Tuesday, January 31, 2012

MAISHA NI MCHEZO

Dunia inafananishwa na uwanja. Uwanja ambao mchezo wa maisha unafanyika. Baadhi ya watu hufananisha mazingira ya kimchezo na harakati za binadamu. Maisha ni mchezo, na kama ilivyo kwa michezo yote (mfano mpira wa miguu) kuna makundi manne ya watu: wachezaji, mashabiki, wazururaji na washangaaji. Makundi hayo yanachambuliwa kama ifuatavyo.

1. Wachezaji.

Katika mchezo wowote, watu hawa ndio huvaa jezi na kuingia uwanjani, ndio sababu ya mchezo kuwepo. Hufanya mazoezi na kupammabana kwa kupitia changamoto zao au za watu waliowatangulia ili kupata tuzo. Hupokea tuzo au lawama kutokana na na matendo yao ya kishujaa.

Katika maisha, watu hawa huchukua jukumu la maisha yao, hujitoa mhanga katika kutetea kile wanachoamini ni sahihi. Hupata mafanikio, hata baada ya muda mrefu kupita. Hutumia muda wao mwingi kutafuta majibu juu ya changamoto zinazowakabili hata watakaposhinda 'ligi'.

2. Mashabiki

Hawa ni watazamaji wa mchezo. Hukaa kwenye majukwaa na kufurahia au kukwazika na jitihada za kufa au kupona zinazofanywa na wachezaji uwajani. Watu hawa ni sehemu ya mchezo au mafanikio ya wachezaji.

Katika maisha, watu hawa hukaa na kushuhudia jinsi wenzao wanapopambana ili kujiletea mafanikio. Hawapo tayari kutumia jitihada (hata za awali) ili kupata mafanikio walionayo wenzao. Miongoni mwao ( kwa kuvutiwa na mafanikio) hutaka kuingia katika kinyang'anyiro, lakini, pindi wanapokutana na changamoto kidogo hukimbia huku wakitoa vilio kama mbwa koko, wakiapa kamwe kutorudia tena. Hutoa sababu zisizo na msingi kama "ningepata.....ningefanya....". Wanaweza kuwa na wazo lakini, hawawezi kutetea wazo lao. Bali wanabaki kutoa mchango mdogo kwa wale wanaofanya jitihada kama vile kuwasaidia kazi ndogo ndogo, ushauri n.k

3. Wazururaji

Watu hawa pia huitwa washadiaji. Katika uwanja wa michezo, watu hawa hukaa nje ya uwanja; sehemu za maegesho ya magari huku wakisikia sauti za mashabiki wakiwapongeza au kuwazomea wachezaji (wakifurahia mchezo), wao sio sehemu ya mafanikio ya wachezaji au mchezo husika.

Katika maisha, watu hawa huitwa wavivu. Wanajua uwanja ulipo (sehemu ya kazi) lakini hawapo tayari kufanya jitihada kutafuta njia ya kufikia mafanikio. Watu hawa husimuliwa na 'mashabiki' juu ya habari za watu waliofanikiwa na kubaki kuwa wasikilizaji tu. Mara chache sana hutaka kuwa na mafanikio lakini, baada ya muda huona hamna haja ya kujitesa. Hivyo hubaki kuongea.

4. Washangaaji

Katika mchezo, watu hawa huwa mbali sana! Mbali kabisa na uwanja, hawajui hata njia au chochote kuhusu mchezo husika. Hawana hata wazo wala mipango ya kutafuta uwanja au habari za mchezo husika.

Katika maisha, watu hawa wamesongwa songwa na changaomto za kimaisha, wamekumbwa na upepo mkali na hawaoni mbele, hawajui hata waanzie wapi. Hawajui maisha gani ni sahihi kwao, japo wanajua maisha yao ni magumu. Hawajui wapewe nini ili wapate maisha bora au hata wakipewa hawawezi kusonga mbele. Wengi wao hawajui siku (tarehe) wala saa, hawajui nini watafanya siku inayofuata. Wanaishi kama ombaomba. Wanaishi kwa kutegemea miujiza ya Mungu.
JE WEWE UPO KWENYE KUNDI LIPI?

