Monday, February 20, 2012

JINSI YA KUEPUKA MADHARA YA TABIA HATARISHI

Kuna watu wengi waliyomo hatarini kutokana na mienendo yao mibaya. Watu wengi hususani vijana wamo hatarini kutokana na kunywa pombe kupita kiasi, kuvuta sigara, kufanya ngono kiholele, kutumia madawa ya kulevya n.k

Watu hawa wanafahamu wanayoyafanya ni hatari kwao na kwa jamii yao. Ni hatari kwao kwa kuwa huhatarisha afya zao, huvuruga uhusiano wao na jamii, hupelekeea kifo (mfano Whitney Houston) n.k. Mienendo mibaya ni mzigo kwa jamii kwa kuwa; jamii inabeba jukumu la kulea wahanga, hupunguza nguvu kazi, hupelekea uvunjifu wa amani n.k

Baadhi ya waathirika wa mienendo hasi hujaribu kujinasua, wachache kati yao hufanikiwa, ila wengi kushindwa kwa kuwa au wao au jamii yao imeshindwa kutoa msaada fasaha. Ikiwa mtu anataka kuondokana na tabia chafu, anapaswa kufanya yafuatayo:

1. Kudhamiria kuacha kama lengo kuu.

Pamoja na kuwa na rundo la malengo ili kufikia maisha bora, mwathirika anapaswa kuamua kuacha tabia chafu kama lengo namba moja. Mtu anapaswa kupanga kwa maandishi siku na saa ya mwisho kufanya jambo hatarishi. Ili kutorudia tena, mtu apange atakachofanya ili kufuta mawazo mabaya.

Inafaa kuacha kidogokidogo (hatua kwa hatua), kusitisha utumiaji wa madawa ya kulevya ghafla kunaweza kusababisha kifo. Mtu anaweza kusoma machapisho juu ya madhara, kushiriki michezo, kujiunga katika vikundi vya watu wema, kuwa karibu na watu sahihi, kuomba ushauri kutoka kwa viongozi wa dini n.k. Malengo yatizame waliofanikiwa kuliko walioshindwa.

2. Kuwazia mafanikio.

Mtu anapaswa kujenga picha ya maisha 'safi'. Kuwaza jinsi atakavyopata ujasiri, jinsi atakavyowekeza nguvu na rasilimali anazotumia kulipia huduma hatarishi. Jinsi mtu husika atakavyokubalika na kuaminika katika jamii, atakavyofaidi utajiri wa jamii yake n.k.

3. Kutafuta njia rahisi na sahihi.

Inafaa kutafuta mbadala wa maisha na ambao ni salama. Hii ikihusisha jinsi ya kuishi na kupata msaada kutoka kwa; ndugu, jamaa, marafiki n.k ambao hawana imani na mwathirika.

Mara nyingi inabidi mtu abadili marafiki, maeneo aliyozoea kukaa (vijiwe), kukataa kusikiliza baadhi ya miziki. Mtu kamwe! asibadili tabia moja dhidi ya nyingine, mfano kunywa pombe kupindukia isiwe mbadala wa kufanya ngono.

4. Kukataa mitizamo hasi

Ili kufanikiwa, mtu anapaswa kukataa mitizamo hasi na misemo kama "kuacha haiwezekani, huu ni ulevi wa kawida, kila mtu ana ulevi wake" n.k. Mitizamo hiyo hasi hufutika kwa kujiambia mara kwa mara "naanza leo na nitapata mafanikio haraka, nitajitahidi kutunza afya yangu, mbona nanii..ameweza, hakuna lisilowezekana" n.k

5. Kujizawadia

Waswahili wanasema "raha jipe mwenyewe babu/ bibi....". Hivyo, ikiwa malengo yamefikiwa kwa kiasi fulani, mtu anapaswa kujipongeza. Zawadi inaweza kugharamiwa kwa fedha zilizokuwa zikitumiwa kulipia huduma angamizi. Mtu anaweza kujipongeza kwa kununua thamani, kutalii, kufanya sherehe na rafiki zake, kusaidia wasiojiweza, kusaidia waathirika wenzake n.k. Kujizawadia huleta uhalisia wa mfanikio ya siku za mbele.

6. Kutafuta msaada,

Watu wenye uwezo mdogo wa kufikiri husema "tabia ni kama ngozi (haibadiiki), kafiri haachi asili" n.k. Watu wanaotaka na kusababisha mabadiliko husema; tabia hubadilika kulingana na mazingira, utayari wa kuacha na msaada kutoka kwa jamii.

Ili kupata mafanikio ya haraka, mtu anapaswa kuomba ushauri kutoka kwa waliofanikiwa kuacha, wataalamu wa ushauri nasaha, viongozi wa dini, kujiunga na vikundi vya wanaharakati, kuonyesha kwa vitendo dhamira ya kutaka kuacha pamoja na kumshirikisha Mungu.

7. Kuweka rekodi ya mafanikio.

Mtu anapaswa kuweka rekodi kutokana na mafanikio aliyoyapata kutokana na malengo. Kabla ya kulala na kuamka, mtu asome mafanikio ya siku za nyuma. Huku akiweka mikakati juu ya kukabiliana na changamoto za siku kwa siku. Mikakati hiyo iwe ya kawaida na inayotekelezeka kulingana na mazingiza na uwezo wa mtu husika.

8. Kumiliki mihemko.

Watu hupata changamoto kuu siku chache baada ya kuacha iliyokuwa burudani yao. Wengi wao hupata homa, kuarisha, kutapika, kusikia kizunguzungu, kukosa usingizi n.k kwa kuwa wameacha kutumia madawa ya kulevya au pombe kali au sigara.

Bahati nzuri ni kwamba mtu hawezi kufa hususani kama atakula mlo kamili (hususani mboga mboga na matunda) pamoja na maji ya kutosha. Pia mawasiliano ya mara kwa mara kati ya mwathirika na mlezi wake ni muhimu sana. Inapendekezwa mlezi awe ni mtumiaji aliyefanikiwa kuacha.

MCHANGO WA JAMII NI MUHIMU SANA KATIKA KUOKOA WATU WALIOMO HATARINI, WENGI WAO HUTAKA KUACHA LAKINI JAMII HAITAKI. JAMII HAITAKI KWA KUENDELEA KUWABAGUA NA KUTOWAPA USHIRIKIANO.

No comments:

Post a Comment