Monday, April 30, 2012

MBINU ZA KUKUZA MAHUSIANO BAINA YA WATU

Mahusiano baina ya mtu na jamii yake ndiyo yanayomfanya mtu au afanikiwe au asifikiwe. Mahusiano baina ya mtu na mtu hutegemea uwezo wa mtu husika kushirikiana na jamii yake, kushikiana kunakojengwa na kutegemeana; na si kutegemea.

Ili kuboresha mahusiano, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:-

a) Upendo.
Ili mtu apendwe anapaswa kujipenda kwanza; kujipenda huanza kwa muonekano wa ndani na kisha wa nje. Kujipenda na kuwapenda watu wengine huonekana machoni mwa watu kupitia mienendo. Mtu anayewapenda wenzake hujitahidi kutoa msaada wa hali au mali ili wenzake watimize malengo yao.

b) Kukumbuka majina.
Mtu anapowaja watu anaowasiliana nao kwa majina. Au kuwaeleza jinsi anavyojua kule watokako huwatia watu faraja, kuwafanya wote wajione ni jamii moja. Pia huwafanya watu husika kujiona ni muhimu (wana thamiwa) miongoni mwa jamii.

c) Kukubali juhudi za watu.
Kukubali matunda (matokeo) ya kazi za watu wengine; kwa kuzipa thamani au ubora unaotakiwa hudhihirisha harakati za watu na kuwafanya waongeze matumaini na juhudi.

d) Kusikiliza kwa makini.
Kusikiliza ni bora zaidi ya kuongea katika nyakati nyingi. Mtu hudhihirisha jinsi gani habari yake inavyoungwa mkono kwa kadiri anavyosikilizwa. Hivyo kukuza hekima na uelewa wa msikilizaji. Baada ya kusiliza, mtu anapaswa kujibu kadiri ya busara na dhamira yake.

e) Kuruhusu hisia za watu.
Kuruhusu hisia, mtizamo, au mada kutoka kwa mtu/watu zijadiliwe humfanya mtu/watu kuzungumza kwa uhuru juu ya kufanikiwa na changamoto zao. Hivyo kumfanya mtu/ watu kufurahia uhusiano wao na jamii yao.

f) Kutia moyo.
Kuwatia moyo watu ambao hawakufanikiwa kiasi cha kuridhisha hutoa ahueni kwa mhanga. Yafaa kuwatendea watu kadiri ya mtu anavyotaka atendewe na wenzake. Kuwatakia watu heri husaidia kuepuka mawazo au kauli za kuwarudisha nyuma.

Thursday, April 26, 2012

KUFANIKISHA MAKUZI YA WATOTO KWA MZAZI MMOJA

Katika nyakati hizi, familia zilizochini ya uangalizi wa mzazi mmoja, hususani mama, zimeongezeka sana hata kufikia idadi sawa au zaidi ya familia zenye baba na mama katika jamii nyingi.
Kuna sababu nyingi zinazopelekea hali hii kama; kifo, utelekezwaji wa familia, kuhamishwa kikazi, masomo hususani elimu ya juu n.k

Changamoto zinazoambatana na malezi ya mzazi mmoja ni nyingi, ikiwamo; ufinyu wa kipato, kukosa ushirikiano kutoka kwa mzazi wa kufikia, upweke unaopelekea msongo mawazo n.k

Kukabili Jukumu.

Jukumu gumu katika malezi ni kelea mtoto/ watoto wachanga. Watoto wadogo wanahitaji uangalizi wa karibu. Hata hivyo jukumu hilo kubwa la malezi linaweza kupunguzwa kwa:

a) Kutafuta msaada.
Kutafuta msaada ni muhimu sana, hata kama mzazi husika anahisi ataweza kulea akiwa peke yake. Ni vigumu sana kulea mtoto bila msaada. Msaada unaweza kuombwa kutoka kwa ndugu, jirani, rafiki au mashirika yanayohusika na kulea watoto. Ikiwa kipato cha mzazi kinaruhusu mzazi anaweza kumwajiri yaya.

b) Kuweka mipango.
Mzazi anapaswa kupanga ratiba na kuhakikisha anaitekeleza. Watoto huwa na amani ikiwa wanajua saa ambayo baba/ mama atakayorudi. Pia ikiwa wanaona juhudi za mzazi katika kuwalea.

c) Kujibu maswali ya watoto.
Watoto huuliza maswali magumu sana, kwa kuwa watoto hupenda kudadisi juu ya yale wanayoyasikia. Watoto huuliza maswali juu ya baba/ mama ambaye hayupo. Mzazi husika hapaswi hata kidogo kupuuza maswali kutoka kwa watoto, bali atoe majibu sahihi na yenye ufafanuzi katika hali ya upole na unyenyekevu.

d) Kuzingatia maadili.
Mzazi anapaswa kuweka sheria na kanuni chache na zinazotekelezeka. Hii itawasaidia watoto kujiwekea mipaka maishani. Watoto wafundishwe kufanya kazi kwa ushirikiano tangu wakiwa wadogo. Mzazi awe na kiasi katika kutoa kazi na adhabu. Pia mzazi awaambie wasaidizi wake, juu ya matarajio yake kwa watoto wake.

