Monday, December 26, 2011

KUZUNGUMZA KWA UFASAHA

Maneno ya heshima, yaliyotamkwa kwa ufasaha huamsha hisia na kufanikisha tafakari. Ili kufanikisha mazungumzo; mazungumzo ya siku kwa siku, mzungumzaji anapaswa kupanga mawazo yake kabla ya kuanza kuzungumza.
Mbali na hilo; yafuatayo ni muhimu kuzingatiwa:

1) Kujipanga.
Ni vyema kupanga mawazo au hoja kabla ya kuanza kuzungumza. Mzungumzaji anapaswa kuweka mawazo ya msingi mwanzoni; na yawe katika mtiririko. Hii hufanikisha ufahamu kwa upande wa pili.

2) Kukaa kimya.
Kama mzungumzaji anahisi atakayosema yatamkwaza mtu; kama mzungumzaji anayo hasira ni bora akae kimya. Maneno ni kama mawe, pindi yanaporushwa hayazuiliki. Mzungumzaji asitishe anayokusudia kusema mpaka hali itakaporuhusu.

3) Kuwa muungwana.
Mtu (mzungumzaji) anapaswa kujenga tabia ya kutoa hoja kwa lugha ya upole. Kuonyesha uungwana na heshima dhidi ya upande wa pili; hufanikisha mazungumzo kwa urahisi pia, kuleta muafaka.

4) Kuepuka maneno "haijatokea" na " ni kawaida".
Kauli nyingi zinazoundwa na maneno hayo huwa hazina ukweli; pia ni vigumu kuzithibitisha. Maneno hayo hujenga jazba na hutatiza mawasiliano. Mfano, "ni kawaida yako kunihadaa", "haijatokea ukakubali mawazo yangu", n.k

5) Kusifia.
Ingawaje mzungumzaji anaweza kukinzana na hoja; lakini si 100%. Mzungimzaji anapaswa kutambua umuhimu wa mada; na ambao unafanya upande wa pili kutetea. Kisha mzungumzaji aanze kwa kuunga mkono au kusifia; na baadaye kutoa hoja zake za kukinzana.

Kwa mfano, "ni kweli kabisa! Lugha na historia ni vielelezo kwa taifa lolote lile, lakini vitu hivyo havichangii kukuza uchumi wa taifa. Kwani hata siasa, amani n.k havitegemei lugha au historia bali uchumi wa nchi husika".

6) Kukubali udhaifu.
Mzungumzaji asiongee kwa kujiamini hata akasahau madhaifu yake au alipokosea. Kuongea kwa kupitiliza hufanya upande wa pili kuhisi unashambuliwa; hivyo unaweza kupata jazba na hatimaye kuanzisha vurugu.

Mawasiliano bora yanapaswa kuleta au kukuza maelewano; wakati mwingine upande mmoja unaweza kutoridhika kutokana na kukubali haraka. Hali hiyo inaweza kuondolewa kwa:

1) Kutokimbilia kusema "Ndio"
Watu hukubali ilimradi yaishe. Kama mtu anahisi anao wasiwasi anapaswa kusema " nipe muda kidogo ili nifikiri juu ya hilo". Hivyo kupata muda wa kutafakari na kutoa jibu sahihi.

2) Kueleza hali halisi.
Kama mtu hana ujasiri wa kukataa; anapaswa kuleza hali aliyonayo, au changamoto zinazomkabili. Hii husaidia kupunguza upinzani pindi atakaposema "Hapana".

3) Kutoa mapendekezo.
Kama mtu yupo katika wakati mgumu; au akatae au akubali ombi la kushiriki jambo fulani, anapaswa kutoa mbadala au majina ya watu wanaoweza kufanya shughuli husika kwa ufasaha.

4) Kutolumbana.
Kama moyo na nafsi vinamwambia mtu asema "Hapana", basi asianzishe malumbano ikiwa kutotoa kwa kina sababu za kukataa; hususani kama alikwisha kueleza hali aliyonayo.

Kama upande wa pili unasisitiza au kuendekeza malumbano; mzungumzaji atumie busara. Mfano anaweza kusema "Tafadhali, nawasihi msinihinikize ili nilumbane, malumbano hubomoa misingi. Jibu langu ni HAPANA"

Monday, December 19, 2011

KUSIKILIZA KWA MAKINI

Kufanikiwa au kutofanikiwa kunafanikishwa na ubora wa mawasiliano. Mawasiliano bora humwezesha mtu kueleweka na kukubalika. Mawasiliano ni muhimu kwa mahusiano baina ya; mtu na nafsi, mtu na mtu, mtu na familia, mtu na marafiki n.k

Maneno tunayozungumza na kusikia hupelekea; faraja au huzuni, usalama au hatari, kukubalika au kukalika n.k. Mbali na maneno, ujumbe wa ishara (kama vile kutazama, tabasamu, kuchezeha kichwa, matumizi ya mikono n.k) unamadhara makubwa sana au sawa na maneno/sauti.

