Monday, May 28, 2012

FAIDA ZA KUTAFAAKARI JUU YA KIFO

Kwa mtu kuamua kuwaza juu ya kifo chake ni jambo zuri, tafiti zimethibitisha hivyo tofauti na mitizamo ya watu.
Watu wengi huogopa sana pindi wanapoona jeneza au kupita makaburini au kusikia juu ya msiba. Hivyo kujikuta wakitafakari juu ya maisha yao.

Kuna baadhi ya mitizamo hasi ya kwamba mtu anayetafakari juu ya hatima yake, na kuongea hakawii muda mrefu bila ya kufariki. Baadhi ya watu huenda mbali zaidi na kusema ya kwamba mtu anayekaribia kufa huona baadhi ya dalili ndani ya siku arobaini kabla ya kifo chake, hivyo kumfanya aongelee kufa.

Kuna faida nyingi sana kwa mtu anayamua kutafakari kwa kina juu ya kifo chake na jinsi mambo yatakavyokuwa baada ya kifo chake. Miongoni mwa faida hizo ni:

a) Kumfanya mtu ajione sawa na wengine.

Watu wenye mali nyingi, hadhi n.k hujisahau. Pindi wanapohudhuria misiba hupata nafasi ya kujishusha, hivyo kujiona hawana tofauti kubwa na wale wanaowazika, kwani hao wanaowazika hawakupenda kufa, pia wao hawajui kwa nini wapo hai na watakufa lini. Hivyo kuimarisha uhusiano baina yao na jamii.

Pia kwenye ibada za mazishi viongozi wa dini hupata wakati wa kuhamasisha watu waishi kwa upendo ili apate mapumziko mema baada ya maisha ya duniani.

b) Kusaidia kuimarisha afya.

Watu hukata shauri na kwenda hosptali au vituo vya afya ili kupata kuchunguzwa afya zao (mfano kupima VVU, malaria n.k) baada ya kuambiwa madhara ya matendo yao au hatari zinazowasonga, kiasi cha kutishia uhai wao.

Pia watu huchukua tahadhari kama kufanya mazoezi, kubadili mfumo wa vyakula n.k ili kupunguza uwezekano wa kupata matatizo kama shinikizo la damu, kisukari n.k.

c) Kuandika mirathi.
Kuwaza juu ya kufa humfanya mtu kuandika mirathi au kuweka utaratibu mzuri wa ugawanyaji wa mali anazomiliki.

Pia huwafanya wazazi kuwajengea watoto wao misingi ya utunzaji na ukuzaji wa mali za familia, hususani kwa familia au watu wasio na uwazi kwa watoto au ndugu zao juu ya idadi na ubora wa mali wanazomiliki.

Kila nafsi itaonja mauti! Hivyo kila mtu anapaswa kutafakazi, je matendo yake yanashabihiana na mapenzi ya Mwenyezi Mungu?

Wakati wa kurudi kwa Muumba hakuna nafasi ya kubeba hata sehemu kidogo ya mali mtu alizozalisha au kwa mabavu au kwa njia njema. Kila mtu anapaswa kuwa mfumo wake wa maisha utakaodumu hata baada ya kifo chake. Kwani mtu hufa lakini matendo na mwenendo wake mwema humweka hai na kubaki kama ua katika jamii alimoishi.

1 comment:

  1. This is a constructive post that add value to peoples life.I will share to my blog (http://olemollel.blogspot.com/) also to reach many of us.Thank you for the nice post

    ReplyDelete