Kufanya kitu bila ya kufanikiwa (kwa makosa) hata mara mia ni bora kuliko kutofanya chochote. Kila aliyefanikiwa ameanguka mara nyingi, na kila anguko limenfanya mtu aimarike zaidi. Baada ya kufanya jitihada za bila matunda yanayoridhisha, mtu hufanikiwa.

Kwa mfano, mwanasayansi aliyegundua balbu ya umeme alifanya majaribio mara 3000 na hatimaye akafanikiwa kutengeneza balbu inayowaka. Hata alipotakiwa na wanahabari kueleza palipokuwa panamshinda hivyo kufanya majaribio mengi aliwaambia "sijui tatizo lilikuwa ni nini".

7. Kununua furaha.

Watu hujidanganya ya kwamba wakimiliki kitu/ vitu fulani vya thamani au kujihusisha na mtu/ watu fulani watakuwa na furaha maishani. Hivyo, hutumia muda nwingi au rasilimali zao kugharamia furaha. Baadhi ya watu hudiriki kununua baadhi ya bidhaa za gharama, kugharamia mitoko na watu maarufu au kutafuta mahusiano ya kimapenzi na watu maarufu ili furaha yao itimie. Mwishowe hupata mgogoro wa nafsi na si furaha.

Ukweli ni kwamba, vitu vya kawaida ndivyo vinavyoleta furaha ya kweli na ya kudumu; vitu au mambo anayafanya mtu kwa hiari ya moyo na akili yake; vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wa mtu.

8. Kutoishughulisha akili.

Mtu asiyefikiri kwa ufasaha ndiye anayetekwa au kutumiwa na shetani kutekeleza uovu. Kila mtu anapaswa kuchambua kwa kina hali aliyonayo na kuchukua hatua sahihi.

Mtu anapaswa kuitumikisha akili ili kupata ya mambo aliyowahi kuambiwa hayawezekani. Kusonga mbele ni kukubali kukabili hatari. Pia mtu asiwaze (asiwaze bila mapumziko) kiasi cha kupata msongo mawazo.

9. Kuamini ukamilifu.

Wapiganaji hawaamini wamefanikiwa kwa 100% hata wapate fursa nzuri kiasi gani! Baadhi ya watu hubweteka kwa mafanikio kidogo, wakiamini wamefikia kilele, wengine huridhia kuacha kazi zao za ziada. Mabilionea hulazimishwa na mafanikio kufanya kazi zaidi; huku wakiamini mafanikio waliopata ndio mwanzo tu, na wanapaswa kutafuta fursa bora zaidi.
AMUA KUACHA HUJUMA LEO!

No comments:

Post a Comment