e) Kuweka vipaumbele.
Ufinyu wa bajeti ni kikwazo kikubwa kwa familia ya mzazi mmoja. Mzazi anapaswa kuweka bajeti kadiri ya kipato chake. Ili kuepuka mzigo wa madeni, mzazi anapaswa kuepuka anasa. Pia mzazi awaambie watoto sababu za mapendekezo yao kutotekelezeka.

f) Kukaa na watoto.
Watoto huwa na furaha na amani ikiwa watakuwa na mahusiano mazuri na ya karibu baina yao na mzazi wao. Mzazi ahakikishe anapata muda kwa ajili ya kuongea, kusoma, kutembea, kuimba n.k na watoto. Mzazi asiruhusu watoto kuangalia TV kwa muda mwigi, hususani vipindi visivyo na umuhimu kwa watoto. Kufanya hivyo huimarisha familia.

g) Kujijali.
Mzazi ahakikishe anajali afya yake, kazi yake, jamii yake n.k. Kufanya hivyo kutasaidia kukuza ustawi wa roho na mwili. Mzazi atenge muda wa kupumzika na kuwasiliana na wadau wanaomsaidia katika malezi. Mzazi husika anapaswa kuchunga afya yake kwani, kama ikiwa ataugua hali ya familia itakuwa matatani.

Monday, April 9, 2012

MISINGI YA THAMANI YA MTU

Kila anachofanya mtu maishani au kuongea kinaakisi jinsi mtu anavyohisi, kile anachotamani, kile anachoamini ni stahili yake na jinsi gani anajali thamani yake popote pale alipo.
Kupata bahati, kuungwa mkono, kupata changamoto n.k ni matokeo ya jumbe zinazotolewa na mtu husika.

Thamani ya mtu inajengwa na mtu mwenyewe pale awapo; iwe kazini, kitaaluma, n.k. Ili kukuza na kuimarisha thamani ya mtu, yafuatayo ni muhimu:

1. Kujiheshimu.
Mtu anapaswa kujiheshimu (kuwa na adabu). Kujiheshimu kunahusisha akili, mwili na nafsi. Kujiheshimu hujidhihirisha jinsi mtu anavyovaa, anavyotembea, anavyowasiliana, anavyopanga mambo ya siku kwa siku n.k

2. Kujisafisha.
Mtu anapaswa kuwa na nafsi inayobubujika kama chemchemu. Nafsi ya mtu inapaswa kububujika upendo; upendo utakaomweka mtu mbali na chuki, kisasi n.k. Upendo ndio unamfanya mtu aombe msamaha kwa dhati na kujutia mabaya aliyowafanyia wenzake.

3. Kujipenda.
Kiungo muhimu katika ustawi wa mtu ni kujipenda. Watu wanaojipenda huwa na fikra na nyoyo nyepesi; huwaza chanya na kuvuta bahati.

Kujipenda na kutambua thamani yake humfanya mtu kufikiri madhara ya matendo yake na kuchukukua hatua stahiki. Kujitambua ndiko kunakomfanya mtu kuwaza madhara ya vipodozi, kukuza viungo, ulevi wa kupindukia, kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa n.k.

4. Kuchuja mawazo.
Mtu hujengwa na mawazo; mtu huishi kadiri awazavyo. Kitu kinachowatofautisha watu ni jinsi wanavyochuja na kufanyia kazi mawazo wanayoyapata kupitia milango ya fahamu.

Mtu hutenda mabaya ikiwa aliruhusu na kuhifadhi mawzo mabaya, vivyo hivyo, mtu hutenda mema ikiwa aliruhusu, kuhifadhi na kuchambua mawazo kwa mtizamo chanya.

5. Kuwasoma watu.
Njia bora ya kupata mafanikio ni kusoma kutoka kwa watu; kusoma jinsi watu walivyofanikisha mafanikio na thamani yao; jinsi walivyozishinda changamoto.
Mtu anapaswa kuwatafuta na kuwa karibu na watu wanaojiamini; kuwasikiliza (kusoma maandiko yao) na kufuatilia jinsi wanavyotenda.

6. Kuchagua vishawishi.
Ni muhumu sana kwa mtu kuwa makini na kile kinachomfanya achukue aina fulani ya maamuzi. Mtu anapaswa kuruhusu vishawishi vinavyompelekea kufanya maamuzi yanayojenga na si kubomoa.

Vishawishi vinaweza kuwa kauli za watu, mienendo ya watu n.k. Vishawishi vinapaswa kusaidia kuondoa au kupunguza changamoto za kimaisha kwa mtu au jamii husika.

7. Kuepuka mizani.
Mtu anapaswa kuwa makini sana pale anapo-oanisha mafanikio yake na ya mtu mwingine. Ni bora kujipima kupitia malengo; japo jamii haiwezi kufanya hivyo. Mara nyingi watu wanaolinganisha mafanikio yao na yale ya wengine huishia kukwazika na kujishusha thamani yao.

Mafanikio ya mtu si mizani sahihi kwa kuwa mtu (mizani) husika anaweza kupata mafanikio haraka kupitia misaada, bahati, kupata changamoto nyepesi n.k