Monday, June 11, 2012

MBINU ZA KUWINDA AJIRA (2)

3. VYANZO VYA MAARIFA
Ili kupata kazi, mtu anapaswa kuwa tofauti na waombaji wengine wote. Ili kuwa tofauti, pamoja na mambo mengine, maarifa ni kitu muhimu. Kuna vyanzo vitatu vya maarifa:

3 (a) Elimu ya Darasani.
Hii ni elimu mtu aipatayo kutoka kwa Wakufunzi rasmi, katika mazingira ya shule; elimu itolewayo katika mfumo rasmi wa elimu. Kwa mfano, Sekondari, Vyuo vya Ufundi n.k. Elimu hii ni ya kufuta ujinga, kwani inao mchango kidogo sana katika kufanikiwa kwa mtu.

3 (b) Elimu ya mitaani.
Hii ni elimu itoknayo na mwingiliano wa mtu na jamii anayoishi. Kwa mfano; kuhudhuria makongamano, kuwasikiliza watu waliofanikiwa, kufanya majadiliano n.k. Elimu hii humpa mtu maarifa sahihi ya kukusanya na kutumia rasilimali zinazomzunguka kwa ufasaha zaidi. Elimu hii ndio iliyowawezesha watu wengi kupata mafanikio.

3 (c) Elimu ya vitabuni.
Elimu hii hutokana na kusoma vitabu vyenye mlengo chanya. Vitabu vinamwezesha mtu kupata mawazo na ushauri kutoka kwa watu maarufu na waliofanikiwa; ambapo isingelikuwa watu hao waliweka mawazo yao katika vitabu, ingekuwa vigumu sana hata kusalimiana nao.

Kupitia vitabu, mtu anapata kujua watu maarufu walifanikiwaje kufanya biashara, kuajiriwa, kuongoza n.k, hivyo na yeye achukue uamuzi gani kulingana na hali inayomsonga.
vyanzo vote ni bora; ila Elimu ya darasani na elimu ya mitaani ni vyanzo sahihi zaidi vya maarifa, kwani ni vya urahisi na uhakika, na vinaelezea hali halisi ya maisha.

4. KUFAHAMU MAHITAJI YA MWAJIRI.

Kabla ya kwenda kuomba kazi kwenye taasisi au shirika (ikiwa kama kazi haikutangazwa), mtu anaweza kufanya uchunguzi juu ya ndoto, mikakati na changamoto zinazoikumba taasisi husika. Kila mwajiri anatafuta:

4 (a) Mtu atakayeongeza thamani kwenye kampuni..
Waajiri hutafuta mfanyakazi atakayeongeza ubora wa huduma au bidhaa huku akipunguza changamoto zinazoikabili kampuni. Waajiri wanataka watu waoweza kuiokoa kampuni isiangukie kwenye msukosuko wa kiuchumi.

Linapokuja suala la kuomba kazi, Watanzania wanamatizo makuu matano nayo:
¤ uwezo mdogo wa kuongea na kuandika lugha ya Kiingereza, kwani Kiingereza ndio lugha inayowaunganisha watu wengi;
¤ kutojiamini, Watanzania wengi hawawezi kutetea kile wanachokiamini kuwa ni sahihi hasa baada ya kupewa changamoto;
¤ kutoa huduma mbaya kwa wateja, kukosa kujua na kumudu mbinu za kuwahudumia wateja hufanya biashara nyingi kufilisika;
¤ kushindwa kujiwasilisha; watu wengi hawajui wavae nini, watembeeje, waongee nini na wapi n.k. Hili ni tatizo kubwa hata kwa viongozi;
¤ uwezo mdogo wa kutumia vifaa pamoja na sayansi na teknolojia. Takribani 3% ya Watanzania ndio wanaoweza kutumia huduma za mtandao wa Intaneti kama; barua pepe, nukushi, Facebook, Twitter, YouTube n.k

4 (b) Watu halisia.
Waajiri hawataki ubora wa vyeti au watu wanaoweza kujieleza bila ya matendo, bali watu wachapa kazi.
Waajiri hawataki watu wenye mipango anuwai, bali mipango inayotekelezeka.
Itaendelea.....

No comments:

Post a Comment