Monday, May 21, 2012

KANUNI ZA KUKUZA MALI

Kuna kanuni kuu nne zinazomwezesha mtu kupata mali au pesa, kuweza kuwa na uhakika wa kipato kwa muda mrefu katika kila uwekezaji.
Kanuni hizo ni kanuni ya mapato, kanuni ya matumizi, kanuni ya kuweka akiba na kanuni ya uwekezaji uchambuzi wa kanuni hizo ni kama ifuatavyo:

1. Kanuni ya mapato.

Kila aina ya kipato (iwe pesa au mali) hutengenezwa kwanza katika fikra.
Ili kupata kila kitu kunahitajika mbadilishano wa mawazo baina ya mtu na mtu au baina ya mtu na mazingira.

Kuna njia nyingi za kupata kipato au rasilimali yoyote ile. Miongoni mwa njia hizo ni; kuomba kutoka katika taasisi za fedha kama benki, kuomba msaada kutoka kwa ndugu au jamaa, kudunduliliza kidogo kidogo, kuomba msaada kutoka katika taasisi zinazokuza uwezo wa makundi ya watu kama vijana, wajane n.k

Ukubwa au ubora wa kipato hutegemea ubora wa mawazo na kiasi cha ushawishi alicho nacho mtu. Ikumbukwa ya kwamba si rahisi kwa mtu kuchangia kwa hali au mali juu ya kumwezesha mtu mwingine, hususani asiye na uhusiano naye.

2. Kanuni ya matumizi.

Bila ya matumizi hakuna mapato. Hakuna cha bure kamwe! Kuna aina kuu mbili za matumizi, nazo ni matumizi ya kawaida na matumizi ya uzalishaji (uwekezaji).

Matumizi ya kawaida ni matumizi yote yasiyolenga kuongeza kipato (mtaji) hata kidogo. Matumizi hayo ni kama kununua nguo, chakula, vinywaji na vitu vyote vinavyohisana na kukidhi mahitaji ya mara kwa mara ya binadamu.

Aina ya pili ya matumizi ni matumizi ya uwekezaji (kukuza kipato). Haya ni matumizi yote yanayohusiana na kuongeza (kuzalisha) mali; kuzalisha mali iwe kwa muda mfupi au mrefu. Matumizi haya ni kama; kununua hisa, kununua bidhaa ili kuuza, gharama za kulima au kufuga ili kuuza n.k

3. Kanuni ya kuweka akiba.

"Matumizi bila akiba, pesa zitatukimbia", pia haba na haba hujaza kibaba. Kwa baadhi ya watu walio wengi suala la kuweka akiba ni ngumu sana. Ugumu huo hujidhihirisha pale mtu 'anapokula mpaka mbegu'.

Watu wengi na mbao ni masikini hawatoweza kupata mafanikio endelevu kwa kuwa hutumia pesa au rasilimali nyinginezo bila ya kufikiri kesho itakuwaje. Humwachia Mungu kila jambo, hata yale mambo ambayo Mungu aliyowapa mamlaka na uwezo wa kuyatatua.

Ili kupata na kutunza mtaji mtu anapaswa kutunza kati ya 25% na 30% ya kipato chake chote, hususani pesa au bidhaa zinazoweza kubadilishwa na pesa kwa urahisi.

Utaratibu wa kutunza (kuweka akiba) humfanya mtu kuwa na nidhamu juu ya kila rasilimali anayoipata. Kuwa na akiba pia humfanya mtu kuwa na utulivu na kufikiri zaidi juu ya kuimarisha kile alichokipata. Kuweka akiba huwa ngumu kwa baadhi ya watu kwa kuwa hawana MALENGO.

4. Kanuni ya uwekezaji.

Tumia pesa zikuzoee, na pesa huzaa pesa ni baadhi ya sentensi chache zinazoweza kueleza dhana mzima ya uwekezaji kama mhimili wa nne wa utajiri.

Uwekezaji huja baada ya kuweka malengo na kukusanya pesa au rasilimali kwa ajili ya lengo husika. Matumizi kwa ajili ya uwekezaji yanapaswa kuelekezwa kwenye lengo husika na kwa makini ili kuhakikisha hakuna ufujaji wa mali.

Ili kuwa makini katika matumizi ya uwekezaji, mtu anapaswa kujiuliza, je natumiaje rasilimali zangu sasa hivi ikilinganishwa na lengo husika?

Watu hupata faida kidogo au isiyoridhisha kwa kuwa; wanaogopa kuwekeza katika miradi inayochukua muda mrefu ili kupata faida au hawana mitaji, au huwekeza kwa kufuata mkumbo n.k. Hivyo watu wengi wakigombania fursa chache za kuwekeza na hivyo kusababisha ukosefu wa soko kwa bidhaa walizozalisha.

Kunahitajika kufanya kazi kufa au kupona ili kuhakikisha uwekezaji unazaa matunda yaliyokusudiwa.
HAKUNA ALIYEZALIWA AKIWA TAJIRI, KILA MTU HUSUSANI MIMI NINANAWEZA KUWA TAJIRI.

No comments:

Post a Comment