Monday, January 23, 2012

MBINU 13 ZA KUWA JASIRI NA KUFANIKIWA KIMAISHA

Mbinu 13 na rahisi za kupata ujasiri ujasiri kimafanikio.
1. Kutoshindana na waliofanikiwa.

Daima mtu ahakikishe anawafanya waliofanikiwa wajione wapo juu. Kama mtu anataka kuwashangaza basi asionyeshe ujuzi wake wote.
Kuwapa waliofanikiwa heshima yao kutamfanya mtu apate msaada na hatimaye afikie kiwango cha juu bila ya kupata tabu nyingi.

Mfano, mtu asishindane na mwajiri wake ili kuonekana anajua sana; asishindane na tajiri katika matumizi hususani mazingira ya kijamii kama baa, misiba n.k. Waliofanikiwa hutafsiri kitendo cha kushindana kama kuonyesha kiburi au maskini jeuri.

2. Kutoamini sana marafiki.

Mtu awe makini 'anapojamiiana' na marafiki au watu wa karibu. Watu wa karibu huwa wasaliti na huvujisha siri kwa wapinzani. Mtu aogope marafiki zaidi ya maadui, ikibidi awape nafasi wale anaohisi ni wapinzani. Ilkiwa mtu hana wapinzani, ajitahidi kuwatafuta. Mtu ajifunze jinsi ya kutumia wapinzani kimafanikio, si kuwaamini marafiki muda wote.

3. Kuficha malengo.

Mtu afiche matarajio yake au dhamira za matendo yake. Kuweka malengo hadharani huwafanya watu wenye nia mbaya kujipanga na kuvuruga malengo husika. Mtu akinge malengo yake na ikiwa yatagundulika iwe nyakati za mwisho; nyakati ambazo wapinzani hawawezi kuweka vikwazo.

4. Kutumia wasidizi.

Kufankiwa kwa mtu kunategemea mchango anaoupata kutoka kwa wale wanaomzunguka (mazingira na marafiki). Mtu atumie busara, ujuzi na maarifa ya wale anaofanya nao kazi ili kusonga mbele. Msaada haupunguzi tu nguvu, bali pia huongeza ufanisi na kuimarisha urafiki. Mtu hupata fadhila kutoka kwa wasaidizi wake, ndipo jamii husika. Hivyo, mtu awaachie watu wengine yale wanayoweza kufanya kwa ufanisi.

5. Kushinda kupitia matendo.

Ushindi mtu anaopata kupitia maneno haufai kitu! Mtu asishindane juu ya uwezo wake kwa maneno bali, aache matendo yaongee. Ushindi makini ni ule mtu anaoupata kupitia matendo yake, na si kwa wingi wa maneno. Uhalisia wa matendo huonyesha umakini wa mtu kwa jamii inayomzunguika. Mtu husifiwa kwa kadiri ya juhudi zake za hali na mali kutatua changamoto zinazomsonga, si kwa kupiga domo.

6. Kujenga utegemezi.

Ili mtu kujua umuhimu wake katika jamii anapswa kjua kwa kiasi gani mchango wake unahitajika. Mtu ajenge mazingira ya kutegemewa; kutegemewa kuleta furaha au ustawi katika mazingira yanayomzunguka.

Ili kfanya hivyo, mtu asitoe mbinu zote alizo nazo juu ya kitu fulani. Kutegemewa humwezesha mtu 'kuuza' kile alichonacho kwa mafanikio yake na ya jamii yake. Hivyo, mtu ajue wakatigani wa kuficha huduma yake, wakati gani wa ktoa kidogo na wakati gani wa kutaka watu wailipie.

7. kutenda kama mpelelezi.

Ni muhimu sana mtu kujua juu ya wapinzani wake. Mtu atumie marafiki (wapambe) ili kupata taarifa muhimu juu ya udhaifu na uwezo wa wapinzani wake. Kufanya hivyo kutamwezesha mtu kupanga mipango ya kiulinzi na ambayo haitazimika katika safari yake ya mafanikio. Kupata taarifa kunafanikishwa kwa kuuliza maswali rahisi, kuuliza kwa njia ya upole na kwa kutumia mifano. Kila wakati ni fasaha kwa upelelezi.

