Monday, February 13, 2012

HOFU KATIKA MAISHA

Hofu au ujasiri ni sehemu ya maisha ya mtu yeyote yule! Kiwango cha hofu au ujasiri hutofautiana kulingana na hisia za mtu. Hisia alizo nazo mtu hutegemea mawazo yake pamoja na mfumo wa kibailojia (homoni).

Hisia hasi za mtu hujengeka kwenye misingi ya woga, ujinga, kutojiamini, n.k. Kwa upande mwingine, hisia chanya hujengeka kwenye misingi ya ufahamu, imani, kujiamini, ujasiri, n.k.

Hofu aliyo nayo mtu yeyote huwa ni mchanganyiko au sehemu mawazo juu ya vitu sita ambavyo ni; kufilisika, kulaumiwa, ugonjwa, kuachwa na mpenzi, uzee na kupoteza maisha.
Mawazo juu vitu hivyo pamoja na suluhu zake ni kama ifuatavyo:

1. Hofu ya kufilisika.

Mtu anaweza kupata hofu ya kupoteza mali alizochuma (hata kupoteza kazi). Hofu hii huwakumba sana watu 'wanaoabudu' mali au hela. Watu hawa hutumia muda wao mwingi kutafuta mali ili kujiimarisha. Watu hawa hutegemea wingi wa mali zao ili kupata amani maishani.

Watu hupata hofu ya kufilisika mara baada ya kuona au kupewa mifano halisi ya watu waliokuwa na mali nyingi na sasa wamefilisika (wamefulia ile mbaya).

Hofu ya kupoteza mali inaweza kuepukwa kwa mtu kukataa kuwa mtumwa wa mali za dunia hii. Mtu anapaswa kuhakikisha anatumia mali na si mali zimtumie yeye. Kila mtu anapaswa kufahamu kwamba mali zake zinaweza kutoweka; kama itatokea awe tayari kuikubali hali hiyo ili aweze kuishinda. Pia ni vizuri kuwa na mahusiano mazuri na ndugu, jamaa na jamii inayomzunguka mtu

2. Hofu ya kulaumiwa.

Takribani watu wote hufanya au kuhakikisha utekelezaji mambo ili wapate sifa kutoka kwa jamii au kundi fulani la watu. Hivyo, hawajiandai kwa ajili ya kudharauliwa, kutusiwa n.k kutokana na maamuzi au yao au ya kundi. Kuogopa lawama kunawafanya watu waogope nafasi za uongozi, kutoa mawazo yao au kukosoa mambo yasiyo sahihi pale wanapotakiwa kufanya hivyo.

Kuogopa lawama kunaweza kuepukwa kwa kusikiliza na 'KUTATAA' yale mtu anayoambiwa juu ya ugumu wa jambo fulani. Mtu anapaswa kuamini mawazo aliyopewa na watu sahihi na anayotekeleza kulingana na hali yatampa tuzo.

Pia mtu afahamu watu wanaomkosoa wana; lengo gani, elimu, au uzoefu gani juu ya jambo husika, kama wanalenga kujenga au kubomoa n.k. Ikiwa watu wangeogopa lawana wasingefanya mambo ya maana kwao au kwa jamii zao. Lawama ni miongoni mwa mavuno, na lawama hazikwepeki.

3. Hofu ya ugonjwa.

Kuna nyakati fulani watu hupata hofu juu ya afya zao. Watu hupata hofu ya homa fulani kwa sababu ya kutokuwa na elimu juu ya ugonjwa, kuona watu walioathirika na ugonjwa fulani, kutofuata kanuni za afya wakati wa kufanya jambo fulani(mfano kushiriki ngono isiyo salama) n.k. Mtu anaweza kupatwa na mafua akahisi ana Kifua Kikuu, UKIMWI.....

Hofu ya homa au ugonjwa fulani inaweza kuondolewa kwa kutafuta habari sahihi za ugonjwa husika, kupata ushauri, kupima, kufuata kanuni bora za maisha kama; mapenzi salama, kunywa maji safi na salama, kufanya mazoezi ya viungo, kula mlo kamili n.k

4. Hofu ya kupoteza penzi.

Mtu anaweza kupata hofu juu ya mwenendo wa kimapenzi wa mpenzi wake baada ya kuambiwa maasi ya kimapenzi yanaoyafanywa na marafiki wa mpenzi wake, kusimuliwa mikasa ya kimapenzi, kuhisi kama anasalitiwa na mpenzi wake n.k. Hofu ya kupoteza penzi kumfanya mtu aamini mapenzi yananunuliwa au kuchukia jinsia nyingine.

Ili kuepuka hofu ya kupigwa chini, mtu anapaswa kuwa karibu na mpenzi wake ili apate kujua ukweli wa mambo, kukumbuka mambo mazuri aliyoyafanya na mpenzi wake, kuchuja anachoambiwa na marafiki zake kuhusu mpenzi wake n.k. Mtu anapaswa kuamini penzi halipotei; kwani penzi ni muendelezo usioisha wa hisia baina ya mtoaji na mpokeaji. Kuaminiana ni suluhu kuu ya hofu ya kupoteza penzi.

5. Hofu ya uzee.

Watoto wadogo hupenda kukua na kuitwa watu wazima. Watu wazima hukataa utu uzima na ambao ni lazima kwa viumbe hai wote. Watu huogopa uzee kwa kuwa wanaihisi watapoteza mvuto, watapitwa na 'wakati', kuzeeka kutawafanya kutofurahia maisha, kupatwa magonjwa ya uzeeni n.k

Kutokana na hofu ya kuzeeka, baadhi ya watu hupenda kuvaa, kuongea, kutumia vipodozi vya ngozi na nywele ili waonekane ni vijana. Baadhi ya watu hupenda kujihusisha na makundi ya vijana; na kuwaacha watu wa umri wao.

Ili kuepuka hofu ya kuzeeka, mtu anapswa kujua ya kwamba kuwa na umri mkubwa katika jamii ni hazina, ni dalili ya kukua, watu wazima huwa na busara na hekima kwa ajili ya kulea jamii (vijana) kwa kuwa mienendo yao bora na ya kuigwa. Uzee ni tunu kutoka kwa Mungu.

6. Hofu ya kupoteza maisha.

Baadhi ya watu hupata hofu ya kupoteza maisha baada ya: kuona mwili au jeneza la marehemu, kuona kaburi, kuugua kwa muda mrefu, kuwaza juu ya kufa. Watu wengine hupata hofu ya kufa baada ya kukata tamaa ya maisha, kukosa kazi, kukosa watu wa kuwalea, kutengwa na jamii, rafiki zao (hasa wa utotoni) kufariki, kusikia magonjwa ya ajabu na yasiyo na tiba yakiua watu wengi n.k

Hofu ya kupoteza maisha huwafanya baadhi ya watu kutotia bidii katika shughuli za uzalishaji mali, kuuza mali walizochuma au kufuja mali zao hatimaye wao au jamii inayowategemea huingia kwenye dimbwi la umasikini wa kupindukia.

Ili kuepuka hofu ya kufa, mtu anapswa kujua kufa ni sifa ya viumbe hai vyote; hata Yesu, Musa na manabii maarufu walikufa. Pia mtu anapokufa hubaki akitukuzwa kwa yale mema aliyosema na kutenda, kwa msimamo wake katika kuleta mabadiliko kwa familia au jamii yake. Mali alizochuma mtu wakati wa uhai wake zitawakilisha uwepo wake hapa duniani.
HOFU ZOTE NI HISIA ZA AKILI, IKIWA MTU ATAZIENDEKEZA ATAANGAMIA!!!...

No comments:

Post a Comment