Monday, May 14, 2012

KUMUDU UVUMILIVU

Mafanikio yoyote yale huja baada ya uvumilivu, kwani hakuna cha bure, pia bure ni ghali. Si rahisi kumudu changamoto na hata kufikia mafanikio, bila ya kuwa na zana sahihi.
Miongoni mwa zana zitumikazo ni zifuatazo:

a) Kuwa na hamu.

Kumudu makali ya changamoto huweza kufanikiwa ikiwa mtu husika anayo hamu kutoka moyoni, kuwa na hamu ya mafanikio husika; anayo dhamira ya dhati itokayo katikati ya moyo wake, wala si itikadi za watu wakaribu. Hamu ya mafanikio hujijenga katika akili, kisha kumpa mtu husika sababu za kusonga mbele; kusonga mbele ili kukabili kile kinacho waangusha wengi.

Kwa mfano; jinsi atakavyosherekea kuhitimu masomo, jinsi atavyoweza kuonyesha kwa matendo ya kuwa hakuna lisilowezekana, tafrija ya kuwa na makazi ya kudumu n.k.

b) Kuchambua mikakati.

Ili kukabiliana na changamoto, mtu husika anapaswa kuchambua kwa makini mikakati (njia) anayotarajia kupita au kutumia.

Uchambuzi wa kina juu kila hatua, na ambao utahusisha vikwazo vya hatua husika humsaidia mtu kuona kwa ufasaha ni nini cha kufanya wakati gani, kwa nini na jinsi ya kukabili vikwazo vitokanavyo. Kwa mfano; ili kuanzisha kilimo mtu anapaswa kujua; sababu ya yeye kulima, mahitaji ya kilimo kwa ujumla, mahitaji ya zao husika, soko la zao husika n.k

c) Kuchukua hatua.

Watu wengi sana huwa na mikakati mizuri sana, bali hushindwa kuitekeleza kwa kuwa hawachukui hatua kwa wakati sahihi. Watu huogopa kuchukua hatua ili kukabili changamoto ingali bado ndogo, hatimaye kuwaangusha nyakati za baadaye.

Waswahili wanasema 'nyani akinyeshewa na mvua husema, nitajenga nyumba kesho' na kesho haitokei. Mtu asijipangie majukumu makubwa ndani ya muda mfupi. Kumbuka, mdogo mdogo ndio mwendo.

d) Kuhusiana na watu sahihi.

Kuwa na marafiki ambao hutia moyo; ambao wamefanikiwa; ambao wanayo ndoto ya dhati ya kufanikiwa husaidia kupata msaada wa hali au mali pindi changamoto zinapajitokeza.
Imeandikwa, "chagua mazingira sahihi kwa kuwa yatakuumba, chagua marafiki sahihi kwa kuwa utafanana nao".

e) Kuamini hakuna kushindwa.

Changamoto zinapaozidi haziashirii kushindwa, bali zinaashiria au mtu hakuchukua juhudi sahihi au hakuchukua njia sahihi, au ni hali ya kawaida ambayo lazima mwana-harakati yeyote aipitie.

Mtu asiangalie ni mara ngapi ameanguka, bali aangalie ni mara ngapi amesimama na kusonga mbele. Pia ifahamike kwamba maisha si lelemama.

f) Kuamini hakuna cha bure.

Katika ulimwengu huu wa utandawazi; ulimwengu wa ubepari; ulimwengu ambao kila kinachofanywa popote pale kinatarajiwa kuleta mapato; kila maamuzi yanahusisha madhara ya kiuchumi au kwa mtu au kwa taasisi au kwa Taifa husika. Hakuna fursa ya bure kamwe!

Kila mtu, taasisi au taifa hupigana ili kupata mafanikio, hivyo mgongano wa kimaslahi ni lazima utokee. Hakuna aliye tayari kutumia gharama zake ili kumshibisha mtu mwingine bure.
Mfano, kutokana na uhaba wa maeneo ya kufanyia biashara, mtu yupo tayari kutoa msaada ili iwe rahisi kushawishi na kununua eneo la biashara kwa bei nafuu sana.
NYANI MZEE AMEKWEPA MISHALE MINGI, VIVYO HIVYO, MTU MWENYE MAFANIKIO AMESHINDA CHANGAMOTO NYINGI.

No comments:

Post a Comment