8. Kuwafahamu watu wa karibu.

katika mazingira yoyote yale kuna watu wa aina nyingi. Watu hutofautiana kiimani, kitabia, kimalengo, kiutendaji n.k. Watu wa karibu ndio wanaotoa au kufanikisha kotoa ushindani katika mazingira yasiyotegemewa. Watu wengi, tena wa karibu ni kama mbwa mwitu. Ili kufahamu watu wa karibu, mtu atafakari kwa kina misingi mikuu ya urafiki huku akibadilisha muonekano, kutoa changamoto kwa walengwa n.k. Pindi mtu anapofanya yote hayo atazame mwitikio ya walengwa.

9. Kuwa na dira.

Dira humwezesha mtu kufika kule anakotaka. Mtu anapaswa kuweka malengo juu ya kule anakotaka kufika baada ya muda fulani pia, changamoto azazohisi zitamkumba sambamba na suluhu sahihi. Kwa kuwa na malengo haitakuwa ngumu sana kukabiliana na vikwazo mtu awapo safarini. Watu wengi huweka malengo huku wakisahau au kupuuzia adha zinazoweza kuwakumba au zilizowakumba watu wengine waliokuwa na malengo kama yao.

10. Kujikuza.

Mtu asipokee na kukubali sifa 'chafu' anazopewa na jamii. Mtu anapaswa kujikuza kwa kuvaa utambulisho mpya; ambao unavuta umakini na hauiudhi jamii yake. Mtu anapaswa kutawala taswira yale, si taswira yake ktawaliwa na nguvu kutoka nje. Kujikiza kwa jitihada za mtu huleta taswira ya kudumu, na ambayo italeta uaminifu wa kweli na kukubalika katika jamii.

11. kuwa na shabaha.

Mtu anapaswa kuelekeza nguvu na jitihada kwa yale anayoamini yataleta matunda mazuri. Mtu awe makini kutunza au kutenga nguvu za ziada kwa ajili ya changamoto. Ili kutokata tamaa, mtu anapswa kuwa na wadu (watu wa karibu) wenye uwazo tofauti tafauti kama vile madaktari, wafanya biashara, waalimu, viongozi wa dini, wazee wenye busara n.k

12. Kujirudisha nyuma.

Kama mtu akiona changamoto zitamzidi siku a usoni, huku mbinu alizo nazo au mikakati yake itakuwa dhaifu ahairishe 'pambano'. Kurudi nyuma kutampa mtu nafasi ya kujipanga kwa kukusanya nguvu na 'kuusoma mchezo zaidi'. Mtu asikubali kuangushwa kabisa na changamoto ndipo ajiandae kuinuka. Ni vigumu sana mtu kuamka baada ya kushambuliwa na kuangamizwa na chahangamoto za kimaisha.

13. Kutojitenga.

Kujitenga na jamii au marafiki ni hatari sana! Kwani ulimwengu ni tambara bovu na uumejaa wapinzani kila kona. Inapasa mtu kujiundia ngome ya ulinzi lakini, si kwa kujitenga. Kujitenga hupunguza mawasiliano na watu na pia uwezekano wa kupata misaada ya hali na mali. Kwa mfano, kuna uwezekano mkubwa wa kukosa habari, ushauri, vitendea kazi n.k. Vitu ambavyo ni muhimu kufikia mafanikio.

Monday, January 16, 2012

TABIA SABA ZA WATU DHAIFU

ANGALIZO: kama mtu anataka kufanikiwa maishani, akwepe tabia saba ambazo watu dahifu huendekeza. Tabia hizo ni zifuatazo.

1. Kuwaza, kutamka na kutenda maovu.

Watu dhaifu huona kila kitu ni kibaya. Huwaza ubaya hatimaye huutamka na mwishowe huutenda. Watu hawa hulaumu kila kitu; hulaumu jua ni kali sana; mvua kwa kuwavurugia mipango yao; upepo kwa kuchafua nguo, nywele n.k.
Huhisi kila mtu anawapinga. Huona changamoto na si majibu. Hukuza ukubwa wa changamoto hata isitatulike. Huchukulia kushindwa ni kama janga. Hukata tamaa mapema na hawako tayari kurekebisha makosa yao. Ni vigumu mafanikio yao kuonekena, kwa kuwa hawako tayari kusonga mbele hasa wakati wa changamoto.