KUSIKILIZA KWA UFASAHA.

Jambo moja na la muhimu katika mawasiliano ya sauti ni KUSILIZA. Binadamu amepewa mdomo mmoja na masikio mawili ili.......... Umakini katika kusikiliza hukuza na kuboresha mawasiliano, humsisimua mzungumzaji na kumhamasisha msikilizaji.

Kufanikisha usikivu fasaha; yafuatayo ni muhimu:
1) Kufahamu lugha ya ishara.
Kuwa makini na matumizi ya viungo vya mwili vya mzungumzaji; kama vile mikono, miguu, kichwa, tabasamu n.k. Lugha ya ishara hutumiwa na mzungumzaji kuboresha ujumbe anaotoa na hivyo kuboresha mawasiliano.

2) Kuondoa vikwazo.
Ili kusikiliza kwa ufasaha, mtu ajitahidi kadiri ya nguvu zake zote kuondoa mawazo na changamoto zinazomsonga. Vikwazo vinaweza kuwa kelele, mtazamo hasi juu ya ujumbe n.k. Kuondoa vikwazo kunawezeshwa na kuelekeza mawazo pia kujenga taswira juu ya kinachozungumzwa.

3) Kuomba ufafanuzi.
Kama mtu hajaelewa ipasavyo; kama anao wasiwasi au kama hajaelewa baadhi ya maneno n.k; anapswa kuomba ufafanuzi. Komba ufafanizi kuwe kwa lugha ya upole na unyenyekevu, lugha ya ukali kama vile "kwani hauna sauti? "unaniongelea kama mgonjwa?", "mimi sikusikii" n.k huondoa hari ya mzungumzaji; na hivyo kusitisha mazungumzo.

4) Kuthibitisha ulichosikia.
Mawasiliano yoyote hutegemea mwitikio. Ili kuhakikisha kuna uelewano hususani mambo ya msingi; inampasa msikilizaji kuthibitisha alichosikia na kuelewa, anapaswa kutoa mrejesho kwa mzungumzaji.
Mrejesho unaweza kuwa ni ufupisho wa ujumbe au ufafanuzi kwa kadiri ya alivyoelewa. Mfano, Mzungumzaji: nitafute kesho saa moja.
Msikilizaji: nikutafute kesho saa moja ya asubuhi?

5) Kutambua hisia za mzungumzaji.
Hisia au hali aliyonayo mzungumzaji husaidia kujua aina ya ujumbe anaoutoa. Mtu anapaswa kujua sababu za mzungumzaji kuongea kwa lugha ya ukali, lugha ya upole, kuangalia chini au pembeni, kuongea mfululizo n.k. Kujua hisia husaidia kuchukua hatua sahihi ili kuelewa ujumbe.
BINADAMU AMEPEWA MDOMO MMOJA NA MASKIO MAWILI ILI, ASIKILIZE ZAIDI YA KUZUNGUMZA.

Monday, December 12, 2011

UBUNIFU.....unaendelea.

Hatua Tatu za Kuongeza Ubunifu.
1) Kuamini inawezekana.
Kuamini jambo unaloona ni gumu; ya kwamba linawezekana huweka akili katika mwendo (njia) kuelekea kwenye suluhu. Kuamini huimarisha misingi na mazingira kuelekea "kusadikika".

Mtu anapaswa kuamini katika vitu vinavyoonekana ni vidogo na havina msaada kwa kuwa, siri za mafanikio hazitegemei mambo makubwa na maajabu ili kufanikiwa.

2) Kuondoa neno "HAIWEZEKANI" katika matamshi.
Mtu anaposema sentensi fulani juu ya jambo fulani mara kwa mara, uhalisia wa anayosema hujitokeza katika matendo.
Pale mtu anapotamka jambo fulani haliwezekani kabisa au zaidi ya ubora fulani, huifanya akili kutochukua hatua zozote au za ziada.
Wataalamu wa akili wanasema, analosema mtu ni matokeo ya mawazo yake, na kwa kiasi kikubwa humtokea. Waswahili wanasema, mdomo huumba.

3) Kukubali kupokea mawzo mapya.
Kufungua akili na kukubali kupokea mawazo mapya ni kama kuongeza mbolea na maji kwenye mimea.
Mtu anapaswa kuchambua mawazo mapya kwa kina, na kwa kadiri ya mahitaji, kudadisi ni kwa nini na kwa vipi mawazo husika hufanya kazi.

