Monday, August 6, 2012

VIASHIRIA VYA BAHATI

Watu wengi hufikiri ya kwamba bahati (nzuri au mbaya) hujijia tu, haibashiriki na ni vigumu kuzuia. Hiyo ni kwa kuwa hawajui maana halisi ya bahati. Ikiwa kama mtu hajui maana halisi ya bahati ni vigumu kuitawala. Waswahili wanasema "mtembea bure si sawa na mkaa bure" pia "bahati ya mbwa ipo kwenye miguu yake".

Bahati ni kujitambua dhidi ya uhalisia. Bahati ni kuwa na hisia chanya juu ya tukio au jambo fulani. Mtu mwenye hisia chanya huona kila kitu kinamtumikia (kila kitu kinamsadia kufanikiwa), kwa upande mwingine, mtu mwenye hisia hasi huona kila kitu kinampiga vita; kila kitu huonekana ni kikwazo.

Kiasi cha imani (nguvu itokayo ndani) huamua kiwango cha hisia na bahati ya mtu. Mtu anapofanya jambo lolote pasipo imani, kufanya jambo kwa mashaka makubwa, huwa na uwezekano mkubwa kufanya makosa ya kizembe hivyo kujiweka katika nafasi kubwa ya kungeza vikwazo au kukosa kabisa kile alichotaka. Pindi mtu anapojiamini kwa kiasi kikubwa ndipo uwezekano wa bahati (kufanikiwa) unapoongezeka.

Kwa kiasi fulani, bahati hutegemea maarifa. Mtu mwenye maarifa hufanya kazi kwa uhuru. Ni vigumu kutenganisha bahati na maarifa; kwani ili kufanya kitu kwa usahihi uwezo wa mtu husika kufuata sheria na kanuni ipasavyo unahitajika.

Kwa kuwa bahati hutegemea imani, mtu anapaswa kuwa makini na kiwango cha imani yake wakati anapofanya jambo lolote lile. Ikiwa kama kiwango cha imani ni kidogo, yafaa kusitisha kufanya jambo hilo, au kufanya hatua kwa hatua na kwa umakini mkubwa kama haiwezekani kusitisha shughuli husika.

Watu wanaolazimisha kufanya jambo bila ya imani nalo hujikuta wakifanya makosa bila ya kujitambua, kusahau hatua za kufuata, kushindwa kujitetea pindi wanapotakiwa kijitetea, hivyo kubaki wakijilaumu kwa kujisemea "nina bahati mbaya".

Kukosa umakini kimawazo huwafanya watu kudharau mambo ya msingi; kujikuta wakifanya mambo wasiyotayatarajia kisha kutokufanikiwa. Ili kuongeza nafasi ya bahati ya kufanikiwa yapaswa kuwekeza kimawazo, kushirikisha maarifa kwenye kazi ifanyikayo kwa wakati husika. Kuwekeza kimawazo husaidia kutumia rasilimali kwa ufanisi zaidi.

Takribani watu wote (wanasayansi mashuhuri, wafanyabiashara wakubwa, wasomi n.k) waliofanikiwa, walifanikiwa kwa kuwa kiwango chao cha imani kilikuwa juu. Kufanya kazi bila ya i tiketi ya kushindwa. Mtu anayetaka bahati nzuri huchagua mtizamo chanya, mtizamo chanya huongeza nishati na kusadia jitihada za kufanikiwa.

Kila mtu anayo nafasi ya kufanikiwa, watu wengi hawajui maana na jinsi ya kulinda nafasi wanazopata katika maisha. Bahati nzuri ipo, na kila mtu anao uwezo wa kuitawala. Kwa kulitambua hilo, hakuna haja ya kuogopa kufanya jambo lolote kwa kuwa hakuna bahati mbaya.

No comments:

Post a Comment