2. Kutenda kabla ya kuwaza.

Matendo ya watu dhaifu huongozwa na vionjo au hisia na wala si mawazo ya kina. Kama wakiona kitu kizuri kwa rangi au harufu wananunua bila ya kufikiria ubora au mbadala wake. Hutumia walichonacho mpaka kiishe kabisa! Hawawzi kuhusu kesho. Wapo tayari kutimiza furaha ya siku. Hawawazi kuhusu madhara ya matendo hatari kama; ngono zembe, ulevi wa kupindukia, matumizi ya sigara na madawa ya kulevya n.k. Wengi wao huwa waalifu kwa namna moja au nyingine.

3. Kuongea zaidi kuliko kusikiliza.

Hupenda kuanzisha mazungumzo, hivyo hujiingiza katika mazungumzo ili waonekane wao ni bora, hata kwa kusema uongo. Hawako makini na yale wanayoyazungumza. Kama wakishauriwa, hawapo tayari kusikiliza kwa kuwa hawapo tayari kukubali makosa au kushindwa. Huamii mawazo yao ni sahihi daima. Hawakubali mapendekezo kwa kuwa wanaamini hadhi yao itashuka.

4. Kukata tamaa mapema.

Watu wanaofanikiwa ni wale wanaochukua 'kuanguka' kama ngazi kuelekea kwenye mafanikio. Watu dhaifu hukata tamaa katika hatua za mwanzo, katika changamoto za kawaida. Mara nyingi watu dhaifu wapo tayari kuanzisha jambo au mradi ghafla, pindi hisia zinaposhuka hupata woga na kuacha mchakato mzima, hususani wanapokumbana na changamoto kidogo.
Watu hawa huacha kukamilisha wazo fulani, kisha kuanzisha lingine. Stori inakuwa kuanza na kuacha bila ya kukamilisha au kuona matokeo ya mawazo yao.

5. Kukatisha tamaa.

Watu dahaifu huponda mafanikio ya watu wengine. Badala ya kufanya jitihada ili wafanikiwe, hueneza uvumi na kujaribu kila mbinu chafu ili kuangusha wengine. Hawapo tayari kuomba ushauri kwa waliofanikiwa ili na wao wafanikiwe. Huona wanachofanya wenzao ni upuuzi au wanataka sifa au wanapoteza muda. Wanajua lakini hawazingatii ya kuwa ili kufanikiwa ni lazima kupata ushauri na mwongozo kwa waliofanikiwa kwa kupitia njia fulani.

6. Kupoteza muda wao.

Watu dhaifu hawajui ni nini cha kufanya baadaye. Hufikiria kula, kulewa, kuangalia TV au kukaa vijiweni wakipiga majungu wenzao. Hawatumii muda mwingi kuwaza na kutekeleza mawazo yao ili kuboresha maisha. Inafaa sana mtu aburudike (kubududika ni bora kwa afya ya akili na mwili) lakini huku mtu akichunga muda. Mtu anapaswa kuwa na muda mwingi wa kazi na kidogo wa burudani.

7. Kupuuzia mambo.

Kama kuna njia mbili za kufikia lengo (fupi na ndefu), watu dhaifu huchagua fupi yenye faida kidogo na kuacha ndefu yenye faida nyingi. Wanapenda maisha mazuri lakini hawapo tayari kutoka jasho. Hawapendi ukweli wa 'utavuna ulichopanda'. Watu wenye (au wanaotaka) mafanikio hawapuzi mambo; hufanikisha malengo yao kwa kujaribu; kwa kurekebisha makosa yao au ya wenzao ambao walishindwa kupita njia ndefu yenye mafanikio. Hawakati tamaa kwa kuwa wanaamini watu hufanikiwa pale wengine waliopshindiwa. Watapanda mlima uliowashinda watangulizi wao.

ANGALIZO: kama mtu anataka kufanikiwa maishani anapaswa kukwepa tabia saba ambazo watu dhaifu huziendekeza.

