Monday, February 27, 2012

KUTUNZA MGONJWA

Ni ukweli usiopingika ya kwamba, mgonjwa huwa na nafasi kubwa ya kupona au kupata nafuu haraka iwapo apata ushiriano wa kutosha kutoka kwa jamii inayomzunguka.

Pindi mtu anapofanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kugundulika kwamba anatatizo, taratibu za matibabu hufuata. Ikiwa mgonjwa atakosa ushirikiano kutoka kwa jamaa, rafiki, ndugu n.k zake hukumbwa na hofu, woga, mtizamo hasi n.k. Hivyo hupungua kinga ya mwili na hatimaye kupunguza uwezekano wa kupona kwa haraka.

Ikiwa mtu atathibitika ni mgonjwa, jamii inayomzunguka (muuguzaji) inapaswa kufanya yafuatayo ili kufanikisha uponyaji:

1. Kumsikiliza mgonjwa.

Si wagonjwa wote hupenda kuongea, ikiwa yupo, anapaswa kusikilizwa kwa makini na upendo. Ikiwa mgonjwa hapendi kuongea, yapaswa ajengewe mazingira ya upole na utulivu wa akili ili aongee kwa uwazi.

2. Kuongea juu ya ugonjwa.

Wakati muafaka ukifika, mazungumzo juu ya ugonjwa yanapaswa kufanyika. Mazungungumzo yanaweza kuhusu ukubwa wa ugonjwa katika jamii husika, dalili na matibabu. Mgonjwa anahitaji taarifa sahihi juu ya ugonjwa ili kujiandaa kiakili juu ya hatua zinazofuata. Pindi mgonjwa anapoomba maoni kutoka kwa mlezi, muuguzaji atumie busara ili kutomkwaza mgonjwa.

3. Kutodharau.

Ni kawaida kwa wagonjwa kulalamika, hata wengine kumlaumu daktari au Mungu. Katika hali hii, mgonjwa asijibu au kutoa ishara za dharau au kebehi. Muuguzaji ajitahidi kujua sababu za majibu au hisia za mgonjwa, huku akimfariji.

4. Kumsaidia mgonjwa kazi.

Iwapo mgonjwa anapenda kusoma, kuandika, kuangalia TV, n.k asaidiwe ili atimize azma yake haraka iwezekanavyo. Yote kwa yote, mgonjwa anapaswa kusaidiwa majukumu ya siku kwa siku kama vile kufua nguo, kunyoosha nguo n.k ili kufanikisha usafi na kumwondolea mawazo.

5. Kuwezesha mawasilaino.

Muuguzaji anapaswa kumuunganisha mgonjwa na rafiki au ndugu zake. Ili kufanikisha mawasiliano, muuguzaji anapaswa kutoa taarifa juu ya hali ya mgonjwa kwa watu wa karibu. Kutoa taarifa kunarahisisha mawasiliano, pia huwezesha upatikanaji wa misaada kwa haraka.

6. Kusimamia utekelezwaji wa magizo.

Muuguzaji anapaswa kupokea na kusimamia kwa makini maagizo kutoka kwa nesi au daktari. Muuguzaji anapaswa kusimamia maagizo juu ya utumiaji wa dawa, ufanyaji wa mazoezi (kutembea), huduma ya kwanza n.k. Ili kurahisisha utekelezwaji wa maagizo, muuguzaji anapaswa kutunza maagizo yote anayoambiwa na daktari au nesi. Ikibidi kuwe na mawasiliano (simu) baina ya muuguzaji na Muuguzi.

Pia ni vizuri kumuomba Mungu kwa pamoja (mgonjwa na muuguzaji) kwani tafiti zimethibitisha kwamba wagonjwa hupata faraja na kupata nafuu/ kupona haraka pale sala zinapofanyika, sala za kuwaombea wapone haraka.
Neno muuguzaji linawakilisha mtu au watu wanaomhudumia mgonjwa siku kwa siku (iwe nyumbani au hosptali), na wala si Nesi.

No comments:

Post a Comment