Monday, July 16, 2012

MBINU ZA KUUKABILI USHIRIKINA

Ushirikina ni hali ya kuamini kuna haja ya kuwa na nguvu ya ziada kutoka kwa mtu au nafsi ili kuweza kufanikisha jambo fulani. Kwa mfano, kuamini kuna haja ya kufanya kafara (kuchinja na kumwaga damu ya mtu au mfugo) ili kuweza kupata kazi. Imani za ushirikina ni maarufu katika jamii na sehemu mbalimbali duniani.

Imani za ushirikina ni kukwazo kikubwa kwa jamii nyingi kwa kuwa:

Hupunguza nafasi za kusoma. Kuamini katika ushirikina kutochukua jitihada za kusoma ili kupata suluhu juu ya changamoto zinazoikabili jamii husika. Kwa mfano, kutegemea ushirikara kunaweza kuwazuia wafanyabiashara kutofanya tafiti mpya juu ya mwenendo wa biashara, hatimaye hufilisika.

Huongeza mzigo. Kuamini ushirikina kunamfanya mtu kuishi akiwa amevaa vitu mbalimbali ili kutimiza malengo, mfano, kuvaa irizi. Vitu hivyo kwa ujumla wake huongeza mzigo katika mwili wa mtu.

Huzuia malengo kutimia. Watu wanaoamini ushirikina huacha kufanya mambo waliyoyapanga kwa kuwa masharti hayaruhusu. Kwa mfano, mtu anayekwenda kufanya biashara fulani, akikutana na bundi asubuhi, kwa kuwa anaamini bundi ni ishara ya mkosi, mtu huyo hurudi nyumbani, hivyo, kuacha kufanya biashara kwa siku husika.

Huleta mfadhaiko. Ikiwa kama mtu anaamini irizi ndio kinga yake, kwa bahati mbaya akasahau kuvaa irizi siku fulani, siku hiyo ataishi kwa wasiwasi na hofu siku nzima. Au mtu akiamini mzee fulani ni mchawi, na akakutana nae, mtu huyo hupata mfadhaiko kwa kuogopa atakuwa amelogwa.

Huongeza changamoto za kimaisha. Kutokana na kuamini ushirikina, mshirikina hujinyima fursa nyingi za kusonga mbele. Kwa mfano, mtu anayeamini ya kwamba jirani yake ni mchawi, mtu huyo hukatisha mawasiliano na jiarani yake, pia, mtu huyo anaweza kuwaacha watoto wake bila ya uangalizi wowote kwa kuogopa wanawe watalogwa na jirani yake.

Mbinu za Kukabili Imani na Madhara ya Ishirikina.

Inawezekana kabisa kuepa ushirikina, na mtu husika asidhurike kwa kufanya yafuatayo:
Kutumia takwimu.
Ili kukwepa mawazo au uhusishwaji wa tukio fulani na imani za kishirikina, mtu anapaswa kusoma takwimu dalili n.kuhusu tukio husika. Kwa mfano, ili kutohusisha kifo na ushirikina, mtu anapaswakusoma takwimu kuhusiana na kifo cha mtu husika.

Kutafuta ushauri.
Ili kupunguza uwezekano wa madhara fulani kutokea mtu anapaswa kuomba na kufuata ushauri kutoka kwa wataalamu. Kwa mfano, ili kukwepa hasara katika biashara, mfanyabiashara anapaswa kutafuta na kutekeleza ushauri kutoka kwa wataalamu wa biashara kabla na wakati wa biashara husika.

Kujaribu nguvu ya ushirikina.
Ikiwa kama mtu anaamini ya kwamba bila ya kuwa na irizi hawezi kufanya vizuri katika mchezo, mtu huyo afanye maandalizi sahihi huku akiwa na imani ya kuwa atafanikiwa bila ya kukumia kizizi. Pia mtu huyo anaangalie kama mara zote anazotumia irizi je anakiwa? Kama kizizi ndio suluhu ya kufanikiwa, je kuna haja gani ya kufanya mazoezi?

Kumwamini Mwenyezi Mungu.
Kila kitu (kinachoonekana au kisichoonekana) kimeumbwa na Mungu. Mungu ndiye mtawala wa kila kitu. Ikiwa kama Mwenyezi Mungu ameweza kuumba kila kitu, je atashindwaje kushinda hila za ushirikina?

Ikiwa kama mambo hayaendi kama mtu alivyopanga, haimaanishi ya kwamba Mungu ameshindwa, bali kwa namna moja au nyingine Mungu anatoa somo. Kwani kutokana na matatizo yanayomkabili mtu, ndipo watu huamini na kutii uwepo wa Mungu. Kupiga magoti kwa Mungu na kufanya kazi kwa bidii ndiko kunakoleta suluhu ya kudumu.

Achilia mbali mila na tamaduni, imani za ushirikina zinachukua nafasi kubwa katika jamii kwa kuwa watu hawana suluhu dhidi ya changamoto zinazowakabili. Kwa mfano, kukosekana kwa elimu na tiba juu ya ugonjwa fulani unaosababisha vifo vingi, huwafanya watu katika jamii husika kuhusisha ugonjwa huo moja kwa na imani za ushirikina.

No comments:

Post a Comment