Monday, January 2, 2012

MBINU ZA KUFANIKIWA WAKATI WA USHAWISHI

Kushindwa kushawishi kumewafanya watu wayaone maisha ni adhabu. Kushindwa kushawishi kumewaangusha wengi katika ulimwengu huu; ulimwengu unaokwenda kwa kasi ya ajabu.

Si rahisi kumshawishi mtu akubali ombi na kutoa huduma au msaada kwa mtu mwingine. Kazi hii ngumu inaweza kufanikishwa kwa kutumia mbinu tano rahisi. Mbinu hizo ni zifuatazo:

Mbinu I. Kwenda sambamba na mshawishiwa.
Mshawishi anapaswa kutazama kwa makini jinsi mshawishiwa anavyowasiliana; iliwa ni pamoja na matumizi ya lugha ya ishara, ili naye afanye vivyo hivyo.

Ingawaje, mshawishi anapaswa kuwa makini ili asionekane anamkebehi mshawishiwa. Ikiwa mshawishiwa atagundua kuna "usanii" hatotia maanani yale anayoambiwa na hatimaye kutokubali kutimiza ombi la mshawishi.

Mbinu II. Kutimiza mahitaji ya wakati husika.
Watu hujipendelea. Watu hupenda mahitaji yao yatimizwe kwanza ndipo ya wengine yafuate. Mshawishi atambue vipaumbele vya msahwishiwa atakavyotekeleza ili maombi yake yatimizwe kwa urahisi.

Mshawishi atizame mahitaji, matakwa, vionjo n.k ili aweze kuvuta hisia za mshawishiwa. Mshawishi ajitahidi kutimiza kero au matakwa ya mshawishiwa kwa kadiri ya maadili, hali na uwezo wake kabla ya kutoa ombi lake.

Mbinu III. Kutoa uthibitisho.
Mshawshi atoe uthibitisho unaoonyesha ya kwamba ombi au lengo lake litatelelezeka bila ya vikwazo vingi. Mshawishi atoe uthibitisho pasipo na shaka ya kwamba atatoa "bidhaa" bora baada ya muda husika; baada ya ombi lake kukubaliwa na kutekelezeka.

Mshindani ashindanishe uthibitisho wake dhidi ya washindani wengine. Mshawishi ahakikishe anayosema au kutoa ni ya kweli na yanawezekana. Msahwishi aonyeshe uhusika au nafasi yake huku akitabasamu ili kukuza imani na urafiki. Pia mshawishi aonyeshe ya kwamba yupo tayari kutoa msaada wa ziada kama ikibidi kufanya hivyo.

Mbinu IV. Kuwasiliana kwa ufasaha.
Takribani watu wote wanapenda wakubalike na na kueleweka kadiri wanavyohisi ni sahihi, kwa kadiri ya hisia zao bila kujali jinsi wanavyowasiliana. Mshawishi anapaswa kujiuliza, je niwasilisheje ombi langu bila ya kumkwaza mshawishiwa?

Ili kufanya hivyo, mshawishi anapaswa kutumia mbinu za mawasiliano bora zilizoandika katika mada mbili zilizopita. Mshawishi atambue na kukwepa maneno ambayo huathiri hasi utu wa mtu au jamii husika kama yasipotumika kwa kuzingatia mazingiza na aina ya mazungumzo.

Mbinu V. Kukubaliana na mshawisiwa.
Takribani watu wote hupenda au huridhika kwa kuambiwa "nimekuelewa". Katika hili mshawishi ahakikishe anasikiliza kwa makini na kukubali mawazo yanayofanikisha ombi lake likubalike.
Mshawishi akubaliane pia mawazo kinzani kabla ya kukosoa au kutoa ufafanuzi. Kwa mfano, "unaweza kuwa sahihi lakini ni bora kama ingekuwa hivi......", "natambua hali halisi lakini nitafanya hivi....ili kuweka mambo sawa"

Mshawishi ahakikishe ya kwamba pindi ombi lake litapokubaliwa na kutekelezeka pande zote mbili zitafanikiwa; ili mshawishiwa akubali kutoa msaada. Mshawishiwa atatoa msaada na ushirikiano pale atakapohisi anafanya uamuzi sahihi.