Jinsi Gani ya Kuishi mbinu za Ubunifu?
1) Kutenga muda na eneo tulivu kwa ajili ya tathmini ya kila siku, kabla na baada ya kulala.
2) Kujenga mazoea ya kutumia akili kuliko nguvu katika kukabili changamoto.
3) Kujenga mazoea ya kuishi kwa kufuata mawazo mapya na si kuishi kwa mazoea.
4) Kufanya kazi na mazoezi ambayo huimarisha na kukuza seli za akili. Mfano, michezo ya kompyuta.
5) Kukuza vionjo na silika; kuacha kushangaa bali kufanya jitihada ili kinachoonekana au kuwazwa kitimie.

Pia mtu anapaswa kufahamu ya kwamba:
¤ Kipawa asilia hakiletwi na milango mitano ya fahamu tu, bali akili fichika (subconsious mind).
¤ Akili fichika inafanikisha ujenzi wa taswira ambayo hupokewa na milango ya fahamu ili kufanikisha ukweli.
¤ Ubunifu wote huletwa na akili fichika.
¤ Ubunifu huonekana baada ya kuweka misingi na kuwaza chanya juu ya maisha.

Monday, December 5, 2011

UBUNIFU

Ubunifu ni nguvu mtu anayoibua kutoka katika taswira, taswira ya kitu kinachoonekana. Ubunifu ni bora kuliko kuwa na maarifa kwani, maarifa yana kikomo ili hali ubunifu hutapakaa ulimwenguni kote, huchochea mabadiliko yanayozaa maendeleo.

Ubunifu ni kiunganishi kati ya kipawa alichonacho mtu na mchango ulimwengu unaotoa kwa mtu husika. Kila kinachoonekana na taswira yake huwekwa katika akili, baada ya muda hutekelezeka kupitia ubunifu.

Kuna aina kuu mbili za ubunifu, nazo ni;
1) Ubunifu sanisi.
Katika aina hii ya ubunifu; mawazo, fikra na mipango aliyonayo mtu hupangwa katika mfumo mpya na tofauti. Aina hii hutegemea elimu na uzoefu alionao mtuu juu ya fani fulani.

2) Ubunifu kipaji.
Aina hii huvuta hisia na maono pamoja, hujengwa na jinsi mtu anavyopokea na kujibu yale anayoambiwa na mazingira. Ubunifu huu hautegemei uzoefu alionao mtu, bali elimu kidogo juu ya nyanja fulani. Ubunifu huu ndio chanzo cha ugunduzi.

Jinsi ya Kijenga Ubunifu.

1) Kuchangamsha akili kwa kusoma.
Kusoma ndio njia ya kuaminika yenye kukuza vipawa na siri zilizofichika katika katika dunia.
Mtu anapaswa kusoma yale yanayonfanya afikiri kwa kina, yanayotoa changamoto juu ya imani ya mtu na kuonyesha njia fasaha ya kufuata. Kumbuka siri za dunia zimefichwa kwenye maandishi.

2) Kuendeleza maboresho.
Kila umbo la kitu kinachoonekana ni maboresho yatokanayo na taswira, taswira aliyokuwa nayo mtu kichwani juu ya umbo hilo.

Uendelezwaji wa maboresho unawezeshwa na mbinu sahihi za kupumzisha akili na mwili. Kila siku mtu ahakikishe anapata mahali kwa ajili ya kupumzika; mahali ambapo atakaa kimya; kufunga macho na kupumua huku akifikiri juu ya mwenendo wa siku inayoisha, inayofuata na maisha kwa ujumla.

3) Kuwa na lengo.
Mtu anapaswa kuwa na lengo pamoja na azma juu ya maisha yake; juu ya maisha ayatakayo.
Ili kufanya hivyo, mtu anapaswa kuvunja vunja na kuunga upya vipande vianavyojenga lengo na azma husika. Kufanya huvyo husaidia kuona mapungufu na jinsi ya kuyakabili kabla au wakati wa utekelezaji wa lengo husika.

4) Kuwa na nguvu za umakini.
Nguvu za umakini huletwa na ridhaa na nidhamu ya mtu, ridhaa na nidhamu ya kutaka kutekeleza kile anachoamini ni sahihi kwa manufaa yake na ya jamii nzima. Nguvu za umakini huwezeshwa kwa utizamaji wa kina juu ya lengo, matendo, mienendo na hisia kuelekea ufanikishwaji wa azma husika.

5) Kumiliki vionjo.
Tamaa na jazba ni visafiria vianyotumiwa na wahujumu ili kuleta vikwazo; kukatisha tamaa; kuondoa imani; kujenga hofu na hatimaye kutochukua hatua sahihi. Hujuma hushambulia nafsi zaidi, hujuma zinaweza kupunguzwa na kuondoshwa kwa jitihada za mtu kumiliki mawazo yake, mienendo na mitizamo kwa hali ya juu.

Ubunifu uhamasishwa na tabia ya mtu ya kufikiri na kudadisi juu ya njia mbadala na sahihi ili kupata suluhu rahisi katika kutatua changamoto inayomkabili mtu binafsi na jamii kwa ujumla