Monday, July 2, 2012

MBINU ZA KUEPUKA TAMAA MBAYA

Tamaa mbaya ni hali ya kutaka kumiliki mali zaidi ya mahitaji halisi; hali ya mtu kutotaka kuridhika, kwa mfano, kurudia rudia chakula ili hali watu wengine wanakosa. Tasnia ya matangazo hutumia mwanya huu kwa kutoa matangazo bora yanayoteka akili za watu na kuwaamuru watu wagombanie bidhaa ili wapate furaha, kwa lengo la kuvutia wateja.

Yafuatayo ni madhara ya tamaa mbaya:

¤ Kukosa kujitawala. Watu wenye tamaa mbaya hawawezi kumiliki hisia zao, hawawezi kutawala malengo yao; huyumbishwa na pepo za ushindani.
¤ Kushindwa kuweka malengo. Watu wenye tamaa mbaya hawawezi kuweka kipimo halisi cha malengo yao, wengi huvutwa na malengo au mipango ya wenzao ili wapate kuwashinda.
¤ Kuingia kwenye madeni. Kutaka kujilimbikizia mali kunawafanya watu kukopa kwa pupa na kulipia mambo yasiyo na tija ya kweli kwao. Madeni hayo hupelekea mtu kudhalilika na kufilisiwa baada ya kushindwa kulipa.

¤ Kukiuka maadili. Tamaa zilizopitiliza huongeza uwezekano wa mtu kukiuka miiko ya kazi au maadili ya jamii yake kama vile; udanganyifu, wizi, utapeli n.k
¤ Kuvunja mahusiano ya mtu. Tamaa mbaya huleta mtafaruku hususani pale mtu anapoingilia na kuhatarisha maslahi ya mwenzie au jamii yake. Kwa mfano kusogeza mpaka wa shamba au kiwanja.
¤ Kuleta tabia hatarishi. Tamaa mbaya hupelekea tabia hatarishi kama kukosa usingizi, kukosa hamu ya kula, hasira n.k. Hali hizo hupelekea kupungua kwa kinga ya mwili na uzito na hatimaye magonjwa.

Jinsi ya Kukwepa Tamaa Mbaya

1. kukubali mafanikio. Mtu anapaswa kutizama ubora wa mali alizo nazo, ikilinganishwa na awali, bila ya kuangalia nani anamiliki nini. Kuridhia mafanikio ni silaha muhimu sana.

2. Kujitathimini na kuweka malengo. Mtu anapaswa kujiweka mbali na hisia mbaya; hisia za kukosa, na kujiangalia kwa kina mahitaji halisi. Mahitaji halisi huwekwa kulingana na uwezo wa mtu husika.

3. Kukwepa kujithaminisha na mtu.
Mtu asifadhaike kutokana na hatua za mafanikio jamaa zake walizopiga, kwani kila mtu anapata fursa tofauti tofauti na kwa nyakati tofauti. Pia kamwe mafanikio hayawezi kufanana, kwani mafanikioa ni kama vidole.

4. Kuwasaidia wengine. Kuwawazia na kuwasaidia watu wanaokosa mahitaji ya msingi kama chakula, makazi na mavazi husaidia kupunguza tamaa mbaya kwa kiasi kikubwa, hii ni ngumu sana kwa watu wenye wivu. Ni muhimu kuwasaidia yatima, wajane, wazee wasio na walezi, vilema n.k.
Katika shida na tamaabu zao.

5. Kumwomba Mungu.
Mtu anapaswa kumomba Mungu kadiri ya imani yake, kwani kila mtu anaamini Mungu yupo. Mtu anapaswa kumwomba Mungu ampatie afya, amani, utulivu wa akili na nafsi na mkate wa kila siku; kwani vitu hiyo ni bora kuliko kumiliki mali zenye thamani kubwa kama tani kadhaa za dhahabu.

No comments:

Post a Comment