Thursday, April 26, 2012

KUFANIKISHA MAKUZI YA WATOTO KWA MZAZI MMOJA

Katika nyakati hizi, familia zilizochini ya uangalizi wa mzazi mmoja, hususani mama, zimeongezeka sana hata kufikia idadi sawa au zaidi ya familia zenye baba na mama katika jamii nyingi.
Kuna sababu nyingi zinazopelekea hali hii kama; kifo, utelekezwaji wa familia, kuhamishwa kikazi, masomo hususani elimu ya juu n.k

Changamoto zinazoambatana na malezi ya mzazi mmoja ni nyingi, ikiwamo; ufinyu wa kipato, kukosa ushirikiano kutoka kwa mzazi wa kufikia, upweke unaopelekea msongo mawazo n.k

Kukabili Jukumu.

Jukumu gumu katika malezi ni kelea mtoto/ watoto wachanga. Watoto wadogo wanahitaji uangalizi wa karibu. Hata hivyo jukumu hilo kubwa la malezi linaweza kupunguzwa kwa:

a) Kutafuta msaada.
Kutafuta msaada ni muhimu sana, hata kama mzazi husika anahisi ataweza kulea akiwa peke yake. Ni vigumu sana kulea mtoto bila msaada. Msaada unaweza kuombwa kutoka kwa ndugu, jirani, rafiki au mashirika yanayohusika na kulea watoto. Ikiwa kipato cha mzazi kinaruhusu mzazi anaweza kumwajiri yaya.

b) Kuweka mipango.
Mzazi anapaswa kupanga ratiba na kuhakikisha anaitekeleza. Watoto huwa na amani ikiwa wanajua saa ambayo baba/ mama atakayorudi. Pia ikiwa wanaona juhudi za mzazi katika kuwalea.

c) Kujibu maswali ya watoto.
Watoto huuliza maswali magumu sana, kwa kuwa watoto hupenda kudadisi juu ya yale wanayoyasikia. Watoto huuliza maswali juu ya baba/ mama ambaye hayupo. Mzazi husika hapaswi hata kidogo kupuuza maswali kutoka kwa watoto, bali atoe majibu sahihi na yenye ufafanuzi katika hali ya upole na unyenyekevu.

d) Kuzingatia maadili.
Mzazi anapaswa kuweka sheria na kanuni chache na zinazotekelezeka. Hii itawasaidia watoto kujiwekea mipaka maishani. Watoto wafundishwe kufanya kazi kwa ushirikiano tangu wakiwa wadogo. Mzazi awe na kiasi katika kutoa kazi na adhabu. Pia mzazi awaambie wasaidizi wake, juu ya matarajio yake kwa watoto wake.

e) Kuweka vipaumbele.
Ufinyu wa bajeti ni kikwazo kikubwa kwa familia ya mzazi mmoja. Mzazi anapaswa kuweka bajeti kadiri ya kipato chake. Ili kuepuka mzigo wa madeni, mzazi anapaswa kuepuka anasa. Pia mzazi awaambie watoto sababu za mapendekezo yao kutotekelezeka.

f) Kukaa na watoto.
Watoto huwa na furaha na amani ikiwa watakuwa na mahusiano mazuri na ya karibu baina yao na mzazi wao. Mzazi ahakikishe anapata muda kwa ajili ya kuongea, kusoma, kutembea, kuimba n.k na watoto. Mzazi asiruhusu watoto kuangalia TV kwa muda mwigi, hususani vipindi visivyo na umuhimu kwa watoto. Kufanya hivyo huimarisha familia.

g) Kujijali.
Mzazi ahakikishe anajali afya yake, kazi yake, jamii yake n.k. Kufanya hivyo kutasaidia kukuza ustawi wa roho na mwili. Mzazi atenge muda wa kupumzika na kuwasiliana na wadau wanaomsaidia katika malezi. Mzazi husika anapaswa kuchunga afya yake kwani, kama ikiwa ataugua hali ya familia itakuwa matatani.

No comments:

Post a Comment